MASKINI WA NIDHAMU

Imepakiwa Saturday December 6 2014 | Na SIMON ITEGI

Kwa Muhtasari:

Vazi lako ukipima, viungovyo lisetiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

NATUMAI msalama, salimini bila shari,

Hu utungo nautuma,  ya moyo ninakiri,

Natumai mtasoma, muelewe shwarishwari,

Maskini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Moyo wangu waterema, kuwaona mwakariri,

Kama samba mwalalama, kijigonga kwa vidari,

Na kidete mwasimama, haki zenu kudhihiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Vazi lako ukipima, viungovyo lisetiri,

Usianze kulifuma, bila kimo kubashiri,

Sio jambo la hekima, maumboyo kuhakiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea

 

Mila zetu kuzitema, hilo sio jambo zuri,.

Kunga zetu za gharama, kupuuza sio heri,

Ni utumwa huo jama, ustarabu kughairi,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Tudumishe na heshima, kwa wadogo wa kiumri,

Tujitunge kina mama, wasiige na vigori,

Hili swala linauma, nanitungu kishubiri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Yashangaza naungama, wenzanguni mafahari,

Kunivua ni dhuluma, vilevile uayari,

Nambie kitaaluma , nelekeze nishauri,

Masikini wa nidhamu, limwengu mekuzoea.

 

Tamatini ninakoma, hilo swala mfikiri,

Moyo wangu wazizima, kwa utungu sio siri,

Hadharani ninasema, ulimwengu ni safari,

Masikini wa nidhamu,limwengu mekuzoea.

SIMON ITEGI NYAMBURA,

Chuo Kikuu cha Laikipia

Tuma mchango wako kwa: swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating