http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

MOLA WALAZE PEMA

Imepakiwa Monday November 10 2014 | Na EKADELI LOKIDOR

Kwa Muhtasari:

Machungu yatulemea, shufaa metutoweka,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

POLISI mlofariki, wakenya twawaombea,

Heshima mnastahiki, muwanga kujitolea,

Kazini likuwa nyuki, katu hamkuzembea,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Simanzi imetuvaa, mauti yalipofika,

Furaha metukimbia, mebaki kusononeka,

Machungu yatulemea, shufaa metutoweka,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Polisi mloumia, afueni twawakia,

Mola awape shufaa, matatibu kipokea,

Katu sikate tamaa, kazini mkirejea,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Wakati sasa mefika, polisi kuwafidia,

Tuwapeni madaraka, polisi walobobea,

Polisi tatamauka, tusipowapa ridhaa,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

 

Polisi tuwape silaha, majangili siwapiku,

Mafunzo yawe silaha, watumie kila siku,

Ya Kapedo si mzaha, Lokidor sina chuku,

Mola awalaze pema, polisi walouwawa.

  

EDWARD EKADELI LOKIDOR,

'Balozi wa Kiswahili'

NAIROBI.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating