Na Peter Mwai
(
email Peter Mwai)
Kwa Mukhtasari
Ikiwa tarehe ya uchaguzi itabaki kuwa siri, huenda kusiwe na nafasi ya kutekeleza Sheria za Uchaguzi.
KWA muda sasa, imekuwa kama ada kuhusishwa mwaka 2012 na uchaguzi mkuu. Lakini uamuzi wa Mahakama Kuu siku chache zilizopita umeonyesha kuwa hili huenda lisiwe.
Uamuzi wa majaji, Isaac Lenaola, Mumbi Ngugi na David Majanja, ulieleza kuwa uchaguzi unaweza kufanyika ikiwa Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga watasikizana na kuvunja Serikali ya Muungano.
Hili lizipofanyika, uchaguzi utafanyika baada ya siku 60 kufuatia kumalizika kwa muhula wa bunge la sasa, ambao majaji walisema unakamilika Januari 14, 2013.
Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ina jukumu la kuamua tarehe halisi ya uchaguzi kuambatana na mamlaka iliyopewa na katika katika hali zote mbili.
Rais Kibaki na Bw Odinga wakivunja Serikali au muhula wa Bunge umalizike, IEBC itatakiwa kutangaza tarehe itakuwa kabla ya kumalizika kwa siku hizo 60.
Badala ya kutoa mwelekeo, majaji yamkini waliongeza kukanganyikiwa miongoni mwa umma na hili limedhihirishwa na hisia mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa kutoka kila upande.
Tarehe ambazo zimependekezwa ni Agosti 14, kuambatana na Katiba inayosema uchaguzi uwe Jumanne ya pili ya Agosti ya mwaka wa tano.
Kuna wale wanaosema uchaguzi uwe Machi 2013.
Waziri Mutula Kilonzo naye alijitokeza na kuwasilisha mswada wa marekebisho ya katiba akitaka uchaguzi mkuu ujao uwe Jumatatu ya pili ya Desemba mwaka huu, ambayo ni Desemba 17.
Waziri huyu ameonekana kuchanganyikiwa hasa baada ya uamuzi wa mahakama. Amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema ataondoa mswada na kwamba anaunga mkono uchaguzi wa Machi.
Kinachozua utata zaidi ni muhula wa Rais Kibaki unaofaa kumalizika Desemba 29 mwaka huu suala kuu likiwa, ikiwa uchaguzi utafanyika Machi, nani ataongoza miezi hiyo miwili?
Ni kutokana na hali hii ambapo Rais Kibaki na Bw Odinga wanafaa kukutana upesi na kutia saini mkataba wa mapema wa kuvunja Serikali zaidi ya siku 60 kabla ya Desemba 29.
Hii itahakikisha kwamba mrithi wake anajulikana mapema na kulainisha shughuli ya mpito.
Zitahitajika zaidi ya siku 60 kwani katiba ya sasa imeweka muda kati ya tarehe ya uchaguzi na tarehe ya kuapishwa kwa rais mpya ikiacha nafasi ya watu kuwasilisha malalamishi ya kupinga matokeo kabla ya matokeo hayo kurasmishwa.
Ili kuupa uzito mkataba huo, unafaa ufanywe wazi kwa kuchapishwa magazetini au uwe kama mswada wa sheria wa kurekebisha Mwafaka wa Kitaifa.
Ingawa hatua hii itahakikisha uwazi, najua haitafurahisha wabunge ambao walihakikisha muhula wao wa miaka mitano unalindwa kabla ya kuunga mkono katiba 2010.
Ili kuwaridhisha, ningependekeza walipwe mishahara yao ya miezi iliyosalia mradi tu wakubali kutuacha kwa amani. Pesa watakazolipwa si nyingi kulipo matuna tutakayopokea kwa kuandaa uchaguzi utakaohakikisha uthabiti wa nchi.
Najua wataunga mkono pendekezo kama hili haraka kwani litawahakikisha pesa za kutosha za kuendesha kampeni. Si neno, lakini waneni husema lisilo budi hubidi.
Sababu yangu kuu ya kutaka Rais Kibaki na Bw Odinga watie saini mkataba wa mapema wa kuvunja Serikali ni matakwa ambayo yamo kwenye Sheria za Uchaguzi zinazofaa kuwa msingi wa uchaguzi mkuu ujao.
Wanasiasa kwa mfano wanapaswa kutoshiriki michango ya harambee miezi minane kabla ya tarehe ya uchaguzi. Maafisa wa umma nao wanafaa kujiuzulu miezi saba kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Ikiwa tarehe ya uchaguzi itabaki kuwa siri, huenda kusiwe na nafasi ya kutekeleza sheria hii.
Huwezi kuanza kuhukumu watu na kuwazuia kuwania nyadhifa mbalimbali kwa kutenda kosa ambalo wakati wa kutendeka kwalo halikuwa kosa.
Tayari tulishuhudia IEBC ikionya kuhusu harambee Desemba, na pia maafisa kutakiwa wajiuzulu kabla ya Januari 14 kwa kufuata tarehe ya Agosti 14.
Baadhi wanapinga uchaguzi wa Machi wakisema utaingilia ratiba za shule na nyingine za kibinafsi lakini nawataka wanipe tofauti yake na Agosti. Kuna wale wanaopendekeza kugawanywa kwa uchaguzi, ule wa urais uwe Desemba na wa wabunge na madiwani Machi. Hili litaongeza tu mzigo kwa kuweka Kenya katika kipindi cha kampeni. Lakini linawezekana kwani nchi nyingi hufanya hivi.
pmwai@ke.nationmedia.com
Wabunge 175 nchini Zimbabwe watapashwa tohara kufikia mwisho wa mwezi ujao katika juhudi za kuhamasisha wanaume
MWANAWE Waziri wa Fedha Njeru Githae anadaiwa kujiua nyumbani kwao Runda, Nairobi. Polisi wameanzisha uchunguzi
Polisi wameanzisha msako mkali kutafuta washukiwa waliotekeleza shambulio la kigaidi katika mkahawa wa Bella Vista,
Ibada mbili tofauti zilifanywa kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha bingwa wa marathon katika Olimpiki Samuel