http://www.swahilihub.com/image/view/-/2522040/medRes/704131/-/lq76gl/-/Minisketi.jpg

KINA DADA WAKO HURU

Imepakiwa Monday November 17 2014 | Na EKADELI LOKIDOR

Kwa Muhtasari:

Jamani si ustarabu, ghashi kumdhalilisha,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

MWANGWANA yu huria, apendavyo kuvalia,

Si haki kumzomea, mja alivyovalia,

Matusi kumrushia, ghashi asiye hatia,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

Jamani si ustarabu, ghashi kumdhalilisha,

Ni jambo isojibu, banati kumdunisha,

Sio tena adabu, rindao kuteremsha,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

Wanawake wana hadhi, yafaa kuwastahi,

Mavazi yao kiudhi, kwa upole wanasahi,

Ni bora kuwanyaadhi, wavalie kisitahi,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

Wakati imefikeni, wanaume tustarabike,

Sheria tufuateni, daima tuwajibike,

Tuwache uhayawani, wanawake watukuke,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

Wakenya tukumbukeni, heshima kitu adhimu,

Maadili tushikeni, ustarabu pate timu,

Tubaidi walakini, kotekote kistakimu,

Kina dada wako huru, kuvalia wapendavyo.

EDWARD EKADELI LOKIDOR,

'Balozi wa Kiswahili'

NAIROBI.

 Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating