http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

DUNIANI KUNA WAJA

Imepakiwa Wednesday November 12 2014 | Na SYLVESTER SIDDI KIROBOTO

Kwa Muhtasari:

Mengi nimeangalia, moyoni nikaumia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

KULIA huku kulia, kuna sababu kulia,
Leo nitawaambia, huzuni yanonitia,
Mengi nimeangalia, moyoni nikaumia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Hapa katika dunia, mambo nimeshuhudia,
Kuna ya kufikiria, mtu ukamlilia,
Kunao wanoumia, na vibaya kusikia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Nanzia hubani mle, ndimo mwenye dhiki tele,
Nimeionja Mpole, japo si sasa ni kale,
Leo kuna wateule, mapenzini wachochole,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Wangine wamefiliwa, na wenzi wao ghafula,
Uchungu waloachiwa, anaoujuwa Mola,
Hufika wakazidiwa, kaburini wakalala,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Wapo wasiojaliwa, watoto wao kupata,
Mifano wakapigiwa, hasa wakiwa wakata,
Kaburini wakitiwa, hakuna wa kuwaita,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Pia kunao fukara, wajaribucho hakiwi,
Huwakimbia ajira, wakiomba hawapewi,
Fungu lao kuzurura, kesho yao hawajuwi,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Wapo mwisho walofika, wakalaumu Rabuka,
Kosani wakamuweka, kwa kudhani ahusika,
Imani hutiwa shaka, na dini wakaitoka,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Tena kuna wenye pesa, walo tajiri kabisa,
Nao dunia yatesa, furaha wakaikosa,
Ila nui hii sasa, afadhali japo tasa,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Moliwa leo nalia, nyuso huzuni zatia,
Naumia kwangalia, mayatima wakilia,
Wajane wajinamia, bwana wakikumbukia,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Sijui mimi sijui, yote hayo sielewi,
Mie siumbi siui, na lolote siamuwi,
Bila uchungu sizui, mkosa hisia siwi,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Rahima nakusaili, imani zetu kumbuka,
Hali zetu zibadili, kukushukuru twataka,
Si kuwa hautujali, lakini twatamauka,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Ilivyo huko mbinguni, timiza na duniani,
Kwa hekima na imani, tuongoze alamini,
Tuepushe ya sharini, tusiingie dhikini,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Kama enzi ya safina, utunusuru Rabana,
Utuponye al’amina, aali wa swahibina,
Uyaone hayo inna, amina Rabb’l amina, ,
Dunia hini dunia, kuna waja yaonea.

Sylvester Siddi Kiroboto
“Kimpole”
Duka la Mihalake (kwa Dhima ya Karima),
Eldoret Mjini

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating