Na Mauya Omauya
(
email Mauya Omauya)
Kwa Mukhtasari
Mataifa kama vile Singapore, India, Korea Kusini na Malaysia ambayo yamelipua fataki ya kasi katika ustawi kiuchumi yalikuwa katika kiwango sawa na Kenya miaka ya sitini. Ruwaza iliyosukuma mataifa haya kuwa katika mstari wa mbele ni ile ambayo mataifa ya Afrika hasa Kenya haijasisitiza au kutilia mkazo.
KIPINDI cha uhuru wa Kenya, miaka ya sitini, Kenya na mataifa mengi ya Asia yalikuwa daraja moja katika ustawi.
Mataifa haya sawa na Kenya yalikuwa na doa la ukoloni na yalianza kujenga miundo misingi ya maendeleo na kujitegemea pindi tu minyororo ya ukoloni.
Mataifa haya ya Asia ambayo sasa yamelipua fataki ya kasi katika ustawi kiuchumi ni kama Singapore, India, Korea Kusini na Malaysia.
Ruwaza iliyosukuma mataifa haya kuwa katika mstari wa mbele ni ile ambayo mataifa ya Afrika hasa Kenya haijasisitiza au kutilia mkazo.
Mataifa haya kwa sasa yamevuka kutoka lindi la kusikitiwa, njaa, umaskini na ujinga.
Kila mataifa ya Afrika yanapopiga kite, kuombaomba misaada kutoka magharibi, kila anayejali hakosi kukumbusha Afrika kwamba miaka hamsini iliyopita masaibu yao yalikuwa sawa na Malaysia au Korea Kusini. Sasa Kenya imejaa bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka Asia.
Kutegemea utendakazi
Mataifa haya yamepiga hatua pia kama soko na chemichemi ya ajira kwa uzalishaji wa viwanda. Kwa sasa mataifa kama Uingereza na Amerika yanategemea pakubwa utendakazi wa raia wa mataifa haya.
Kwa sababu ya uwepo wa raia walio na ujuzi mkuu na elimu ya taaluma za kila aina, mataifa haya huvutia wawekezaji wanaosaka watu wa maarifa. India kwa mfano imeshamiri kama kitovu cha vijana walio na ujuzi mkuu katika teknolojia za tarakilishi na mawasiliano.
China inafahamika kama kiwanda cha ulimwengu; tazama bidhaa madukani na utaona ‘kimeundwa China’
Kuna kipengele kimoja cha ustawi kilichosukuma mataifa haya kujitwalia utukufu huu; elimu.
Kenya imebadilisha mfumo wa elimu mara mbili tangu uhuru na sasa tuna 8-4-4. Miongo michache tu Kenya imegundua labda 8-4-4 ina hitilafu na sasa kuna mapendekezo ya kubadili tena mfumo huu.
Yamkini mifumo hii yote haijafaulu kusukuma wanafunzi wawe tegemeo la ubunifu na kuchochea Kenya iwe kama wenzake wa Asia.
Kuna dosari moja ambayo imesibu elimu nchini Kenya.
Dosari yenyewe ina ukosefu wa kupiga akili za wanafunzi msasa wasiwe tu wakiwaza ushindani wa alama darasani bali wafunguke mawazo na kung’amua mbinu za kupekecha mazingira yao na kuyabadili yawe msaada kwa taifa na bara lao.
Elimu ya sasa inafinyanga mwanafunzi awe na dhamira tu ya kuajiriwa afisini na kujichumia kipato kinono.
Wanafunzi waliojitoa uhai baada ya matokeo ya KCPE hivi majuzi ni kielelezo cha utamaduni huu potovu wa ushindani sio wa maarifa bali wa alama darasani.
Kila Mkenya, hata walioajiriwa wako mbioni kutafuta stakabadhi za masomo ya juu ilmuradi waongezwe madaraka.
Vyuoni tunashuhudia wanafunzi wanaotumia ujanja, mlungula na hata mapenzi kujipatia alama za juu. Alama za juu pasipo maarifa ya taaluma na uwezo wa kuinua viwango vya uzalishaji au kuzaa vitega uchumi ni ishara ya udufu kwa taifa lolote.
Mashirika ya kimataifa
Sababu inayofanya mashirika ya kimataifa kama Microsoft na Apple kuweka viwanda vya teknolojia ya tarakilishi nchini India au Korea ni moja; kuna wataalamu walio sio tu na stakabadhi za elimu bali wana maarifa na uwezo wa kitaaluma kutenda kazi hiyo.
Elimu yetu imedorora kwa kuzingatia alama na cheo cha hela kuliko kusisitiza maarifa na uwezo wa mwanafunzi kugeuza mazingira yake kufaidi jamii na taifa.
Ngozi ivute ingali mbichi. Nchini Singapore, serikali inafahamu wazi umuhimu wa elimu kiasi kwamba walimu huteuliwa kutoka kwa wale waliofuzu daraja ya juu kabisa masomoni. Ikumbukwa kwamba hawa walimu watakuwa sio wa vyuo vikuu bali wa shule za msingi na chekechea.
Na malipo ya juu wanayopata yanaashiria manufaa wanayoletea jamii kupitia elimu.
Taaluma ya ukufunzi haiachiwi wale waliogonga mwamba vyuoni. Nchini Kenya, mambo ni tofauti.
Walimu wa shule za msingi ni wale waliokosa kufuzu kwenda chuo kikuu. Vijijini wengi ni walevi au wana biashara kando ili kukimu mahitaji yao kwa sababu ya mshahara wao mdogo. Hadi Kenya ibadili mwongozo wake kuhusu elimu, ushindani wa alama utaendelea na maarifa yatazidi kudorora.
mauyaomauya@live.com
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel