http://www.swahilihub.com/image/view/-/2423050/medRes/336861/-/1af5pdz/-/eaLamu.jpg

 

TUJIFUNZE KISWAHILI

Ufuo wa bahari Kenya

Ufuo wa bahari katika Pwani ya Kenya. Picha/MAKTABA 

Na SWALEH SUHEILl ABEID (SAUTI YA HAKI)

Imepakiwa - Wednesday, December 3  2014 at  18:10

Kwa Muhtasari

Neno moja liliyoko, la tafauti maani
Nami pia tabaini, niongeze yaliyoko

 

Shukurani zije kwako, ewe Nsura Hassan
Kwa kutoa hoja zako, ulotuma kilingeni
Neno moja liliyoko, la tafauti maani
Nami pia tabaini, niongeze yaliyoko

PAA ni ya kuruka angani, ya kupaa kama nyuni
PAA ni la masikani, lavimbwa sivuje ndani
PAA ni ya hayawani, kama mbuzi wa mwetuni
PAA nyengine baini, para samaki karoni

UNGA ni kushikanisha, pabovu pawe pazima
UNGA ni wa kujilisha, wa ngano au wa sima
UNGA ni ya kupatanisha, ukashikamana uma
UNGA nyengine nonesha, kama iko utasema.

PANGA ni ya lile panga, la kufyekea nyasini
PANGA ni ya ile panga , yenye ndonga mzimuni
PANGA ni kule kupanga, kuweka sawa swafuni
PANGA nyengine ni panga, kudanganya na kukhini

MBUZI ni ya hayawani, zizini twawashungia
MBUZI ni ya mapishini, ni ya nazi twakunia
MBUZI mwitu mjuweni, msituni atokea
MBUZI nyengine siyoni, kama iko nionyeni
UWA ni ya lile uwa, la kuchanuka mtini
UWA ni kwenda kuuwa, mja afe duniyani
UWA ni boma hutiwa, au ukuta nyumbani
UWA nyengine tambuwa, kama iko ibaini

KATA ni ya kuyachota, kwa kata maji uteke
KATA ni kukatakata, hadi m’ti uanguke
KATA ni ya kuukata, ukuruba ukatike
KATA nyengine kukata, kiuno kitibwirike

TAA ni ya kumulika, tukaoneya kizani
TAA ni ya makhuluka, samaki wa baharini
TAA taa kushikika, kuhangaika ndweleni
TAA nyengine nataka, kama iko ileteni

FUA ni ya kuzifuwa, kisha nguo ziswafika,
FUA ni chombo kufuwa, kama pete ipendeke
FUA ni nazi kufuwa, hadi kumbi limbambuke
FUA nyengine tambuwa, kama iko itajike

TANGA ni kutangatanga, kubeheneka mjini
TANGA ni roho kutanga, mtu hawi na makini
TANGA ni ya lile tanga, la jahazi baharini
TANGA nyengine kuchanga, pesa zifae chamani
TUNGA ni kule kutunga, kwa usaha wa jipuni
TUNGA ni ya kujitunga, ukae tahadharini
TUNGA ni kule kutunga, mbuzi walishe nyasini
TUNGA nyengine kutunga, kishada cha asimini

TUNGA ni ya kuvitunga, vina viwe na mezani
TUNGA ni ya kuutunga, unga mule tungiyoni
TUNGA ni ya kuvitunga, vitinyango kijitini
TUNGA nyengine kutunga, Insha kule shuleni

Swaleh Suheil Abeid
(Sauti Ya Haki)
Dubai – U.A.E.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com