http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

MIHADARATI ACHENI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na "ZIMWI LIKUJUALO" - ABUBAKAR FAKHI

Imepakiwa - Wednesday, November 12  2014 at  19:36

Kwa Muhtasari

Haya ninayoyanena, si mambo ya kutania

Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni

 

BISMILLAHI ya Jabbari, Mola uliye Azizi,
Nakuomba yenye kheri, na baraka kwenye kazi,
Isinifike ya shari, na yote ya pingamizi,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Haya ninayoyanena, si mambo ya kutania,
Ni kitu nilichoona, katika hini dunia,
Wala sitopingana, na kaumu wenye nia,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Mihadarati hakika, humdhuru mtumizi,
Na katika pata shika, kama wenye usingizi,
Humfanya kuteseka, na mwishowe huwa mwizi,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Ulevi na misokoto, ugoro na ya uvundo,
Huwapoteza watoto, kwa afiya na matendo,
Na kuacha kama ndoto, uchomao uzalendo,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Jambo la kuhuzunisha, ni kuona mtegemewa,
Akiwa anawakisha, na kupuliza kwa hewa,
Ugoro na hiyo shisha, kwake zikiwa ni sawa,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Hasa kiwa msichana, alo na hino tabia,
Huwa ni hasara sana, kwa walimwengu jamia,
Hata pia mvulana, wote jangani hungia,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Kuhusika ulevini, ni hatari ya maisha,
Mitaani na shuleni, takuwa waogopesha,
Hata walio moyoni, kwako utahangaisha,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Ugomvi hujitokeza, pindi akizitumia,
Kuwapiganisha wenza, kwake hilo ni sawia,
Hakika inachukiza, hilo kwangu ni hatia,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Sijakuwa wa kukoma, ila wino unaisha,
Kueleza ya kuchoma, moyoni hayajaisha,
Huku muda wayoyoma, na pumzi nikishusha,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

Beti kumi zimefika, nafupisha yangu mada,
Ni mambo yaso na shaka, yalosababisha shida,
Nawaombea Rabbuka, kuwapa yenye saada,
Kueleza ilo wazi, mihadarati acheni.

"ZIMWI LIKUJUALO"
ABUBAKAR FAKHI

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com