http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

Bodaboda zatuponda

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na FRANKLIN MUKEMBU

Imepakiwa - Wednesday, November 5  2014 at  16:56

Kwa Muhtasari

Kila mara yatendeka, wananchi waumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari

 

Nimejawa na kumaka,kadhia nasimulia,
Shairi naliandika, kujuza yalotokea,
Kila mara yatendeka, wananchi waumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Mapema tukidamuka, kazini kuelekea,
Bodaboda zatumika, upesi zatudumia,
Madhari zina haraka, ndiani kutokawia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Haraka hina baraka, ajali zinatokea,
Abiria wadhurika, vibaya wanaumia,
Hela nyingi zatumika, kutibu waloumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Wendeshaji twawataka, mafunzo kuhudhuria,
Vyeti ghushi mukisaka, ujuzi tawondokea,
Ufisadi tukiepuka, tajiriba tawafaa,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Barabara vema shika, ishara nazo tumia,
Matutani mukifika, mwendo wako pungua,
Hatimaye utafika, ajali hitotokea,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Vituoni mukifika, abiria kadiria,
Lukuki ukiitaka, matatani tajitia,
Trafiki watakusaka, majanga tajichumia,
Bodaboda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


Kaditama nimefika, dereva mewahusia,
Nidhamu yahitajika, barasite kitumia,
Maafa yatosikika, raia tahudumia,
Boda boda zatuponda, wendeshaji tahadhari!


FRANKLIN MUKEMBU
Mawimbi Ya Nchi Kavu
Kajuki-Nithi

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com