http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596958/medRes/926972/-/15uh5o1/-/AbuMarjan.jpg

 

BURIANI MARIJANI

Imepakiwa Thursday January 22 2015 | Na BENSON NYALE

Kwa Muhtasari:

Kifo chako Marijani, wengi tumeshitukiya,

Kule kwetu ukumbini, kilio umetwachiya

BARA hadi visiwani, habari tulipokeya,

Kwa huzuni mioyoni, mwendani kuondokeya,

Kattu hatujaamini, Abu umetanguliya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Kulla pahala huzuni, sute tunaluliliya,

Kifo chako Marijani, wengi tumeshitukiya,

Kule kwetu ukumbini, kilio umetwachiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Utasaliya nyoyoni, japo umetanguliya,

Ndugu Abu Marijani,mangi katufunuliya,

Kote makongamanoni, lugha uliichangiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Soteni tumo ndiani, kwa Mola tatarejeya,

Tuishipo duniani, imani twashikiliya,

Si kwetu ulimwenguni, vumbini tunarejeya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Ninautungu moyoni, nashindwa kuvumiliya,

Katutoka Marijani, mwalimu wa kwaminiya,

Mweledi wa hino fani, sote tulitumaniya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Kalale pema peponi, Abu umetanguliya,

Wino wako vitabuni, daima utasaliya,

Naswi twendapo dukani, wanetu twanunuliya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Kuna pengo ukumbini, nani tashuhulikiya,

Tu makiwa wana fani, tumebakiya kuliya,

Meondoka Marijani, kilio katwachiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Mlezi we Marijani, salama twakutakiya,

Ulazwapo kaburini, Mola tunakuombeya,

Amekuita Manani, nawe ukaitikiya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

Litufaa Marijani, hilo ninashuhudiya,

Sio hapa ukumbini, chipukizi 'lituleya,

Mshairi we mwendani, welekezi litupeya,

Buriani Marijani, mbele umetanguliya.

 

BENSON NYALE

"Sauti ya Mbali"

Nakuru.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

Share Bookmark Print

Rating