Na Mauya Omauya
(
email Mauya Omauya)
Kwa Mukhtasari
Kalonzo alipoteza hekima yote na kuvunja miiko ya siasabora. Wakati wa kura ya maoni kuhusu katiba, Kalonzo alishindwa kuamua waziwazi, akasalia anacheza mdundo wa ndiyo mchana na usiku akasakata ule wa la.
ALIYEZOEA vya kunyonga, vya kuchinja hawezi. Stephen Kalonzo Musyoka ni mwanasiasa aliyezoea vya kunyonga, hana uwezo kuchukua msimamo thabiti na anaamini njia zake za mkato hazifikii fahamu ya raia wa kawaida.
Katika ulimwengu wa Kalonzo Musyoka ni yeye pekee aliyesahihi na wengine wote wanasaka kumtilia kitumbua chake mchanga.
Lakini pwagu hupata pwaguzi na sasa anga yake Kalonzo imevurugwa baada ya wenzake Uhuru Kenyatta na William Ruto kuelekea kumtema kutoka kwa muungano ulio na nia ya kuchukua hatamu za uongozi pindi Rais Kibaki akistaafu.
Wafuasi wa Uhuru na Ruto wanasadiki Kalonzo hana nia safi katika muungano huo. Wanashuku anasubiri wawili hao waingie motoni Hague, naye apate kuvuna kura zao kwa kujipendekeza kama rafiki yao mkuu.
Mikakati hii ya Kalonzo imechukua muda mrefu tangu alipojitwika jukumu la kuzuru dunia kupinga shughuli za mahaka ya kimataifa ya ICC.
Alijiingiza topeni, akakaidi maoni ya wakenya wengi na kuvumilia fedheha ya juhudi zake kuambulia patupu.
Picha maarufu
Kuna picha moja maarufu Kalonzo amepigwa akimkumbatia marehemu Muammar Gaddafi.
Kalonzo alikuwa ameenda Libya kueneza injili ya kutaka ICC iruhusu Kenya kuendesha kesi za wale sita wa Ocampo. Kila nionapo picha hiyo, ninamhurumia Bw Kalonzo.
Ninamhurumia kwa sababa vitendo vyake havina hekima yoyote ya kisiasa. Alipojiunga na siasa Bw Kalonzo hakuhitaji hekima yoyote ya kufanya uamuzi au kuchukua msimamo kuhusu masuala muhimu ya kitaifa. Alichohitaji ni kuimba sifa za ‘Mtukufu’ Rais Moi.
Kalonzo hakuwahi kupinga maovu yaliyotendwa na utawala wa Kanu na uaminifu wake ulimfaa kwani amesalia bungeni tangu enzi hizo.
Kwenye ligi hii ya vibaraka kuna kina yakhe kama Sharif Nassir, Joseph Kamotho
Kwa kuzoea vya kunyongwa, Kalonzo amezoea miteremko na njia za mikato katika siasa.
Kuondoka kwa Moi mamlakani kulimuacha yatima. Japo muda mrefu umepita, Kalonzo anaamini atatumia ujanja ule ule aliotumia enzi za Moi na kufaulu kwenye miereka hii ya kizazi kipya.
Urafiki wa Kalonzo na Uhuru Kenyatta au William Ruto ni kipengele tu katika jitihada zake kupata njia ya mkato kufika ikulu.
Aliposafiri mataifa kadha ya Afrika kupinga ICC, alifanya kwa sababu ya tama yake, hakuwa anawaza Kenya, haki au amani nchini Kenya.
Kuwapokea kutoka Hague
Alipowapokea Ruto na Uhuru kutoka Hague kwa mara ya kwanza na kuandamana nao hadi Uhuru Park, labda alifahamu chombo chao kinazama na alinuia kujizolea ushabiki wa wafuasi wao. Katika mawazo yake, aliamini kwamba wawili hao wana kinyongo na Raila Odinga na iwapo hawatakuwa ulingoni wangeagiza wafuasi wao kumpigia Kalonzo kura,
Katika kusaka matunda ya tamaa hii ya maslahi yake, Kalonzo alipoteza hekima yote na kuvunja miiko ya siasabora. Wakati wa kura ya maoni kuhusu katiba, Kalonzo alishindwa kuamua waziwazi, akasalia anacheza mdundo wa ndiyo mchana na usiku akasakata ule wa la.
Hii ni kwa sababu mwelekeo wake wa siasa haujali falsafa yoyote ya usahihi wa msimamo wake, kilicho muhimu ni yeye apate njia ya mkato kusalia kileleni. Anapenda mno kujipata upande wa washindi hata kama mwenyewe hachangii ushindi huo.
Alipovuka na kuunga Rais Kibaki
Baada ya uchaguzi wa 2007, mbinu hii ya Kalonzo ilidhihirika pale alipovuka na kuunga mkono Rais Kibaki hata ilipokuwa wazi kwamba uchaguzio ulikuwa na utata. Hakuwaza iwapo ingekuwa kheri aongeze sauti yake kutaka matokeo ya uchaguzi wa urais yapigwe darubini. Aliona nafasi ya kujipata serikalini hata baada ya kugonga mwamba katika juhudi zake za kusaka urais.
Uhuru Kenyatta alifafanua tabia hii ya Kalonzo zaidi ya mwaka mmoja kwenye mkutano uliofanyika mjini Kericho. Alimfananisha Kalonzo na fisi anayetazama mwanadamu akitembea. Kila aonapo miondoko ya mikono kutokana na mwendo, fisi aliamini mkono huo utaanguka apate kitoweo.
Kwa ujinga wa fisi alifuata mwanadamu akisubiri mkono uanguke lakini wapi! Iwapo Uhuru Kenyatta na William Ruto watamtenga Kalonzo sina hata tone la chozi au kiwewe kuhusu hilo. Kalonzo si mwanasiasa wa kuaminika katika kundi, hana msimamo na amejaa ubinafsi, acha avune alichopanda.
mauyaomauya@live.com
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel