http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

Mkosa si mwana

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na SOUDY PODOS (TALL G

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:51

Kwa Muhtasari

Mkono utaniunga, na kuitia saini
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

 

NIMWEJITOA mhanga, kuwambia wenye kani,
Fika hata kwa mganga, na ramli kubaini,
Mkono utaniunga, na kuitia saini,
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi,

Ni mengi anayotenda, na wengi wanamsema,
Ayatenda yenye inda, yasio leta salama,
Ni wengi wanamuinda, ayatendayo si mema,
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

ziwe nyingi tendekeza, akitakacho chukua
Hutaki kumchukiza, na mwana silie ngowa
Atakuja kukukweza, ujute na kuzaliwa
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Humkanyi akosapo, eti ni mwana mdogo
Kumi na tano alipo, asema nawe kwa kogo
Hajaupata mchapo, wala utamu wa hogo
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Akitumwa hatumiki, alisemalo ni basi
Nenda kanunue hiki, dukani kwa Almasi
Atakujibu sitaki, isiyo na wasiwasi
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Alitakalo hufanya, lafaradhi au suna
Ukimuonya la njia, takupa jibu la kina
Tamaka kwa kusikia, jibu alilolinena
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Jina lake Athumani, na mkofu ushingoni
Rangi zimo vidoleni, na kidani kifuani
Nywele kachoma kichwani, na nshi ameauni
Usimlaumu mwana, makosa niye mzazi

Jina lake Mariamu, tamati ni kituoni
Si halali si haramu, atendayo si yakini
Baa nyumba ya kudumu, anayo kesha mjini
Usimlaumu mwana ,makosa niye mzazi

SOUDY PODOS (TALL GUY)
DUKUDUKU LA ROHONI
BIN SUDI FARM
GANDA MALINDI

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com