KIMAKONDE SI KINGINDO

Imepakiwa Saturday December 6 2014 | Na WILSON NDUNG’U

Kwa Muhtasari:

Timazi ya lugha gwanda, ata kuiweka kando,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

TIMAZI ya lugha gwanda, ata kuiweka kando,

Jinsi unavyo enenda, wazi hufwati mkondo,

Jina na tungo si chanda, na pete ufunge fundo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Umepiga parapanda, bilashi kuanza kondo,

Silaha za kujilinda, zako ni fimbo na nyundo,

Hutapata ukomanda, kwa vidondo na vishindo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Lafudhi hipigwi randa, Mwangi haneni ja Fondo,

Msiu si mnyarwanda, ndimi zao zina pindo,

Kiswahili cha Uganda, si kile cha Loliondo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Wanenavyo Mijikenda, wa Ganze hata kinondo,

Wagiriama wa nyanda, uluyani Kavirondo,

Pamoja na Waholanda, wanatofauti rundo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Lahaja kumi na kenda, zapitana kimuundo,

Washairi wa Mpanda, tofauti na Waendo,

Ada zao zimetanda, kwa ndimi na midundo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Kiswahili ni matunda, ya bantu wenye pendo,

Waishi katika kanda, Afirika ya utando,

Mambasa hadi Ruanda, wamo siwaweke kando,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Uko kwenye njia panda, hujakuwa mzalendo,

Lugha yenu hujalinda, kwa silaha za kishindo,

Umeazima magwanda, ya Waswahili mitindo,

Kimakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

Wangindo wameshatanda, kisauni kwa mgando,

Kujifunza wamedinda, lugha yao ya kingindo,

Mwaka rudi mwaka nenda, hawabadilishi mwendo,

Kamakonde si Kingindo, lafudhi hipigwi randa.

WILSON NDUNG’U MUCHAI,

"Mjoli wa Shekinah",

Kitale

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com 

Share Bookmark Print

Rating