http://www.swahilihub.com/image/view/-/2594676/medRes/925535/-/6gau0o/-/DNLANGATASCHOOL1901v.jpg

HAKI HAIPO

Imepakiwa Saturday January 24 2015 | Na PHILEMON KONGA

Kwa Muhtasari:

Napangusa machozi, liyotukia Lang’ata,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

NAPANGUSA machozi, liyotukia Lang’ata,

Unyanyaso siku hizi, mizizini imekita,

Nasema mi' sinyamazi, ardhi meleta sakata,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

Mtoto kupiga kelele, akidai zake haki,

Askari mwaenda mbele, kukinga asishtaki,

Akili zenu mna ndwele, hamfuati itifaki,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

Kikosini cha askari, pamejaa sana doa,

Kila wakati tu amri, isiyoweza okoa,

Mliotenda si nadhari, heshimenu mebomoa,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

‘Fisa wapigwe kalamu, 'metuaribia sifa,

Nchi iliyotimamu, miongoni mataifa,

Sasa watuuhujumu, tokana hiyo kashfa,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

Swala hili la ardhi, kukija ni mahudhui,

Imekuwa  ni hadithi, imezua uadui,

Walaghai wanaridhi, tukiona asubuhi,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

Mbona vitoa machozi, watoto wakereketwa,

Chunguza hicho kikosi, kuanzia yule mkubwa,

Huo ni gani uzazi, usiokuwa na utwa,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

Hebu nyinyi katubuni, mbele zake Rabuuka,

Apate kuwasamehni, maovu 'liyotendeka,

Maana huo ni 'huni, kweli liyolaanika,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

Hapa mimi ninagura, 'mekosa matumaini,

Napunguzami hasira, Mola uwasameheni,

Naomba utupe sura, tustahilisi machoni,

Tutapata wapi haki, Kenya imejaa dhambi.

PHILEMON KONGA

"Ustadh Malenga"      

Chuo Kikuu cha Masinde Muliro.                                             

Share Bookmark Print

Rating