http://www.swahilihub.com/image/view/-/2527502/medRes/879410/-/awh8orz/-/kajwang%25271911.jpg

 

KIFO CHA OTIENO KAJWANG

Imepakiwa Wednesday November 19 2014 | Na LUDOVICK MBOGHOLI

Kwa Muhtasari:

Daima alisimama, kutetea walegevu

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

KIFO cha mwanasiasa, bwana Kajwang Otieno

Ni pigo kuu kwa sasa  twalia twasaga meno

Hakika tutamkosa, katika yetu maono

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Mola amlaze pema, huyu wetu kiongozi

Alosimama daima, akawa mpingamizi

Wa dhuluma na hujuma, mfano wa ulanguzi

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Alikemea daima, siasa za kipumbavu

Hakutaka uhasama, wa chuki, hila na wivu

Daima alisimama, kutetea walegevu

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Hivi moyo waniuma, nikikumbuka maneno

Aloteta akisema, kwamba ‘bado mapambano’

Wimbo wake ulovuma, ‘mapambano mapambano!’

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Wakenya kinatuchoma, kifo chake pigo kuu

Kisiasa kawa chuma, hakutia makuruu

Wakinzao kawazima, kama moshi wa kifuu

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Nasema poleni sana, poleni mliofiwa

Hasa mkewe na wana, na marafiki wafiwa

Na Raila pole sana, kifo kimekuumbuwa

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Ndio hali ya dunia, muda ukimalizika

Lazima unajifia, kwani Mungu kakutaka

Huishi kuendelea, lazima utaondoka!

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

Kaditamati Mbogholi, mwisho wa shairi hili

Mliofiwa kwa kweli, nafahamu hamlali

Hata na kula hamli, huzuni imesaili

Bwana Otieno Kajwang, Mola amlaze pema.

 

LUDOVICK MBOGHOLI

Al-Ustadh-Luqman

Ngariba – Mlumbi

Taveta – Bura / Ndogo

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating