http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

Mnafiki ni mfitini

Imepakiwa Wednesday November 5 2014 | Na NYAMWARO wa NYAGEMI

Kwa Muhtasari:

Wangi wao ni ja nyuki, na ukiwo mizingani

Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!

SIINGIYI kwa mikiki, nisikize kwa makini,
Kujua mwastahiki, nililetalo mezani,
Iwapo humakiniki, tego litakutegeni,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Tafakari uhafiki, wadhamuwo maishani,
Si kwamba huwakumbuki, kutokea uchangani,
Wako tele marafiki, walokutiya tabani,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Wangi wao ni ja nyuki, na ukiwo mizingani,
Semo halisahuliki, li tamu toka kinwani,
Na uchungu husemeki, kututiya hatiani,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Mabaya wanashabiki, japo sio hadharani,
Kisiri wanashiriki, kukuongoza gizani,
Kutangaza taharuki, wao ndio namba wani,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Husababisha hilaki, kwa wangi waso makini,
Chambua utasadiki, akhi ni majoka kijani,
Nyasini hatambuliki, mwendo wa chini kwa chini,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Mangi hayafikiriki, usidhani ni matani,
Mawi wanayashiriki, kikulacho ki nguoni,
Songombwingo wazandiki, fanya kuwatambueni,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na na mfitini!


Mbona hawaeleweki, nyendo za kihunihuni,
Wafuge hawafugiki, hayawani wa nyikani,
Pika sumu hawachoki, za kondoo kavaeni,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


Nawaaga halaiki, lumbo natamatishani,
Wajuweni wazandiki, wanafiki wafitini,
Si eti nawashitaki, bali tupate makini,
Twabiya ya mnafiki, ni moja na mfitini!


NYAMWARO wa NYAGEMI
'Malenga wamigombani'
Verce Ndumberi High-Kiambu.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating