http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596732/medRes/926858/-/3ry3h/-/OmarBabu.jpg

 

MTUNZI OMAR BABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na JUMA NAMLOLA

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  10:58

Kwa Muhtasari

Kazi yake Rahamani, kwa Omari ‘metimia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

WASHAIRI pulikani, huzuni imeningia,

‘Menipotea uneni, Namlola ninalia,

Kazi yake Rahamani, kwa Omari ‘metimia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

Tulijuana zamani, mashairi kichangia,

Tukawa sote kazini, Nation akifanyia,

Hadi kenda Jerumani, lugha kuipalilia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

Na vitabu madukani, ukenda kuulizia,

Hutakosa japo thani, alivyotuandikia,

Mimi naye kwenye fani, pamoja tumechangia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

Beti zenu gazetini, Jumamosi nategea,

Mkono wa buriani, tupate kumpungia,

Sote tumo safarini, yeye ametangulia,

Tumuage kwa heshima, mtunzi Omari Babu.

 

JUMA NAMLOLA,

"Hakimu wa Mashairi"

S.L.P 49010 - 00100

Nairobi, Kenya

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com