Tutosheke na mipaka tusonge mbele : Hatuwezi kuridhisha kila mtu

Imepakiwa Friday, February 3,   2012 | Na Peter Mwai
Profile

NIMESEMA mara nyingi na yamkini nitaendelea kulalamika kwamba Wakenya ni watu wasiotosheka. Ni sawa tu na wana wa Israeli, katika Biblia. Baada ya kukombolewa kutoka minyororo ya utumwa misri, walimtetesha Musa na Mungu wakisema heri wangeendelea kuishi huko wakila matunda na mboga badala ya “kufia jangwani”.
Nchini Kenya, shida ni kwamba wananchi wengi ni walafi na huhisi kuwa wana haki ya kumiliki kila kitu. Ndio maana ingawa imesifiwa an baadhi ya watu, ripoti ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuhusu maeneo bunge mapya imekosolewa.
Sitaki kutaja watu halisi, lakini nimekasirishwa sana na wanaoipinga. Hii ni kwa sababu, hawana msingi wowote wa kuipinga ila uroho na ulafi ulio nyoyoni zao.
Ninashangaa ikiwa hawa ni wale tu waliopiga kelele katiba mpya ipitishwe kwenye kura ya maamuzi Agosti 4, 2010. Wamegeuka na kukosoa yale yale waliyotetea.
Katiba yenyewe imesema wazi na kutoa mfumo unaofaa kutumiwa kuunda maeneo bunge mapya ndipo yafikie 290. Kwa kuwa kumekuwa na maeneo 210, ya uwakilishi, kunafaa kuundwa maeneo 80 mapya.
Mfumo wa kutumiwa unasema mipaka ya kila eneo inafaa ikaribiane sana, sawa na idadi ya watu. Idadi ya wakazi wa eneo bunge inaweza kuwa kubwa au ndogo kwa kiasi kisichozidi asilimia 40 katika majiji na yaliyo na watu waliotawanyika.
Katika sehemu nyingine, tofauti inaweza kuwa asilimia 30 pekee. Ni mwongozo huu uliotumiwa na iliyokuwa Tume Huru ya Muda ya Mipaka (IIBRC) iliyoongoza na Andrew Ligale.
Katika kubuni maeneo mapya, tume hiyo iliamrishwa na Katiba Mpya isivunjilie mbali eneo bunge lolote lililoko kwa sasa. Hili hata sasa limeendelea kutekelezwa na kwenye ripoti ya IEBC iliyozinduliwa Jumatatu iliyopita, hakuna eneo lolote la awali lilitupiliwa mbali.
Hii iliheshimiwa bila kujali kama eneo hilo lina watu wachache sana. Kilichotendeka katika maeneo mengi ni kwamba wodi kutoka maeneo jirani zilichukuliwa na kuongezwa kwa maeneo hayo kuyafanya yakamilike.
Kwa kutumia matokeo ya sensa ya 2009, yaliyoonyesha idadi ya watu nchini ni 38,610,097 na kugawa kwa kutumia maeneo bunge 290, hii inaonyesha eneo kamilifu linafaa kuwa na wakazi 133,138.
Ukitumia maelezo ya asilimia 40 juu ya usawa, maeneo yaliyo mijini kwa mfano Nairobi, Kisumu na Mombasa yanaweza kuwa na watu 186,393.
Katika maeneo mengine, idadi inaweza kwenda juu au chini kwa hadi asilimia 30 pekee ambayo ni sawa na 173,079 upande wa juu na 93,197 upande wa chini. Kwa kufuata mwongozo huu, ni maeneo 20 pekee ambayo hayakuguswa.
Mwenyekiti wa IEBC, Bw Isaack Hassan, na makamishan wamesema wazi kwamba katika baadhi ya maeneo mwafaka haukupatikana. Kama wamba ngoma, wakazi waliwasilisha mapendekezo ya kuwafaa binafsi na si eneo kwa jumla.
Katika kuitisha maeneo zaidi, tunafaa tuelewe kuwa hatuwezi kuongeza idadi zaidi ya 290 ila tu kwa kubadilisha katiba yenyewe. Isitoshe, hata kama tungekuwa na uhuru hatuwezi kuunda maeneo bunge kiholela kwani yatakuwa si maeneo bunge tena.
Ungeniuliza, au ungenipa uhuru wa kuamua, ningesema kijiji ninamotoka, kiwe eneo bunge kuhakikisha tunawakilisha vilivyo bungeni. Hii itatupa fursa ya kupokea vinono kutoka kwa bajeti ya taifa. Lakini hili ni tamanio tu na haliwezi kuwa.
Ningeshauri wote, tulidhike na tuliyopata na tulewe kuwa ni wenzetu waliopata.
Waliobahatika si raia wa Uganda au Tanzania, bali ni Wakenya wenzetu. Kwa kufanya hivi, tutaweza kuendelea mbele kama taifa na kuanza maandalizi ya uchaguzi mkuu.
Shughuli muhimu kama vile usajili wa wapiga kura na uchapishaji wa karatasi za upigaji kura haziwezi kuanza wala kuendelea bila mipaka ya maeneo bunge.
Aidha, shughuli za kiusimamizi ikiwa ni pamoja na uteuzi wa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo mbalimbali na kufunguliwa kwa afisi haziwezi kuendelea.
Wanaolalamika kuwa watabaguliwa kirasilimali, wanafaa waelewe kuwa mambo yamebadilika, na sera zitafuatwa kugawa mali ya nchi.

Share Bookmark Print

Rating

 

 

 

 

 

 

Most Popular

Wabunge 175 kutahiriwa Zimbabwe

Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume

Mwanawe Waziri wa Fedha ajitia kitanzi

MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi

Polisi waendelea kusaka walioshambulia Mombasa

Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,

Utengano wakumba ukumbusho wa Wanjiru

Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel