http://www.swahilihub.com/image/view/-/2534870/medRes/884849/-/i6mmisz/-/dnmandera2511ta.jpg

 

TUMECHOKA KUFA

Imepakiwa Friday December 5 2014 | Na LUDOVICK MBOGHOLI

Kwa Muhtasari:

Kila siku visavisa, roho zinadekadeka

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

SASA tumechoka kufa, na miili kuizika

Twafa bila taarifa, ya maradhi kutushika

Kila kuchao maafa, ya ugaidi kuzuka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kila siku visavisa, roho zinadekadeka

Hatutulii kabisa, twafa huku tukizika

Ndipo napiga kamsa, kufa sasa tumechoka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kiongozi wa taifa, Uhuru Kenyatta kaka

Nakwambia huku kufa, kipumbavu tumechoka

Kama kufa ndio sifa, basi tumekinaika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Tumechoka kufa sasa, UhuRuto wahibaka

Hata kwenye makanisa, mabomu yanalipuka

Na misikitini visa, vingi mno vinazuka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kufa sisi tumechoka, twafa kama takataka

Twauliwa kama nyoka, kwa risasi na mashoka

Hakuna wa kuponyoka, twambe amenusurika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Ovyo ovyo twauliwa, na doria wanashika

Wanajeshi wetu hawa, na polisi kadhalika

Waona tukiuawa, huku twafanywa mateka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Mimi naona ajabu, helikopta zazunguka

Mandera zikijaribu, ati amani kuweka

Na huku Al-Shababu, nao kasi wanashika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Kuuawa kikatili, wananchi tumechoka

Huku tuna serikali, tuloipa mamlaka

Tena ni ya dijitali, vijana walochipuka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Narudia mauaji, ya Mandera tumechoka

Tunaona wachinjaji, wa vipanga na vishoka

Wakija kwenye vijiji, kuchinja na kutoroka!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Na sio tuu Mandera, hata Pwani wamefika

Na maeneo ya bara, nako wameshazunguka

Magaidi na wakora, na wahuni kadhalika!

Mauaji ya Mandera, sasa tumechoka kufa!

 

Share Bookmark Print

Rating