http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

MAZINGIRA TUYATUNZE

Imepakiwa Wednesday November 12 2014 | Na WAMBUGU YUSUF

Kwa Muhtasari:

Tafakuri naileta, iwe chanzo cha karamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

UFANISI na ukata, asilize mwafahamu,
Kukosa pia kupata, kipimo chake ni hamu,
Tafakuri naileta, iwe chanzo cha karamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Ni ilani kwa wakata, nanyi mnaojikimu,
Mtakuja kula mwata, mazingira kihujumu,
Tunajitia utata, tunaishi kwenye sumu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Tukumbuke kuikata, miti ni kujihukumu,
Maafa tunayaleta, kwa vizazi takadamu,
Masika kutoyapata, mazao yawe adimu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Chemichemi kuzipata, ndu’angu lipo jukumu,
Shiriki pasi kusita, isije kutugharimu,
Kwa ghaidhi ninateta, nipulikeni adamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Usafi kote kunata, ndiyo silika timamu,
Umbijani tukipita, wahakiki tabasamu,
Wanyama macho wavuta, wanatutia hamumu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Laazizi nawasuta, mambo haya ni muhimu,
Masaibu yatang’ata, tukikosa utalamu,
Tuondokee kujuta, tusende bure kuzimu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

Sikio toeni nta, msije kujidhulumu,
Piganeni hivi vita, vya mazingira adhimu,
Tuwe mtungi na kata, maisha yawe matamu,
Tuiambae sakata, mazingira tuyatunze,

WAMBUGU YUSUF,
Malenga wa mlimani.
Thika.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating