http://www.swahilihub.com/image/view/-/2596732/medRes/926858/-/3ry3h/-/OmarBabu.jpg

 

ILLAHI TUHIFADHIE

Imepakiwa Thursday January 29 2015 | Na ALAMIN SIWA SOMO

Kwa Muhtasari:

Alikuwa ni mteshi, sikizani niwambie.

Amehama Ulimwengu, Omar katuondokea.

KADARA Mghani wangu, nakuomba nighanie,
Shairi la ndugi yangu, lighani nilisikie,
Ijapo nina utungu yabidi nivumilie,
Amehama Ulimwengu, Omar katuondokea.

 

Alikuwa ni mteshi, sikizani niwambie,
Hakupenda ya ubishi, upole ndio kazie,
Kamtwaa mwenye Arshi, Illahi Muumba yeye,
Kweli maisha ni moshi, ni nani atabakia.

 

Tulikuwa marafiki, ninaweleza mujue,
Katika kitabu hiki, kitachotoka badae,
Nawambia muswadiki, Somo nimetunga nae,
Amemtwaa Razaki, Illahi Mola Jalia.

 

Sina hamu ya kutunga, na kiu inishishie,
Kwa kuwa wetu Malenga, hivi sasa siko nae,
Illahi Muumba anga, twaomba tuhifadhie,
Kwa pepo zenye na kunga, Upate tuingizia.

 

Zatosha beti kidogo, heri hapa niishie,
Mithili pande la gogo, msiba umetungie,
In Sha Allah wake mzigo, kwa kuliani apawe,
Ili awe na vigogo, Swahaba na Tumwa Nabia.

 

Illahi ninakuomba, naomba nikubalie,
Uumfanyie wembamba, kaburini na badae,
Meupe kuliko pamba, kwa maisha yake yawe,
Na kaburi liwe nyumba, ya pepo ya kuvutia.

ALAMIN SIWA SOMO

'Malenga wa Mombasa'
Chuo Kikuu cha Kenyatta

Mombasa. 

Share Bookmark Print

Rating