Wa Shinyanga nambieni

Na MAGDALENA MAREGESI

Imepakiwa - Thursday, July 14  2016 at  20:18

Kwa Muhtasari

Mi Shinyanga sijafika, yalikuwa maongezi,

Aliyenena Mayunga, kwenye zake simulizi,

Mi Shinyanga sijafika, yalikuwa maongezi,

Aliyenena Mayunga, kwenye zake simulizi,

Kasema wanarumanga, ugali bila mchuzi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Aliniambia Mayunga, kwao ni Maswa Mwanuzi,

Kuwa mwalima mpunga, kutafuta wanunuzi,

Kula nyie mwajivunga, mapishi hamyawezi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Kanisifia ujinga, kurudi kwao hawezi,

Matajiri wa kufuga, ng’ombe tele kwenye zizi,

Lakini nyumba kujenga, ni tembe boma la zizi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Kasema mkishachunga, katu hamna ajizi,

Mbina ya Mwanagandila,  jadi yenu kuienzi,

Ndiko kwenye chakulaga na kutafuta wapenzi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Kasifu mukijigamba, matajiri mwabarizi,

Kuwa ng’ombe wenu chapa, chini ng’ana matanuzi,

 Juu alama ya pamba viatu vya makubazi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Msimu unapofunga, pamba mwapata mavazi,

Vilabu mnavifunga, kwenye walwa manaizi,

Wanywaji mnawapanga, pombe nyie wanunuzi,

Wa Shinyanga nawambieni, kauli yake  Mayunga.

Beti  saba nazifunga, Wasukuma sema wazi,

Mayunga ndiye nyakanga, mkazi na mtambuzi,

Nena nicheke ujinga, nawasifu Wanyamwezi,

Wa Shinyanga nambieni, kauli yake Mayunga.

Mwisho