http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596732/medRes/926858/-/3ry3h/-/OmarBabu.jpg

 

KIFO CHA MARIJANI PIGO

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na NYAMWARO O'NYAGEMI

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  09:27

Kwa Muhtasari

Angengoja ziraili, Marijani awe babu,
Akitutiya makali, Kiswahili Kiarabu,
Kifo chake shaha 'Abu, ni mjeledi mkali!

 

KIFO umetukatili, kutwaa Omar Babu,
Mwalimu wetu wa kweli, maswali yetu kujibu,
Kwangu kanitowa mbali, nikiwa mbumbumbu bubu,
Kifo cha Omari Babu, ni pigo kwa Kiswahili,

Ni pigo kwa kiswahili, kifo cha Omar Babu,
Angengoja ziraili, Marijani awe babu,
Akitutiya makali, Kiswahili Kiarabu,
Kifo chake shaha 'Abu, ni mjeledi mkali!

Ni mjeledi mkali, kifo cha Omar Babu,
Litungia hoja kali, kanifanya mraibu,
Misamiati asali, ni ushairi wa Abu,
Lingoja tungo za Babu, Jumamosi jumapili!

Jumamosi Jumapili, lingoja tungo za Babu,
Taifa Leo faili, zake ni tele za Abu,
Omar mtajamali, leo kifo kamsibu,
Muandishi wa vitabu, mtuzwa kwao na mbali!

Mtuzwa kwao na mbali, uandishi wa vitabu,
Mwaka wa elfu mbili, ni mwanahabari 'Abu,
Ujerumani ni mbali, huko katangaza Babu
Saratani kakusibu, kakulaza sipitali!

Kakulaza sipitali, saratani kakusibu,
Si mara moya si mbili, linambiya shehe 'Abu,
Tumbo lauma vikali, wapokezwa matibabu,
Kumbe waondoka Babu, vipi tutalikubali?

Vipi tutalikubali, kuondoka kwako Babu?
Mjane wana wawili, kifo kimewaghusubu,
Nawasihi sende mbali, nayo jamii ya 'Abu,
Yanitoka ndiya mbili, matozi nalia Babu!

NYAMWARO O'NYAGEMI
"Malenga wamigombani"
Verce Ndumberi High-Kiambu.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com