http://www.swahilihub.com/image/view/-/2597414/medRes/927271/-/jbfveuz/-/TFOMARBABU2101.jpg

 

AMEONDOKA MHENGA

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na NUHU ZUBEIR BAKARI

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  18:02

Kwa Muhtasari

Umetuwacha mhenga, akusetiri Jalali,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani.

 

TUMEPOTEZA Swahiba, muandishi mashuhuri,

Mtu na zake haiba, mtunzi wa mashairi,

Umetufika msiba, mwenzetu Babu Omar,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Umetangulia sweba, amekuita Kahari,

Tunalia kwa msiba, metuwacha Jemedari,

Tunakuvika vikuba, ili ikufike zari,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Tungo ulizozitunga, na riwaya tumbitumbi,

Ziliibua kinganga, kwenye za watunzi kumbi,

Meenda ngali mchanga, tutaku-misi walumbi,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Michango uliyochanga, kwa lugha ya Kiswahili,

Metoa nuru na mwanga, katika janibu hili,

Umetuwacha mhenga, akusetiri Jalali,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Uende hadi peponi, aliko mtume wetu,

Katika mabustani, ya mitende na misitu,

Akufae Rahmani, Mungu muumbaji wetu,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Kaka umetangulia, bado ungali kijana,

Umeiwacha dunia, meenda kwa Marjana,

Leo tunaomba dua, iwe ni yako hazina,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

Hapa mefika hatwima, nakamilisha kutunga,

Ulale mahala pema, ewe Omar mhenga,

Kifo kwetu ni lazima, mja hawezi kupinga,

Mungu akulaze pema, ndugu yetu Marjani;

 

NUHU ZUBEIR BAKARI

“Al-Ustadh Pasua”

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com