http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596958/medRes/926972/-/15uh5o1/-/AbuMarjan.jpg

 

MOLA AMLAZE PEMA!

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na BISMARCK KIMANGA

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  18:36

Kwa Muhtasari

Ninasoma gazetini, hayupo tena Omari,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

NINASOMA gazetini, hayupo tena Omari,

Mwenye tungo za makini, nzito na zenye urari,

Daima mwenye hisani, asiyependa kiburi,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Ndugu yangu Marijani, ameifunga safari,

Kasifika kwa yakini, mkufunzi mashuhuri,

Mwenye nyingi samahani, sumile pia kaburi,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Nashindwa kuamini, nimebaki ghururi,

Kanilea kwenye fani, na kunipa ushauri,

Meondoka duniani, Babu asopenda shari,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Chuoni na vitabuni, fasihi ikanawiri,

Kama  ‘Ndoa ya Samani’, ‘Heri Subira’ nakiri,

‘Kala Tufaa’ jamani, nayo mengi mashairi,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Metangulia njiani, amekwenda kwa Qahari,

Hayumo tena kundini, imemmeza kaburi,

Ametuacha mwendani, kaenda pasi kwaheri,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

 

Umekatika uneni, meniisha sitari,

Nalia ndani kwa ndani, zahuzunisha habari,

Kalamu naweka chini, machozi kama bahari,

Mola amlaze pema, peponi palipo wema.

BISMARCK KIMANGA

'Malenga Mwadilifu'

Rongai -Nakuru.