http://www.swahilihub.com/image/view/-/2597414/medRes/927271/-/jbfveuz/-/TFOMARBABU2101.jpg

 

KIFO KIMEATUWA MIOYO

Imepakiwa Wednesday January 21 2015 | Na RICHARD  MAOSI

Kwa Muhtasari:

“Mti mkuu kugwaa, viyoyo tu mashakani,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.”

AMEKWENDA kaburini, baba yetu wa fasihi,

Keshazima zake mboni, mekuja kutanabahi,

Kujiunga mavumbini, muwandishi wa tarihi,

Kifo cha Omar Babu, kimeatuwa mioyo.

 

Mti mkuu kugwaa, viyoyo tu mashakani,

Yamebakia mawaa, kulizana maskani,

Shehe wetu hukufaa, kuondoka duniani,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.

 

Yamemteka mauti, mshairi wa nudhuma,

Ale shika madhubuti, kiwa mesimama wima,

Leo hayupo hayati, imetuvaa nakama,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.

 

Mchangizi hatunasi, mekuwa mwalimu wangu,

Meuona ufanisi, Ulaya mekuwa tangu,

Waima sio kukisi, yametufika machungu,

Kifo cha Omari Babu, kimeatua mioyo.

 

Mwalimu nenda salama, pumzikoni makiwa,

Tunaukwea mlima, huko sote tutakuwa,

Mana haina ulama, mauti yanapotuwa,

Kifo cha Omari Babu, kimeatua mioyo.

 

Hazina ulonifunza, sitowacha kuishika,

Yote uliyoyakinza, utabaki kutajika,

Wasanii ulitunza, na vitabu kuandika,

Kifo cha Omari Babu, kimeatua mioyo.

 

Ndani ya Damu Nyeusi, ndoa yako ya samani,

Mikusanyiko sisisi, mathalani ni diwani,

Heri subira sikosi, ulivosema mneni,

Kifo cha Omar Babu, kimeatua mioyo.

 

RICHARD  MAOSI

"Amiri Kidedea"

Rovy Girls High School,

Nakuru.

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

Share Bookmark Print

Rating