Na MILKAH RIGHA ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Wednesday, February 22 2012 at 19:3Kwa Mukhtasari
Ndege hiyo, iliyozinduliwa na Kampuni ya ndege ya Kenya Airways (KQ) kwa ushirikiano na kampuni ya KLM Royal Dutch, mnamo Jumanne, itakuwa ya kwanza kabisa itakayotoka Uchina moja kwa moja hadi Afrika.
WAFANYIBIASHARA wa Kenya wataweza kusafirisha jumla ya tani 120 za bidhaa zao kwa wakati mmoja, kufuatia kuzinduliwa kwa ndege mpya ya mizigo nchini.
Ndege hiyo, iliyozinduliwa na Kampuni ya ndege ya Kenya Airways (KQ) kwa ushirikiano na kampuni ya KLM Royal Dutch, mnamo Jumanne, itakuwa ya kwanza kabisa itakayotoka Uchina moja kwa moja hadi Afrika.
Huduma za ndege hiyo ya mizigo aina ya Boeing 747-400F, inayomilikiwa na shirika la Martin Air, ambalo ni sehemu ya shirika la ndege la Air France KLM, zitatolewa na KQ kwa ushirikiano na KLM Cargo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Airways, Bw Titus Naikuni, alisema kwamba kampuni hiyo inanuia kununua ndege nyingine mbili, katika kipindi cha pili cha mwaka huu. Aliongeza kwamba zitasaidia pakubwa kufungua nafasi za kazi kwa watu wengi nchini.
“Tunatarajia ndege nyingine 12 kama hizi katika kipindi cha miaka 10 ijayo, na tuna hakika kwamba hiyo itasaidia kubuni nafasi za kazi na kupunguza idadi ya vijana wasio na ajira,” alisema Bw Naikuni.
Aidha aliongeza kwamba, Kenya itasafirisha maua na chakula hadi Uchina kupitia kwa huduma hii huku ikipokea vifaa vya kielektroniki, vipuri vya mashine, simu na bidhaa nyingine kutoka Uchina.
Bidhaa za ujenzi zitasafirishwa kutoka Amsterdam hadi Uchina. Aidha inalenga kusaidia katika kukua kwa uchumi wa Kenya na mataifa mengine ya Afrika, na pia kupunguza kutegemea sehemu ya mizigo ya ndege za kawaida za abiria, ambazo zimekuwa zikitegemewa licha ya uwezo wake mdodo wa kubeba mizigo.
“Biashara baina ya Uchina na Kenya inazidi kupanuka, hivyo ndege hii itasaidia sana kuimarisha uhusiano mkuu kati ya nchi hizi mbili,” alisema Meneja wa Mizigo wa Kampuni ya Martinair Cargo, Camiel Eurlings.
Ndege hiyo inatarajiwa kuhudumu kati ya Amsterdam-Guangzhou (Uchina)- Nairobi na kurudi Amsterdam.
Vilevile, inatarajiwa kufanya safari zake kutoka Nairobi kupitia mji wa Lagos, Nigeriac kabla ya kuenda katikia Uwanja wa Ndege wa Amsterdam, Uholanzi, kuanzia Mei mwaka huu.
Ndege hii itafanya safari mbili kamilifu kati ya miji hii mitatu kwa wiki.
Kwa sasa, huduma ya mizigo ya KQ imekuwa ikiletea shirika hili jumla ya asilimia 8-9 ya mapato yake na inatarajiwa kuongeza mapato haya hadi asilimia 15, katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Na DANIEL MULE ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 21 2012 at 20:50Kwa Mukhtasari
Total Kenya imezindua rasmi taa zinazotumia nishati kutoka kwa jua ili kuchangia katika juhudi za kusaidia uhifadhi wa mazingira.
KAMPUNI ya kuuza mafuta ya Total imezindua rasmi taa zinazotumia nishati kutoka kwa jua ili kuchangia katika kutunza mazingira.
Akizungumza katika warsha ya uzinduzi huo Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa Total nchini, Bw Alexis Vovk, alisema hiyo ni mojawapo ya hatua za kampuni hiyo kutunza mazingira.
“Total imekuwa ikijihusisha na upanzi wa miti na kutoa mafunzo kuhusu usalama barabarani kwa muda. Sasa tumeamua kuuza taa zinazotumia nishati kutoka kwa jua ili kupunguza idadi ya watu wanaotegemea mafuta kuwashia taa au kuendesha jenereta,” alisema Bw Vovk.
Alisema kuwa taa hizo kwa jina 'Total Sola’ zimekuwa zikifanyiwa majaribio tangu 2010 na sasa imebainika kuwa kiwango chake ni cha hali ya juu.
Bw Vovk aliongeza kuwa watu wa viwango vyote vilizingatiwa katika shughuli ya uundaji wa taa hizo.
“Kuna taa za kuanzia Sh999 hadi Sh28,000. Kila taa ni tofauti na ina manufaa yake tofauti na nyingine. Mtu anaweza kununua taa yoyote kulingana na mapato na mahitaji yake,” alisema Bw Vovk.
Masaa manane
Alisema taa aina ya S10 inayouzwa kwa Sh999 inaweza kutoa mwangaza kwa muda wa saa nane baada ya kuwekwa kwenye jua kwa saa sita pekee.
“Taa inayotarajiwa kufanya vyema zaidi ni ile ya S250 inayouzwa kwa Sh3,400. Taa hiyo inatoa mwangaza mara kumi zaidi ya taa za kawaida na inaweza kutumika kuongeza nishati kwenye betri za simu,” alisema Bw Vovk.
Naibu Rais wa Total ulimwenguni katika kitengo cha kutunza mazingira, Bi Manoelle Lepoube, alisema kuwa kuna haja kubwa ya kutafuta njia badala za kuzalisha nishati.
“Ili kujitayarisha kwa siku za usoni, ni muhimu kupanua mawazo yetu kulenga mbinu nyingine zitakazotuwezesha kukimu mahitaji huku tukijua hatuvipunji vizazi vijavyo,” alisema Bi Lepoube.
Na PETER MWAI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Friday, February 17 2012 at 20:2Kwa Mukhtasari
Faida hiyo ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na Sh4.2 bilioni iliyopata katika kipindi cha mwaka 2010. Faida kwenye kila hisa iliongezeka Sh4.03 mnamo 2010 hadi Sh5.55.
KAMPUNI ya East African Breweries ilipata faida ya Sh4.9 bilioni katika kipindi cha nusu mwaka kilichomalizika Desemba 31.
Hili ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na Sh4.2 bilioni iliyopata katika kipindi cha mwaka 2010 kwa mujibu wa matokeo ya kifedha yaliyotolewa jana.
Matokeo hayo yametolewa siku moja tu baada ya kustaafu kwa mwenyekiti wa bodi wa muda mrefu, Bw Jeremiah G Kiereini, aliyehudumu kwa miaka 24 tangu mwaka wa 1988.
Amekuwa akihusika sana kwenye kampuni nyingi tangu kuondoka kutoka serikali ya Rais Mstaafu Daniel Moi ambapo alikuwa Katibu Mkuu, 1984.
Mrithi wa Kiereini
Wadhifa wake katika EABL, umechukuliwa na Bw Charles Muchene ambaye alikuwa mshauri mkuu katika kampuni ya PricewaterhouseCoopers.
Faida ya EABL kwenye kila hisa iliongezeka Sh4.03 mnamo 2010 hadi Sh5.55.
Mgao wa faida ambao utalipwa wenye hisa umeongezeka kutoka Sh345 milioni nusu ya mwaka iliyotangulia hadi Sh546 milioni.
Katika kipindi hicho, EABl ilinunua mali na mashini zenye thamani ya Sh3 bilioni, na pia kununua hisa za NCI kwa Sh21 bilioni.
Na MATHIAS RINGA ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 14 2012 at 19:39Kwa Mukhtasari
Mwenyekiti wa Baraza la Tana River asema endapo Mumias Sugar itaanzisha ukuzaji miwa katika chemchemi hiyo, huenda wakulima zaidi 50,000 wa mifugo wakaathirika kutokana na kukosa maeneo ya kulisha mifugo.
BARAZA la Tana River limepinga vikali mpango wa Kampuni ya Sukari ya Mumias (MSC), kuanzisha mradi wa uzalishaji miwa katika maeneo ya chemchemi ya mto Tana.
Mwenyekiti wa baraza hilo Salim Golo Gure aliomba kampuni hiyo ifutulie mbali mradi wa kulima miwa katika chemchemi ya mto Tana.
Bw Gure alisema endapo MSC itaanzisha ukuzaji miwa katika chemchemi hiyo, huenda wakulima zaidi 50,000 wa mifugo wakaathirika kutokana na kukosa maeneo ya kulisha mifugo.
Mbali na wafugaji kutoka wilaya za Tana River na Tana Delta, alisema, wafugaji kutoka Mkoa wa Kaskazini Mashariki pia hulisha mifugo yao katika chemchemi hiyo.
Eneo la chemchemi
“Eneo la chemchemi ya Tana, lina umuhimu mkubwa kwa wakazi wa Tana Delta na Tana River kwani mifugo yote hupata malisho na vile vile maji,” alisema.
“Baraza la Tana River linaomba kampuni ya MSC ifutilie mbali mpango wa ulimaji miwa katika maeneo haya ya mto Tana mara moja,” akasema.
