Kiswahili bado ni mtoto wa kambo huku kwetu Kenya

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, January 30  2019 at  10:13

Kwa Muhtasari

Hata katika mapambano dhidi ya ufisadi kuna chembechembe cha utambuzi wa Kiswahili katika harakati na hamkani za kitaifa.

 

KINA CHA FIKIRA

MNAMO wiki iliyopita nilihudhuria kongomano la kitaifa dhidi ya ufisadi.

Na mpaka sasa sijui kwa nini ndugu zetu Watanzania hupenda kuuita ufisadi rushwa.

Sikuwa na hakika kama lilidhamiria kutuhamasisha dhidi ya ufisadi au kutufundisha mbinu mwafaka zaidi za ufisadi.

Nilitoka huku nikiwa na mseto wa matumaini na kutokuwa na matumaini.

Matumaini kwa sababu kwa mara ya kwanza niliona Wakenya wanajadiliana waziwazi na tena katika mawanda rasmi kabisa kile wanachokiona kama janga la kitaifa.

Bango la kongomano lilikuwa kauli mbiu katika maandishi ya Kiswahili yanayosema: “Pamoja tuangamize ufisadi.”

Neno ‘pamoja’ siku hizi linabeba vivuli vya mirengo ya kisiasa, lakini hilo lisitufumbe macho tusione fahari ya kongomano kuongozwa na kauli mbiu iliyoandikwa kwa Kiswahili.

Haiwi hivyo siku zote.

Hata katika mapambano dhidi ya ufisadi kuna chembechembe cha utambuzi wa Kiswahili katika harakati na hamkani za kitaifa.
Nilitaka kuona kama wajumbe wa kongomano wataruhusiwa kutoa maoni yao kwa uwazi na ujasiri. Pili nilitaka kuona kama Kiswahili kitapewa kipaumbele katika mdahalo mzima. Kuhusu utoaji wa maoni, wajumbe wa kawaida kama mimi hatukuruhusiwa kupaaza sauti. Tuliundiwa wenzo wa mtandao mahsusi kutuma maoni yetu ambayo yalirushwa kwenye viwambo. Ni juu yako ewe msomaji kuamua kama tija ya kuruhusiwa kuandika maoni kunafidia hasara ya kutoruhusiwa kutamka waziwazi kila mtu kwa kinywa chake mwenyewe.
Niliona kwamba wote waliozungumza ni wale waliokuwa wameratibiwa kuzungumza. Mama mmoja aliyejaribu kupaaza sauti muda mfupi kabla rais Uhuru Kenyatta kuingia ukumbuni, alitoswa nje. Mpaka sasa sijui alichotaka kukisema hasa maana hawakumpa fursa ya kumwaga dukuduku la moyoni mwake. Je, huenda ikawa yule mama (ambaye kwa mbali nikidhani alikuwa anazungumza Kiswahili), alikuwa na suluhisho (napenda hili neno hapa kuliko suluhu) kwa janga la ufisadi nasi tumemtilia mguu wa kausha?
Basi tuje kwa wasemaji walioratibiwa kuzungumza. Idara muhimu serikalini ziliwakilishwa, si bunge la Senati, si bunge la taifa, si serikali kuu, si serikali za kaunti, si idara ya mahakama, si walinda usalama na wapelelezi wa jinai. Isitoshe, tasnia mbalimbali pia ziliwakilishwa ikiwemo ile ya vyombo vya habari, muungano wa wanataaluma, dini na vijana. Karibu kila msemaji alizungumza Kiingereza, kama nilivyotarajia. Hata balozi wa Marekani Robert Godec alipowasalimu wajumbe kwa Kiswahili, “Humjambo? Niaje?” walionekana kushangaa.

Kiswahili

Mkurugenzi wa mashtaka ya umma, Bw Hajji ndiye peke yake aliazimia kuwasilisha hotuba yake kwa Kiswahili.

Alifafanua kwa Kiswahili fasaha kidogo hamasa yake ya kuangamiza ufisadi na changamoto zinamkabili yeye na idara yake. Kama kuna mtu aliyeeleweka vizuri zaidi na Wakenya waliomsikiliza redioni au kumtazama kwenye runinga basi ni huyu Bw Hajji. Baadaye rais Uhuru na Raila walijaribu kutupatupa maneno mawili matatu ya Kiswahili. Wengine wote walikuwa wanawahutubia mabalozi wa kigeni.
Hitimisho: Kiswahili bado ni mtoto wa kambo nchini Kenya.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara" 

 

 

Mauko ya Bhalo na Kimaro yametuacha hoi kwa kweli

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, January 16  2019 at  16:48

Kwa Muhtasari

Marehemu Mwalimu Hugholin Kimaro anazikwa Ijumaa, Januari 18, 2018, kule Rombo, Tanzania, karibu na eneo la mpaka la Loitoktok.

 

MAJIRA ya majonzi ndiyo kauli inayofumbata vizuri msimu tulio nao sisi wapenzi wa Kiswahili kwa sasa. Watu wanapenda kuambiana “Happy New Year!” au “Mwaka Mpya wenye Fanaka!” kauli ambayo sasa inapoteza maana hasa mwaka wenyewe unapoanza kwa tanzia baada ya tanzia.

Haya yanaonekana maneno matupu au mawanio, (neno la Prof Mugyabuso Mulokozi), yasiotimia hasa kutokana na kuondokewa kwa mkumbo mmoja na Mwalimu Hugholin Kimaro na Malenga Ustadh Ahmed Nassir, Malenga wa Mvita.

Tanzia za wenzetu hawa zimeniacha hoi hata sijui niseme nini? Labda mwanzo nimpisha shabiki wangu mmoja kutoka Mombasa, Mohamed Shaaban ambaye ameniletea habari zifuatazo kumhusu Ahmed Nassir: “Makiwa! Huenda Kusema Ahmad Nassir amekufa kukawa ndio ukweli ila si uhalisia.

Uhalisia ni kuwa ameondoka.Hii inatokana na ukweli Kuwa athari za Maisha yake zingalipo! Bwana Ahmad Nassir almaarufu malenga wa Mvita hakuacha vitabu na wana tu kama idhaniwavyo atakumbukwa kwavyo; ameacha ushairi ambao ni pambo la lugha chambilecho mwendazake Shaaban Robert.

Binafsi nilimpa mwanangu Jina Ahmad aliyezaliwa tarehe Saba mwezi Machi mwaka 2013 baada ya kukutana na Ahmad Nassir mwezi Februari mwaka 2013 nikiwa pamoja na marehemu Omar Babu.

Mkutano wetu alasiri  ile ulinidhihirishia kuwa wapo Watu wanaouishi ushairi hasa.

Bwana Bhallo alipozungumza  kama alikuwa akikariri mishororo ya nudhuma alizoandika.Ni sadikifu kuwa mwenye mkahawa tuliokuwemo alifurahishwa mno na uwepo wetu mle kwani chai nyingi ilinywewa na mazungumzo ya sauti za kunong'ona kiasi cha kutomsumbua yeyote yaliendelea.

Miongoni mwa kauli zake ni ile ya ukwelikinzani Kuwa 'Kuna tofauti Katika usawa'. Bwana Bhallo hakuona usawa Katika maisha haya tuishimo na kuipambanua Kauli hiyo Kwa Vina na mizani nisielewe no Sadfa tu au aliazimia. Tuliagana naye majira ya magharibi tusionane naye tena hadi mwishoni mwa mwaka 2014 nilipomzuru tena nikiwa na Abu Marjan.

Wenzangu katika kurasa hizi kama vile Mwalimu Henry Indindi na Mwalimu Bitugi Matundura walinitangulia kuandika mengi kumhusu mwalimu Hugholin Kimaro aliyetuacha mkono. Nitamkumbuka mwalimu Kimaro kwa uraufu wake na uungwana wake. Alinihoji mara nyingi na kuchapisha makala kuhusu kazi zangu na maisha yangu.

Mara nyingine akinihoji kuhusu kazi za wengine, mathalan makala yake nzuri sana kuhusu mchango wa Shaaban bin Robert kwa fasihi ya Kiswahili. Katika makala hiyo alisifia uwezo wa Shaaban kuchangia Kiswahili pakubwa ingawa alikuwa na kitembo cha chini kabisa cha masomo.

Nilidiriki kufanya kazi na Mwalimu Kimaro kwa ushirikiano mkubwa sikwambii kualikwa naye  katika shule mbalimbali alikofundisha niwahamasishe wanafunzi kuhusu Kiswahili.

Mnamo 2014 alinipeleka katika shule moja ya msingi huko Kamulu ambako bintiye  kitindamimba Jacklyne alikuwa anakaribia kuufanya mtihani wa darasa la nane.

Alitaka hata bintiye ahamasike.

Hakika aliwahamisha wengi si haba, nikiwemo mimi.

Tunaziombea faraja familia za wenzetu hawa wakati huu wa jitimai.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara" 

 

 

Uchambuzi wa kina kuhusu dhana ya maana

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Thursday, December 20  2018 at  07:48

Kwa Muhtasari

Aghalabu huwezi kuchambua maana katika lugha ambayo huelewi miundo yake na utamaduni wake.

