http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596958/medRes/926972/-/15uh5o1/-/AbuMarjan.jpg

 

BURIANI ABU

Imepakiwa Thursday January 22 2015 | Na ISMAIL BAKARI

Kwa Muhtasari:

Alikuwa maridhia, si mtu mwenye kuringa,

Na asingeshabikia, lugha ukiiboronga

KILIO tunacholia, kimetanda kwenye anga,

Wengi mmeshasikia, kilotufika kisanga,

Abu ametukimbia, sasa tunalegalega,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Si rahisi kwitikia, kukubali hili janga,

Hasa ukizingatia, juzi tukiwa twalonga,

Kwenda kumsalimia, Omar kumwengaenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Hayo yameshatukia, hakuna wakuyapinga,

Na kazi yake jalia, si ya mavangamavanga,

Msizue yakuzua, maneno kuungaunga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Mwalimu mulimjua, ni bingwa wa umalenga,

Vipindi alichangia, kwa radio na runinga,

Wengi vikawaingia, kuwatoa ushambenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Vitabu katwandikia, vyenye tungo zenye kunga,

Na vya Kiswahili pia, riwaya zenye muanga,

Vyote vimesaidia, kuongoza vijulanga,
Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Alikuwa maridhia, si mtu mwenye kuringa,
Hakupenda kupapia, mambo yasiyomlenga,

Na asingeshabikia, lugha ukiiboronga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Nataka kuwahusia, kina manju na malenga,

Japo ameshakimbia, hatupo naye mkunga,

Fuateni zake njia, na ninyi muwe wahenga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Maswahiba na insia, jamaa na wamachinga,

Mwaombwa kuvumilia, wala sio kujitenga,

Poleni twawatumia, tena bila kujivunga,

Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

Maneno yaniishia, sina tena la kubonga,

Kilobaki kumwombea, ndugu yetu na malenga,

Mola kutakabalia, dua zetu kutopinga,
Mola mlaze peponi, Kaka Abu Marijan;

 

ISMAIL BAKARI

(Swila Mchiriza Sumu)

NAIROBI.

 

Tuma mchango wako kwa swahilihub@ke.nationmedia.com 

Share Bookmark Print

Rating