“Wakazi wapatao 50,000 ambao ni wafugaji watapoteza riziki zao za kila siku ikiwa mpango huo utatimizwa,” akaonya.
Bw Gure aidha, alionya kwamba fujo huenda zikazuka iwapo kampuni shughuli hiyo ya ukuzaji. Wafugaji wa Tana River, Bw Basa Ware, pia alipinga mradi huo wa miwa akisema kwamba itatatiza wafugaji.
Bw Ware alidokeza kuwa wakati wa ukame, ni eneo hilo pekee ambalo hutumika kwa ulishaji wa mifugo kutoka Tana River na Mkoa wa Kaskazini Mashariki.
“Nyakati za ukame mifugo kutoka maeneo ya Tana na hata kutoka maeneo ya Mkoa wa Kaskazini Mashariki hulisha katika eneo hilo,” akaarifu.
Hivi majuzi, Mkurugenzi Mkuu wa MSC, Bw Kidero aliarifu kuwa kampuni hiyo pamoja na Halmashauri ya Maendeleo ya Mito Tana na Athi (TARDA) itakuza miwa katikahektari 16,000 kwenye sehemu hiyo.katika maeneo ya chemchemi ya Tana.
Na JOHN SHILITSA ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 14 2012 at 19:35Kwa Mukhtasari
Wachangiaji wasema adhabu ya Sh800 ni juu sana na wakataka Waziri wa Huduma za Matibabu, Prof Anyang Nyong’o kuingilia kati.
SERIKALI imeshauriwa kuondoa adhabu inayotozwa kwa wanaochangia kwa Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Matibabu (NHIF), wanapochelewa kulipa.
Wachangiaji ambao hawajaariwa walisema adhabu ya Sh800 ni juu sana na wakataka Waziri wa Huduma za Matibabu, Prof Anyang Nyong’o kuingilia kati.
“Wengi wetu huenda tukakosa kuwa katika bima hiyo ya matibabu,” alisema Bi Angela Mukongolo, ambaye ni mke wa nyumbani.
Uchunguzi wa Taifa Leo katika afisi za NHIF Mumias, ulionyesha kuwa idadi kubwa ya wanaokosa kulipa kwa wakati ni watu ambao hawajaajiriwa. Wengi wao ni wahudumu wa bodaboda na wakulima wakujikimu.
Bi Mukongolo alisema adhabu hiyo inastahili kuangaliwa upya kwa sababu madhumuni ya bima hiyo, hayatafaulu ikiwa wanaolengwa wanawekewa masharti wasiyoweza kutimiza. Wanaokosa kulipa hutozwa kiasi hicho cha pesa kila mwezi kando na mchango wao wa Sh160 kwa mwezi.
Walioathiriwa walidai kuwa wanadaiwa na NHIF kati ya Sh3,500 na Sh7,000 kwa sababu ya kutozwa adhabu hiyo.
Na PETER MWAI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 14 2012 at 19:30Kwa Mukhtasari
Waziri Shitanda asema wengi wa waliopewa kandarasi wamekuwa wakikosa kuwajibika na kushindwa kukamilisha miradi yao.
WAZIRI wa Nyumba Soita Shitanda ameonya wanakandarasi wa humu nchini kwamba hawatabembelezwa katika utoaji wa kandarasi za Serikali.
Waziri alisema wengi wa waliopewa kandarasi wamekuwa wakikosa kuwajibika na kushindwa kukamilisha miradi yao.
Alikuwa akiongea mtaani Kileleshwa wakati wa kukabidhiwa rasmi kwa nyumba 105 zilizojengwa na Shirika la Kitaifa la Nyumba (NHC) kwa gharama ya Sh800 milioni.
“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumetoa kandarasi kwa kampuni nne za humu nchini. Ni moja tu iliyomaliza kazi yake. Nyingine tulilazimika kuanza kutafuta watu wa kuzimaliza,” akasema Bw Shitanda.
Mradi huo wa Kileleshwa Park Appartment ulipewa kampuni ya China Wu Yi kutoka Uchina ambayo ilishirikiana na Enderman Properties.
Ujenzi ulimalizika katika kipindi cha miezi 15 pekee. Kampuni za humu nchini huchukua hadi miaka minne kumaliza ujenzi wa nyumba 200.
“Hata kama tungependa sana kukuza kampuni na wawekezaji wa humu nchini, lazima watoe huduma bora na kushindana na China Wu Yi na wengineo,” akasema waziri.
Ujenzi katika kaunti
Aliwatahadharisha wazinduke na kujiimarisha mapema akisema kuna kandarasi nyingi za ujenzi ambazo zitachipuka katika ngazi za kaunti baada ya kuanza kutekelezwa kwa ugatuzi.
“Shida iko kwenye wawekezaji wa humu nchini na hasa Waafrika. Lazima wajikakamue,” akaongeza.
Nyumba hizo za Kileleshwa zimejengwa katika ardhi ya ekari 3.55 iliyomilikiwa awali na Shirika la Reli la Kenya (KRC).
Ardhi hiyo ilikabidhiwa NHC kama sehemu ya malipo ya deni lililodaiwa na shirika hilo miaka minne iliyopita.
Na PETER MWAI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Friday, February 10 2012 at 19:31Kwa Mukhtasari
SERIKALI imebadilisha deni ambalo inadai Shirika la Reli la Kenya (KRC) kuwa mchango wake wa kifedha (mtaji) na kuimarisha udhibiti wake katika shirika hilo.
SERIKALI imebadilisha deni ambalo inadai Shirika la Reli la Kenya (KRC) kuwa mchango wake wa kifedha (mtaji) na kuimarisha udhibiti wake katika shirika hilo.
Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha shughuli za shirika hilo ambalo linategemewa kutekeleza jukumu muhimu Kenya inapojiandaa kutimiza Ruwaza ya 2030. Baraza la Mawaziri liliidhinisha hatua hiyo Alhamisi kwenye mkutano ulioandaliwa chini ya uongozi wa Rais Mwai Kibaki katika Ikulu ya Nairobi.
“Mawaziri wameidhinisha kubadilishwa kwa hesabu ya kifedha ya Shirika la Reli la Kenya. Hii itahusisha kubadilishwa kwa deni ambalo Serikali inalidai shirika hilo kuwa mtaji. Hatua hii itaondolea shirika hilo mzigo na kuliwezesha kuwa na msingi thabiti,” ilisema taarifa ya Chumba cha Habari cha Rais (PPS).
Mkopo
Kufikia Novemba 2005, serikali ilikuwa imelikopesha shirika hilo Sh14 bilioni. Kwa jumla, shirika lilikuwa likidaiwa Sh20 bilioni na wadeni mbalimbali.
Shirika hilo humiliki na kusimamia miundo msingi ya reli ambayo hukodisha kwa wahudumu wa reli.
Nchini, mfano ni kampuni ya Rift Valley Railways (RVR) ambayo ilikabidhiwa kandarasi ya kusimamia uchukuzi wa reli Kenya na Uganda kwa muda wa miaka 25 kuanzia 200.
Kuiamrisha huduma
Ujenzi wa reli ya kutumiwa kuimarisha huduma Nairobi unapangiwa kugharimu Sh16 bilioni, huku ule wa kujengwa reli ya kisasa kote nchini ukipangiwa kugharimu Sh320 bilioni.
Uchukuzi wa gari moshi una mchango mkubwa na muhimu katika kufanikisha uchukuzi wa mizigo na bidhaa nchini.
Katika jiji la Nairobi, unapangiwa kupunguza msongamano na pia uharibifu unaotokana na kupitishiwa kwa mizigo mizito kwenye barabara za lami.
Kadhalika, serikali imekuwa na mipango ya kubadilisha kabisa mfumo wa reli nchini kufikia mwaka wa 2050.
Na JOYCE BOKE ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Friday, February 10 2012 at 19:27Kwa Mukhtasari
Mamia ya wazazi wanamiminika maduka ya sare mjini Nakuru huku msimu wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka jana ukiwa umeshika kasi.
HUKU msimu wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa wanafunzi waliofanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka jana ukiwa umeshika kasi, mamia ya wazazi walimiminika maduka ya sare mjini Nakuru.
Foleni ndefu zilishuhudiwa madukani humo hadi nje na barabani huku baadhi ya wazazi na wanao wakikosa kupata sare hizo kutokana na uhaba. Katika duka la Shah Outfitters na lile la Nakuru Wool shopping ni wanafunzi tu walioruhusiwa kuingia ndani ilihali wazazi walilazimika kuongoja nje ili kuzuia msongamano.
Wazazi walilalamika kuwa walilazimika kupanga foleni kwa hadi masaa manne na walipofika ndani wakajulishwa kuwa sare za mashule yao hazikuwepo au kuwa zilikuwa zimenunuliwa zikaisha. Walinzi walikuwa na wakati mgumu kumudu idadi hiyo na kuwatuliza wazazi waliokuwa na hasira baada ya kukosa sare za wanao.
Msimamizi wa mauzo katika duka la Nakuru Wool Shopping Martin Jaoko alisema kuwa uhaba huo umetokana na mashule kubadilisha sare zao bila kuwajulisha wauzaji na kucheleweshwa kwa sare hizo kutoka kwa makampuni ya utengenezaji.
