http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596958/medRes/926972/-/15uh5o1/-/AbuMarjan.jpg

 

BURIANI MARIJANI

Omar Babu

Bw Omar Babu. Picha/MAKTABA 

Na GITAA HERMAN ANGWENYI

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:11

Kwa Muhtasari

Mangi ulinifundisha, Lugha ngeli na mitungo,

Buriani marijani, Mola kakulaze pema!

 

UMETUFIKA msiba, watunzi tunatetema,

Mauko yamemuiba, ndu' yangu ninalalama,

Katangulia kwa baba, ni wapi tutaegema,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Mangi ulinifundisha, lugha ngeli na mitungo,

Kifo umekaribisha, tutakosa viambajengo,

Japo menitamausha, hutotoka langu bongo,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Tanzia nikapokea, mwanzo sikuziamini,

Ja kitoto nikalia, nikimlani shetwani,

Moyo zikaniatua, dawamu umo kitwani,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Watunzi ulikubali, toka bara pia pwani!

Katu huna mushekili, Mola kutunze peponi,

Vitabu vya Kiswahili, na tungozo tazighani,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

 

Limenilemea tozi, kwendeleya numeshindwa,

Manipiku michirizi, mtima umeshapondwa,

Omar Abu mwuguzi, uliko juwa wapendwa,

Buriani Marijani, Mola kakulaze pema!

GITAA HERMAN ANGWENYI

 'Mlawandovi Malenga'

Migombani- Nyancha.