http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596958/medRes/926972/-/15uh5o1/-/AbuMarjan.jpg

 

MSIBA ULOTUFIKA

Imepakiwa Thursday January 22 2015 | Na EDISON WANGA

Kwa Muhtasari:

Hatuwezi kususia, kifo ni tangu wa tangu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

YA Illahi Jalalia, Muumba wa nchi na mbingu,

Kwa yaliyotufikia, kukubali ni uchungu,

Hatuwezi kususia, kifo ni tangu wa tangu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Mtimani naumia, msiba ulotufika,

Siwezi kujizuia, mat'ozi kutiririka,

Umeenda pasi nia, ja mwizi ukatoroka,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Ulivyonisaidia, nakumbuka ndugu Babu,

Yeyote hukubagua, 'limfunza taratibu,

Siwezi kusingizia, uliyotenda sahibu,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marjani.

 

Kwa asilimia mia, ni wengi walikupenda,

Wataukosa wasia, kwa huzuni wakishinda,

'Lokuwa ukitetea, Kiswahili ushakwenda,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Umeacha familia, mke na wana wadogo,

Wote wanakulilia, umewapa kipigo,

Babu umewakimbia, haupo tena kigogo,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Omari Babu sikia, ulikokwenda ahera,

Nitafwata zako njia, mtazamo na taswira,

Haikuwa yangu nia, kifo kije kukupora,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marijani.

 

Natamati nikilia, mkono unatetema,

Edi nikifikiria, ulonitendea wema,

Simanzi menizidia, kwanilemea kuhema,

Mola mlaze peponi, ndugu Abu Marjani.

 

EDISON WANGA,

Son Bin Edi,

Mwana wa Mambasa.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

Share Bookmark Print

Rating