http://www.swahilihub.com/image/view/-/2597414/medRes/927271/-/jbfveuz/-/TFOMARBABU2101.jpg

RAMBIRAMBI BABU

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Thursday, January 22  2015 at  13:17

Kwa Muhtasari

Swahiba Babu Omari , alikuwa ni mahiri

Mtunzi wa mashairi , mwandishi na mhariri

IILIKUWA Januari, asubuhi Jumatano

Nlipopata habari, Babu kafika kikomo

Ametuacha Omari, ulimwenguni hayumo

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Hakika nlishtuka, kupata habari hiyo

Ya Omari kututoka, akatwachia kilio

Hivi nnavyotamka, moyo wanienda mbiyo

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Swahiba Babu Omari, alikuwa ni mahiri

Mtunzi wa mashairi, mwandishi na mhariri

Wa makala na habari, na riwaya kufasiri

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Alikuwa mhadhiri, Omari Babu Chuoni

Vilivyo alishamiri, kazini Ujerumani

Hivi yatubana shari, hayu nasi duniani

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Walakhi Omari Babu, katika historia

Ni mwandishi wa vitabu, kisha m’bunifu pia

Hakubuni kujaribu, ni m’bunifu kwa nia

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Mie moyo waniuma, wanipandisha kiwewe

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe

Na sote nchi nzima, tuombe nyoyo zipowe

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Ingawaje linachoma, tukio la mtu kufa

Ndio ada ya Karima, kinachozaliwa hufa

Kikiishi kitazima, japo kife kwa kifafa

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Leo yeye ameenda, katangulia kuzimu

Tunalia twajipinda, zimetutoka fahamu

Tukumbuke nasi twenda, tutakuwa marehemu

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Jambo la mwisho kunena, sisi sote wafiliwa

Si vyema tulie sana, tumkufuru Moliwa

Ndiyo ada ya Rabbana, ya kufa na kufukiwa

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.

Naomba naomba sana, tupunguzeni makiwa

Tujaribu kukazana, huzuni kuiondowa

Maana ni dhambi tena, mungu tunamkosowa

Rambirambi nazituma, kwa mkewe na wanawe.