http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596732/medRes/926858/-/3ry3h/-/OmarBabu.jpg

 

KWAHERI OMAR BABU

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na MWALIMU STEPHEN DIK

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:04

Kwa Muhtasari

Kwanza ni mwanzaji, mwisho ni kwa muishaji,

Kwaheri Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

KWANZA ni mwanzaji, mwisho ni kwa muishaji,

Kifo chako ewe gwiji, kwa kweli sikutaraji,

Kilio kwa mtungaji, wa mijini na vijiji,

Kwaheri Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

La sivyo tunakumbuka, wosia ulotuacha,

Lidunde libingirike, jikombora limechacha,

Litupwe na lisiwake, likeshe usiku kucha,

Lala pema Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Mlo hai sisahau, umoja wetu ndo' nguvu,

Mtu awe akijua, maisha ni kama povu,

Miaka nayo ni ua, mwili wetu ni majivu,

Milele Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Naandika ukurasa, napiga nduru kichizi,

Naenda nikipapasa, maneno sizungumzi,

Ni Marjan kwa sasa, amaliza matembezi,

Nenda hima Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

Om shanti wa shanti, kaditama wa tamati,

Ole wako we mauti, ningakuvua makoti,

Ondoka kwetu mauti, sura mbaya we mauti,

Ohh nalia Omar Babu, tulobaki twakumbuka.

 

MWALIMU STEPHEN DIK,

'Mpenda Ushairi',

Siaya.