Na PETER MWAI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Tuesday, February 7 2012 at 20:16Kwa Mukhtasari
Mteja anaweza kununua gesi ya kupikia ya Sh50. Gesi hiyo inauzwa kwenye mitungi ya kilo moja, na inaruhusu mnunuzi kununua kiasi chochote cha gesi anachohitaji.
KAMPUNI ya Premier Gas imezindua huduma mpya ya gesi ya kupikia kwa jina Pima Gas inayowezesha wateja kununua gesi ya Sh50 pekee.
Gesi hiyo tayari inauzwa maeneo kadha jijini Nairobi na inatarajiwa kufika maeneo yote ya nchi katika kipindi cha miaka miwili.
Gesi hiyo inauzwa kwenye mitungi ya kilo moja, na inaruhusu mnunuzi kununua kiasi chochote cha gesi anachohitaji.
Akiongea wakati wa kuzinduliwa kwa huduma hiyo jana, Meneja Mkurugenzi wa Premier Gas, Bw Michael Momanyi alisema huduma hiyo imetokana na haja ya kuhudumia watu maskini.
“Mtungi wake ni mdogo na rahisi kubeba. Utasaidia sana wanawake na watoto ambao hutumia muda mwingi wakitafuta kuni au makaa,” akasema.
Mtungi wa gesi, pamoja na jiko lake unauzwa Sh2,000. Kwa Sh50, mteja anaweza kupata gesi inayokaribia robo kilo. Gesi hiyo kwa sasa inauzwa Embakasi, Pipeline, Kawangware na Rongai.
Na MWANGI MUIRURI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Friday, February 3 2012 at 22:4Kwa Mukhtasari
Jina ambalo sarafu hiyo ya Afrika Mashariki inapendekezwa kuitwa ni Afri-Shilling.
HUENDA Jumuiya ya Afrika Mashariki izindue sarafu mpya itakayotumika kwa pamoja na mataifa husika karibuni.
Sarafu hiyo itakuwa ikidhibitiwa kama ile inayotumika kwa pamoja katika bara Uropa kwa Jina Euro.
Jina ambalo sarafu hiyo ya Afrika Mashariki inapendekezwa kuitwa ni Afri-Shilling.
Uwezekano wa uzinduzi huo unatarajiwa kuchipuka katika Mkutano wa viongozi wa Mataifa hayo ya Jumuiya utakaofanyika mjini Arusha, Tanzania mwezi wa Aprili mwaka huu.
Mataifa hayo yanajumuisha Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda na Burundi na ambayo yameafikiana kuwa sarafu itarahisisha biashara miongoni mwao.
Aidha, sarafu hiyo itasaidia katika kupambana na mfumko wa bei za bidhaa katika biashara huru kati yao ambayo husababishwa na uyumbaji wa sarafu tofauti wanazotumia.
Kulingana na ripoti ya Wizara ya Afrika Mashariki, hatua kubwa zimepigwa kufanikisha juhudi hizo.
Aidha, hatua hiyo itayawezesha waekezaji wa bara nyingine kurahisishiwa awamu nyingi za kukadiria hesabu za sarafu katika uekezaji kwani hiyo itakuwa ndiyo kigezo cha ukadiriaji huo kote jimboni.
Na LUCAS BARASA ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Friday, February 3 2012 at 22:33Kwa Mukhtasari
Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni wa Uingereza, Bw William Hague, amefurahishwa kwa kurejea kwa utulivu Mogadishu na sehemu nyingine za nchi hiyo.
UINGEREZA imeitaka jamii ya kimataifa itumie fursa ya usalama Somalia kuimarisha uthabiti nchini humo.
Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni wa Uingereza, Bw William Hague, aliyefika nchini jana alisema nchi yake imefurahishwa kwa kurejea kwa utulivu Mogadishu na sehemu nyingine za nchi hiyo.
Hii imetokana na juhudi za walinda usalama wa Muungano wa Afrika (Amisom), wale wa Serikali ya Mpito ya Somalia (TFG) na Majeshi ya Ulinzi ya Kenya (KDF) dhidi ya wanamgambo wa kundi la Al-Shabaab.
“Usalama umeimarika. Nilijionea mwenyewe jana (Alhamisi),” akasema. Alikuwa mjini Mogadishu kabla ya kutua Kenya kukutana na Rais Mwai Kibaki.
Alisema raia wa Somalia wanatamani amani baada ya miaka mingi ya mapigano. Alisema Uingereza itatetea kuunganishwa kwa majeshi ya Kenya na yale ya Amisom katika mkutano wa baraza la Umoja wa Mataifa.
