http://www.swahilihub.com/image/view/-/2597938/medRes/927550/-/15flpcqz/-/BobOkoth.jpg

 

AII! BOB OKOTH TENA?

Bob Okoth

Bw Bob Okoth. Picha/HISANI  

Na LUDOVICK MBOGHOLI

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:30

Kwa Muhtasari

Mhariri mtajika, wa zama Taifa Leo,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Kifo cha Bob Okoth, nacho kilinisakama,

Kilinishukisha hadhi, mwili ukanitetema,

Nilidhani ni hadithi, gazeti niliposoma,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Kwa hakika kifo chake, moyoni kiliniuma,

Nilijihisi mpweke, kama kipande cha nyama,

Kidogo tu nianguke, sikwona mbele na nyuma,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Mbogholi nilishtuka, moyo ukanenda mbio,

Mhariri mtajika, wa zama Taifa Leo,

Ghafula katuondoka, hatuoni mwelekeo,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Nnakumbuka miaka, ilopita zama zake,

Hakujali matabaka, wala mume au mke,

Sote tulichanganyika, waandishi chini yake,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Bwana Bob mhariri, nyaka hizo zilopita,

Alipenda washairi, na wanamaoni hata,

Wanasalamu mahiri, pamoja na maripota,

Namlia bwana Bob , kumbe hayu nasi tena!

 

Bob alikuwa gwiji, kipenzi cha wote hata,

Alienzi wasomaji, wanachama wa WAKITA,

Akawa ni msemaji, wa kuzima vutavuta,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Enzi ya Hamisi Keya, mwenyekiti wa WAKITA,

Bob alikuwa geya, chama kukivutavuta,

Kiweze kuendeleya, Taifa Leo kumeta,

Namlia bwana Bob , kumbe hayu nasi tena!

 

Namkumbuka Opundo, mwanamaoni wa zama,

Alikizusha vishindo, akiwa ndani ya chama,

Bob akasema bado, WAKITA itasimama,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Walofata nyayo zake, ushauri walopawa,

Waume na wanawake, walokuwa na vipawa,

Leo hii teketeke, ni mabingwa wamekuwa,

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

Hapano nipumzike, kwa kufika kaditama,

Siandiki nitosheke, alazwe peponi pema,

Kwasababu kifo chake, Bob sote chatuuma!

Namlia bwana Bob, kumbe hayu nasi tena!

 

LUDOVICK MBOGHOLI

'Al-Ustadh-Luqman Ngariba-Mlumbi'

Taveta-Bura / Ndogo.