http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596958/medRes/926972/-/15uh5o1/-/AbuMarjan.jpg

 

PENGO KUBWA LITABAKI

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na KIMANI WA MBOGO

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  12:21

Kwa Muhtasari

La mno limetukia, katukumba ukumbini,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

 

HUMU tu wapita njia, kesho haijulikani,
Majonzi limetutia, likatanda la huzuni,
La mno limetukia, katukumba ukumbini,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Imetuchukua muda, jambo hili kukubali,
Tumefikwa nayo shida, wapenzi wa Kiswahili,
Twakumbuka zako mada, lugha ulivyoijali,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Pakubwa ulichangia, bidii zako mwalimu,
Pengo umetuwachia, pote ulipohudumu,
Kwa mengi umepitia, ughaibuni na humu,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Ulinifunza kutunga, fani nikaibaini,
Lugha hukuiboronga, ulivyokuwa makini,
Kusarifu ulilenga, lugha ulivyotamani,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Vitabu uliandika, kumbukumbu itakuwa,
Vitabaki kusomeka, daima kuenziwa,
Upesi umetoweka, mauti kukuchukuwa,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Sana ulinyenyekea, na bora hukujiona,
Wengi ulitembelea, urafiki ukafana,
Sifa zilivyoenea, zilifika kila kona,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Ilikujaa hekima, njema hiyo kufaana,
Pafaapo ulisema, wingi wa busara tena,
Nitaukumbuka wema, mazuri yako kwa kina,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

Kifo ni adui kweli, hunyakua walo wema,
Tupendao hukabili, wazuri waliovuma,
Kifo hugeuza hali, yalo mema yakakoma,
Pengo kubwa litabaki, Marjan kutuacha.

 

KIMANI wa MBOGO

Mwanagenzi Mtafiti

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com