http://www.swahilihub.com/image/view/-/2583868/medRes/918270/-/3d6qdcz/-/mganga.jpg

WAGANGA MNA NINI!

Mganga ajaribu kufufua

Mganga Samuel Kanundu (akiwa na nguo nyekundu) awahutubia wanahabari katika kijiji cha Mwazaro, Shimoni Januari 09, 2015 akiwa katika shughuli ya kujaribu kufufua Dominic Kyalo aliyefariki Oktoba 2013. Picha|FAROUK MWABEGE  

Na NYAMWARO O'NYAGEMI

Imepakiwa - Tuesday, January 13  2015 at  16:12

Kwa Muhtasari

Enzi ya utandawazi, kwa wengine tandawizi,

Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

WAGANGA wa mitishamba, Afrika mashariki,

Itaneni kwenye chemba, na gumzo mshiriki,

Sio la watu kuchimba, ni nyie kujihakiki,

Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Nimechunguza kwa muda, madai ya ndugu Duba,
Shehe Abduba Dida, yakini mchungu mwiba,
Waganga wengi ni shida, au imani ndo haba?
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Lilikuja zee lile, maarufu la Loliondo,
Mbelekile Mwashavile, mganga mwenye huondo,
Waja kanywa dawa ile, kafaulu lake windo,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Enzi ya utandawazi, kwa wengine tandawizi,
Matangazo kote wazi, hipo ndwele hamuwezi,
Mmepotosha kizazi, kikongwe na chipukizi,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Wengine ni wanajimu, ya kesho kuyabashiri,
Kumbe ni kupika sumu, matapeli wajeuri,
Hawachagui msimu, lengo wawe matajiri,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Wajitanua vifua, nguvu kufufua wafu,
Kulisimamisha jua, kwa uwezo mtukufu,
Hatuachwi kupumua, wamepora maelfu,
Twambie nani mkweli, na nani ni mtapeli!

Zangu saba zimetosha, beti natia kufuli,
Ama kweli mnatisha, wasoamini Jalali,
Komesha zenu tamasha, mche Mungu tafadhali,
Twambiye nani mkweli, na nani ni mtapeli!

NYAMWARO O'NYAGEMI

“Malenga wa Migombani”

Kiambu Mjini