Na RICHARD MUNGUTI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Friday, February 3 2012 at 21:57Kwa Mukhtasari
KESHIA watatu na walinzi wawili Alhamisi walishtakiwa kuiba zaidi Sh54milioni kutoka benki ya Barclays (BBK), tawi la Eastleigh mwezi
KESHIA watatu na walinzi wawili Alhamisi walishtakiwa kuiba zaidi Sh54milioni kutoka benki ya Barclays (BBK), tawi la Eastleigh mwezi jana.
Wizi wa mamilioni hayo ya pesa uliwazuzua wengi kwa vile polisi walidai hakukuwa na uvunjaji wowote.
Waliofikishwa mbele ya hakimu mkuu wa Nairobi Bi Esther Maina ni Richard Kimanthi Kiilu, Fredrick Omondi Okoth na Stephen Githinji waliokuwa wameajiriwa kama makeshia katika benki hiyo.
Walikana kuiba pesa hizo.
Watatu hao walishtakiwa pamoja na walinzi wawili Jacob Kioko Mbutu na Japheth Kiprop Tanui.
Kiilu, Okoth na Githinji walidaiwa waliiba Sh54milioni, dola za Marekani 42,000 na Euro 16,900 katika benki ya BBK tawi la Eastleigh kaunti ya Nairobi mnamo Januari 29.
Kioko na Tanui walikana shtaka la kukataa kutumia uwezo walio nao kama walinzi kuzuia wizi huo.
Wote waliomba korti iwaachilie kwa dhamana.
“Tunaomba hii korti iwaachilie kwa dhamana washukiwa. Washtakiwa ni raia wa Kenya na kamwe hawawezi kutoroka na kuacha mali zao humu nchini,” wakili mmoja akaieleza korti.
Kiongozi wa mashtaka Suparitenda Onesmus Towett alimsihi hakimu atilie maanani kiwango cha pesa kilichoibwa.
“Naomba korti iwaamuru washukiwa waweke dhamana ya kiwango cha juu cha pesa kwa vile pesa zilizoibwa ni zaidi ya Sh54milioni na hazijapatikana bado,” akasema Supt Towett.
Bi Maina aliamuru kila mmoja wa washtakiwa hao watano alipe Sh5milioni pesa tasilimu kabla ya kuachiliwa kutoka korokoroni alikoamuru wazuiliwe.
Pia aliamuru watakaoshindwa kulipa pesa hizo wawasilishe kortini dhamana mbili za Sh5milioni.
Kesi hiyo itasikizwa Machi 19.
Katika mahakama hiyo hiyo mkongwe wa miaka 81 anayedaiwa alipokea Sh11.5milioni alimweleza Bi Maina hawezi kupata dhamana ya Sh1milioni aliyopewa Januari 12, aliposhtakiwa.
“Mimi nilikuwa mtumishi wa Serikali. Nilistaafu baada ya kuitumikia nchi hii zaidi ya miaka 30. Ukweli ni kwamba siwezi kupata dhamana hiyo. Naomba unipunguzie,” akasema Edward Singe Amisi.
Babu Amisi anakabiliwa na mashtaka nane ya kupokea pesa kwa njia ya undanganyifu akijifanya alikuwa na shamba la kuuza.
Akaiambia mahakama aliposhtakiwa,” mimi nilitayarisha hati ya ugavi wa shamba.
Lakini hakimu akamweleza zaidi , “ sikiza vile nimekueleza utapewa muda wa kujitetea kesi itakapoanza kusikizwa. Kwa sasa tafadhali jibu ikiwa ulipokea pesa kwa njia ya undanganyifu ama ulitengeneza hati za umiliki wa shamba.”
Akasema mshtakiwa, “sijui sababu ya kulundikiwa mashtaka nane ilhali mimi nilitayarisha hati moja ya shamba. katika eneo.”
Bi Maina atatoa uamuzi wake Feburuari 7, 2012.Bi Maina atatoa uamuzi wake Feburuari 7.
Na Na JOHN KIMWERE ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Thursday, February 2 2012 at 23:17Kwa Mukhtasari
Wabunge hao wametishia kuungana na wenyeji wa mtaa wa Mukuru kwa Njenga, kufanya maandamano hadi katika afisi ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw George Saitoti.
WABUNGE watano wakiongozwa na mawaziri wasaidizi, Bw Ferdinard Waititu na Bi Wavinya Ndeti, wamempatia kamshina wa Polisi, Bw Mathew Iteere, hadi kesho kutia nguvuni polisi waliohusika na mauaji Mukuru.
Wabunge hao wametishia kuungana na wenyeji wa mtaa wa Mukuru kwa Njenga, kufanya maandamano hadi katika afisi ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw George Saitoti, iwapo Iteere atashindwa kuwakamata waliohusika na mauaji hayo.
Wiki jana, wakazi watatu wa mtaa huu walipigwa risasi katika ubomoaji ambao ambao ulisitishwa punda baada ya kuanza.
Wabunge hao walisema hayo, kwenye mkutano uliofanyika katika uwanja wa eneo kulikofanyika ubomoaji huo Jumatano jioni.
Bw Waititu aidha, alikuwa ameandamana na Wabunge Gideon Mbuvi, John Mututho na Yusuf Hassan.
“Tutashirikiana na wenzangu Bw Waititu na Bi Ndeti kugharamia mazishi ya waliokufa kwenye ghasia hizo,” alisema Bw Sonko.
Aliongezea kwamba watahakikisha vijana wote waliokamatwa wakati huo wameachiliwa.
Aidha wabunge hao waliwakikishia wenyeji kwamba hakuna ubomoaji utafanyika eneo hilo.
Na MWANGI MUIRURI ( email Mwandishi)
Imepakiwa - Thursday, February 2 2012 at 23:50Kwa Mukhtasari
Biashara ya dawa haramu yakadiriwa kuwa ya thamani ya Sh11 bilioni kwa kila mwaka, hali ambayo inazua wasiwasi wa maafa ambayo yangezuiliwa ikiwa dawa mwafaka zingetumika.
MAISHA ya maelfu ya Wakenya yamo hatarini kufuatia taarifa kwamba dawa bandia zinasambazwa na wafanyabiashara walaghai nchini.
Dawa hizo ambazo ni pamoja na zile zilizopitwa na wakati ambazo yasemekana huuziwa wauguzi katika baadhi ya hospitali za kibinafsi, maduka ya kuuza dawa na pia katika zahanati nyingine za Serikali.
Kiwango cha biashara hiyo haramu kinakadiriwa kuwa ya thamani ya Sh11 bilioni kwa kila mwaka, hali ambayo inazua wasiwasi wa maafa ambayo yangezuiliwa ikiwa dawa mwafaka zingetumika.
Ripoti ya Shirika la Kimataifa la The Global Counterfeit Medicine Tracker (GCMT 2010) inasema kuwa wafanyabiashara hao wameunda mtandao wenye mizizi katika mataifa ya Afrika Mashariki.
Ripoti hiyo inatilia mkazo msimamo wa Serikali kuwa biashara hiyo kwa kweli inaendelezwa hapa nchini na imekuwa ikiweka mikakati ya kuizima.
Tayari, Serikali imepiga marufuku ya kuingizwa madawa nchini kupitia maeneo ambayo hayasajiliwa rasmi.
Aidha, imekuwa ikivamia hospitali na maduka ya matibabu na kuamrisha kufungwa kwa yale ambayo hayajaidhinishwa kuhudumu.
Katika biashara hiyo, waagizaji wa dawa na ambao ni memba wa mtandao huo hata huibiwa dawa katika hospitali za nchi jirani na kisha, zinapofika hapa nchini, zinauziwa umma na nyingine kuuzwa nje ya nchi.
“Mtandao huo huendeshwa na watu wafidhuli na ambao ni wakora ambao kuhonga baadhi ya maafisa wa Ushuru, wale wa usalama na wenye kulinda mipaka ya nchi,” yasema.
Aidha, ripoti hiyo imedai kuwa, baadhi ya maafisa wa idara ya afya wanashiriki biashara hiyo haramu kwa huhonga baadhi ya wabunge ili wasiunde sheria mwafaka za kusambaratisha biashara hiyo haramu.
“Magenge hayo hujua kuficha shughuli zao kwani wao huanzisha biashara halali lakini ndani ya biashara hizo huwa na shughuli hizo za haramu,” ripoti hiyo yasema.
Kufuatia biashara hiyo, wagonjwa wengi wanaendelea kudhoofika kiafya licha ya kuwa chini ya mpango wa madawa.
Wanaohofiwa zaidi kuangamizwa na jinamizi hili la ufisadi ni watoto wachanga ambao mara kwa mara huwa wakihitaji madawa kutibu maradhi mbalimbali.
Wananchi nao wanakemewa kwa kutokuwa makinifu katika matumizi ya dawa na huwa hawatafuti ushauri wa madaktari wanapoamua kununua dawa.
“Hatua hii ya mtu kuamua kujitambua anaugua wapi na ni dawa gani anafaa kununua kumefanya mtandao huo nafasi ya kunawiri,” ripoti hiyo yaonya.
Wauzaji wa dawa hizo hutumia mbinu ya bei kuuza dawa zao haramu kwa kumpa mteja nafasi ya kujichagulia dawa.
