http://www.swahilihub.com/image/view/-/2522040/medRes/704131/-/lq76gl/-/Minisketi.jpg

VISKETI VYA KUBANA

Imepakiwa Wednesday November 19 2014 | Na LUDOVICK MBOGHOLI

Kwa Muhtasari:

Wavaaje rinda duni, tena rinda la kubana

Lioneshalo mwilini, viungo vya siri pana

Kama huo si uhuni, tuuitaje kwa jina?

KAMA mwavaa vaeni, nguo ndefu tena pana

Sio kuvaa vimini, visketi vya kubana

Tuwaone hadharani, jinsi mlivyo jazana!

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Hiyo ni tabia gani, mwawafundisha vijana

Ujinga wa uzunguni, mwatuletea bayana

Halafu mwataka nini, walifanye wavulana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Unapovaa vimini, na kamisi za kichina

Na sidiria chuchuni, na chupi ya ndani huna

Unatarajia nini, ukipita kwa kijana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Kuvuliwa hadharani, tena mchana mchana

Kiguo cha kishetani, kwangu ubaya hakuna

Maana uhayawani, nadhani umekubana!

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Wavaaje rinda duni, tena rinda la kubana

Lioneshalo mwilini, viungo vya siri pana

Kama huo si uhuni, tuuitaje kwa jina?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Mwaenda barabarani, ati mnaandamana

Mwampinga Maanani, kwa kuvalia vimina?

Nambieni hiyo nini, kama hiyo si laana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Havifiki magotini, visketi vya kubana

Vyaishia mapajani, karibu na hiyo ‘zana’!

Nyinyi ni viumbe gani, wala adabu hamna?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Nguo hizo nguo gani, fupi kisha za kubana

Wala huokoti chini, kilichoanguka tena

Huinami mapajani, zimebana raha huna!

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Na hicho chako kimini, dada yangu msichana

Kwani kina hadhi gani, kama siyo ya laana

Wamtamanisha nani, kama sio wavulana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Nusu uchi hadharani, watembea twakuona

Wala haya hauoni, na mnyama wafanana

Unamvutia nani, kama si hao vijana?

Kama mwadhani mwafana, basi tembeeni uchi!

Share Bookmark Print

Rating