UBAKAJI USHINDWE

Na JAMES MUTWIRI

Imepakiwa - Saturday, December 6  2014 at  17:47

Kwa Muhtasari

Rijali liso utu chembe, kiusena lawazuga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

MEAMUWA nisifumbe, kitendawili kutega,

Ninene wazi ujumbe, fahamu kinaganaga,

Ndo nazatiti kabambe, kuyataja bila woga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Nina vigoli wakembe, kuwatilia ja boga,

Rijali liso utu chembe, kiusena lawazuga,

Kalilazimisha jembe, kondeni kulivuruga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Waso hiari viumbe, nduli tundalo kumega!

Wali tosa maembe, ndanimo kuwakoroga,

Vipi kero situkumbe, geuzwa karaha uga?

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Shani watoma halumbe, kutesa waliofuga!

Wawadaka wawarambe, maeneo yalo viga,

Kuso mianya wachimbe, wakidai ni shuga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Vigoli tele niambe, mebakwa kawa mzoga,

Maradhi yasio tembe, najisiwa mekanyaga,

Majuto mesali kumbe! Dunia teke wapiga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Tuwapatie uvimbe, wajulikane chambega,

Tuwatie ja vikombe, baada ya kuwatoga,

Juujuu tuwasombe, hadi jela kuwachega,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Kike sigeuze ng’ombe, kiimla kuwasaga,

Sheria kali itambe, wadhalimu kuwatega,

Ikatekate ja wembe, wapate kugugayuga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Hili la kichwa tuvimbe, lisendelee kutaga,

Ubakaji tusiimbe, tupige kondo wakwiga,

Mkawini tumuombe, ya shwari ya omega,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

Malenga niso uzembe, wasikizi nawaaga,

Mepuliza hii pembe, ujumbengu meuaga,

Kiumbe kike tupambe, ili wapate kunoga,

Twamkemeya shetani, wa ubakaji kabisa!

 

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

“Malenga Msifika”,

 CHUKA - Tharaka Nithi

 

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com