Imepakiwa - Friday, January 27 2012 at 12:44
Kwa Mukhtasari
Bw Kenyatta ang'atuka kutoka wadhifa wa Waziri wa Fedha lakini abaki kuwa Naibu Waziri Mkuu. Francis Muthaura ang'atuka kutoka nyadhifa za Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri
Na PETER MWAI
WASHUKIWA wawili wa ghasia za baada ya uchaguzi, Mabw Uhuru Kenyatta na Francis Muthaura wameng’atuka kutoka nyadhifa zao serikalini kufuatia shinikizo kali.
Hii ni baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kuthibitisha mashtaka dhidi yao Jumatatu.
Bw Kenyatta alijiuzulu kutoka wadhifa wa Waziri wa Fedha, wadhifa alioushikilia tangu 2009.
Lakini katika hatua ya kushangaza, alikataa kuachilia wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu.
Bw Muthaura aliondoka kutoka nyadhifa za Mkuu wa Utumishi wa Umma na Katibu wa Baraza la Mawaziri.
Hatua hiyo ilitangazwa rasmi na Chumba cha Habari cha Rais (PPS) baada ya Rais Kibaki kujulishwa na kukubali uamuzi wao.
“Rais amekubali uamuzi wa Uhuru Kenyatta kujiuzulu kutoka wadhifa wa Waziri wa Fedha. Hata hivyo, atabaki kuwa Naibu Waziri Mkuu kuambatana na Katiba,” ilisema taarifa ya PPS.
Rais aliteua Bw Robinson Githae, ambaye ni Waziri wa Ustawi wa Jiji la Nairobi, kushikilia Wizara ya Fedha kama kaimu waziri.
Aliyekuwa Katibu wa Wizara ya Utawala wa Mkoa na Usalama, Bw Francis Kimemia, naye aliteuliwa kushikilia nyadhifa zilizoshikiliwa na Bw Muthaura.
“Bw Mutea Iringo atakuwa Kaimu Katibu wa Wizara ya Utawala wa Mkoa na Usalama wa Ndani,” ilisema taarifa ya PPS.
Kabla ya kuteuliwa kwake, Bw Iringo alikuwa naibu katibu katika wizara hiyo ya usalama.
Shinikizo zilikuwa zimepanda kutoka kwa wanasiasa, mawakili na watu wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuwataka wawili hao waondoke serikalini.
Hii ni kuambatana na Sura ya Sita ya Katiba kuhusu maadili ambayo inasema mtu hafai kushikilia wadhifa wowote wa umma ikiwa mienendo yake ni ya kutiliwa shaka.
Waliotaka wang’atuke walisema kesi hizo zinakosesha wananchi imani katika utendakazi wao.
Waziri wa Haki na Sheria Mutula Kilonzo alikuwa awali amesema sharti wawili hao wajiuzulu ikiwa mashtaka dhidi yao yatathibitishwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria cha Kenya (LSK), Bw Kenneth Akide, alisema mashtaka yanayowakabili “ndiyo mabaya zaidi kuwahi kusikika katika sheria,” na hivyo hawafai kuendelea kuhudumu.
“Katiba na Kenya mpya inanuia kwa kina cha moyo wake uongozi mwadilifu,” akasema Bw Akide.
Aliyekuwa mwenyekiti wa LSK, Dkt Gibson Kamau Kuria, na Mbunge wa Imenti ya Kati, Bw Gitobu Imanyara, pia waliunga mkono msimamo huo.
“Wakiendelea kuhudumu serikalini watahujumu uhalali wa matendo ya Serikali pakubwa,” Bw Kuria akasema.
Lakini Mkuu wa Sheria, Prof Githu Muigai alikuwa ameeleza maoni tofauti na kusema wawili hao hawafai kushinikizwa wajiuzulu kabla ya kujulikana ikiwa watakata rufaa dhidi ya uamuzi wa ICC, na rufaa hizo kuamuliwa.
Kufuatia kujiuzulu kwa Bw Kenyatta na Bw Muthaura, mjadala sasa huenda ukaangazia suala la ikiwa Bw Kenyatta na mshukiwa mwingine, Bw William Ruto (mbunge wa Eldoret Kaskazi) wanafaa kuwania urais. Vile vile, huenda wengi wakahoji kuhusu uhalali wa kuendelea kuhudumu kama Naibu Waziri Mkuu ambao ni wadhifa wa umma.
Kabla ya uamuzi wa majaji, wawili hao walikuwa wameapa kuendelea na ndoto zao licha ya pingamizi kutoka pande mbalimbali.
Bw Kilonzo (Waziri wa Haki) amekuwa akisema hawapaswi kuruhusiwa kuwania urais.
Maoni ya Bw Mutula yanakinzana na ya Tume ya Utekelezaji Katiba (CIC) iliyosema hakuna sheria inayozuia washtakiwa hao kuwania urais, hata kesi iliyo Hague.