http://www.swahilihub.com/image/view/-/2597414/medRes/927271/-/jbfveuz/-/TFOMARBABU2101.jpg

 

MSILILIE MARIJANI

Imepakiwa Thursday January 22 2015 | Na MAIYO BIN MAIYO

Kwa Muhtasari:

Tukiuliza kwa nini, atayejibu ni nani?

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

AMETUACHA Marijani, so rahisi kuamini,

Hakupunga buriani, atuweke tayarini,

Tukiuliza kwa nini, atayejibu ni nani?

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Kudura zake Manani, hainani walakini,

Na ijapo ni huzuni, nawaomba kubalini,

Na ninyi tafakarini, hatima yenu ni lini?

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Alinena darasani, marehemu Marijani,

Akafunza ukumbini, hapa petu gazetini,

Kunga zake maishani, ziwe funzo mwafulani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Keshafika ukingoni, napo mwisho aushini,

Katu siseme haneni, akiwapo kaburini,

Alondika vitabuni, yanasema na wendani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Kazuru ughaibuni, mswahili uzunguni,

Katamba Ujerumani, sikwambii Marekani,

Akafundisha vyuoni, Fasihile kama nini,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Roho zenu lilieni, ufufuo u njiani,

Waingiao mbinguni, ni wenye haki yamini,

Jisaili mtimani, taingia pande gani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

Nimetimiza kanuni, za kuzijenga mizani,

Na laziada sinani, naondoka kwa huzuni,

Makiwa enyi wapwani, na wenye lugha barani,

Msilie Marijani, roho zenu lilieni.

 

MAIYO BIN MAIYO

'Malenga Wa Kiplombe'

Chuo Kikuu cha Baraton.

 

Share Bookmark Print

Rating