http://www.swahilihub.com/image/view/-/2597414/medRes/927271/-/jbfveuz/-/TFOMARBABU2101.jpg

 

AMETUAGA OMAR BABU

Kariakor, Nairobi

Marafiki na ndugu zake mwandishi Omar Babu wakiwa wamebeba maiti yake kuelekea makaburi ya Kariakor, Nairobi Januari 21 2015. Picha/ANTHONY OMUYA 

Na JAMES MUTWIRI WANJAGI

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  19:42

Kwa Muhtasari

Alo msomi aali, gonjwa kamfanya tuli,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

KIFO Babu mekabili, kamtwaa kikatili!

Abu Marjan ukweli, katunga kidijitali,

Kighafula ja ajali, ye kafa pasipo swali,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Alo msomi aali, gonjwa kamfanya tuli,

Kamwe aso uzohali, kasomeya uzamili,

Alolonga kulihali, jambo lugha kajadili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Katangaza kiwa mbali, sauti tamu dalili,

Mshairi kwelikweli, shairi jadi shughuli,

Lugha mustakabali, kapenda kama asali,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Jamani gani kauli, kuibwa Nguli kamili?

Mtunzi kote mahali, twaomboleza halali,

Jukwaani mbalimbali, akaghani si kalili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Akawa Mcheshi kali, kuandika hakufeli,

Kubuni yake amali, kukazana kakubali,

Aliyapinga madhili, malenga aso bahili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Ujerumani mahali, kapambana ja fahali,

Kaonyesha kiakili, tungoze ziso mithili,

Waama kajua ngeli, kaeneza Kiswahili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Katu hakuchoka mwili, ubunifu alijali,

Jagina kwetu twakuli, amfadhili Jalali,

Mwandishi tutaamali, hongera asitahili,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

Ninawaomba kibali, utunzi nt’ie kufuli,

Kapata tele medali, tungo zake afadhali,

Kiswahili lo jabali, galacha kote angali,

Jalia mlaze pema, mhadhiri Omar Babu.

 

JAMES MUTWIRI WANJAGI,

'Malenga Msifika'

 Chuka-Tharaka Nithi.