 

Na MARY WANGARI

HUWEZI kuchambua maana katika lugha ambayo huelewi miundo yake na utamaduni wake. Hata hivyo, maana ya maana bado ni ngumu na ina utata sana. Kwa mujibu wa Matinde (2012:237) neno maana hudokeza fahiwa (sense) nyingi sana.

Mifano ifuatayo inaonyesha utata wa neno maana katika kila sentensi linamotumika

 

i. Una maana gani kutojibu sms yangu?

ii. Kufuka kwa moshi kuna maana kuwa mahali hapo kuna moto.

iii. Mchoro wa fuvu la binadamu una maana ya hatari.

iv. Mradi huu una maana kubwa sana kwetu.

vi. Asiyejua maana haambiwi maana. 

vii. Kumbe yule mtu hana maana hata kidogo.

viii. Kweli nilisema hivyo lakini sikumaanisha. 

ix. Juzi ilinyesha mvua ya maana maeneo ya Moshi.

 

Kutokana na fasili hizi za maana, tunaweza kugundua kuwa kuna utata mkubwa unaolizingira neno maana kwani linadokeza fahiwa zisizo na ukomo. Hata hivyo, uchunguzi wa sifa za ufasiri wa maana ni sehemu muhimu katika taaluma ya semantiki au isimu maana.

 

Alama au Ishara na Maana

Taaluma ya semantiki ni taaluma ndogo katika taaluma iitwayo Semiotiki au Semiolojia.Semiolojia/ Semiotiki ni taaluma ya alama na ishara katika kuashiria maana Wakati semantiki huchunguza alama za lugha za binadamu na maana zake, semiolojia huangalia alama na ishara mbalimbali katika kupata maana mbalimbali.

Kuna aina tatu za ishara

  1. Ishara za usababisho/index

  2. Ishara za ufananisho/ icons

  3. Ishara za nasibu au ishara nasibu

Ishara za usababisho/index

Kuna kufungamana kwa kiusababishano kati ya alama au ishara na kile kinachoashiriwa. Hii inamaanisha kwamba jambo moja husababisha jambo la pili. Kwa mfano:

moshi - alama ya moto

mawingu - alama ya mvua

 

Ishara za ufananisho/ icons

Hapa kufanana kwa kipicha kati ya ishara na kinachoashiriwa. Kwa mfano picha ya mtu mke au mume katika milango ya vyoo. Au mchoro wa kitu na kitu chenyewe. Mfano ramani ya nyumba, picha ya mtu.

 

Ishara za nasibu au ishara nasibu

Katika ishara hizi, hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya ishara na kitu kinachoashiriwa lakini uelewekaji wake hutokana na mazoea tu. Kwa mfano, jina la mtu. Ishara hizi ndizo zilizopo katika lugha kwa kiasi kikubwa ingawa ishara za usababisho na ufananisho zipo pia. Kwa mfano Bendera kama kiashiria cha kikundi au chama/nchi inayoiwakilisha.

Rangi nyekundu kama kiashiria cha hatari/mapenzi na kadhalika.

Baruapepe ya mwandishi: marya.wangari@gmail.com

Marejeo

Kihore, Y. M, Massamba, D.P.B na Msanjila, Y.P. (2003). Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TUKI.

Massamba, D.P.B, Kihore, Y.M na Msanjila, Y.P (2004). Fonolojia ya Kiswahili Sanifu. Sekondari na Vyuo. Dar es Salaam: TUKI.

Mgullu, R. S. (1999). Mtalaa wa Isimu, Fonetiki na Fonolojia ya Lugha ya Kiswahili. Nairobi: Longhorn Publishers.

Je, una swali, maoni au mapendekezo kwa Swahili Hub? Tuandikie kupitia baruapepe: swahilihub@ke.nationmedia.com

 

 

Tukumbatie wingilugha ili kukabili changamoto nyingi za kimawasiliano

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, December 19  2018 at  08:53

Kwa Muhtasari

Tukipende Kiswahili na hata wengi wetu tuwe tuko tayari kukifia ikibidi, lakini tusiachwe tupitwe na umuhimu wa wingilugha.

 

@KenWalibora

 

KINA CHA FIKIRA

SIKUJUA tija ya wingilugha hadi nilipozuru Senegal kwa mara ya pili mwezi huu unaofunga mwaka wa 2018.

Mwaliko wa kuhudhuria na kuwasilisha mada katika kongomano la Baraza la Ukuzaji Utafiti wa Sayansi za Jamii baranani Afrika (CODESRIA) imenifikisha katika nchi ya mwanafalsafa na kiongozi wa Kiafrika Leopold Senghor kwa mara ya pili maishani mwangu.

Mara ya kwanza kuzuru Senegal ulikuwa mwaka 2015. Katika kongomano la kwanza sikuwasilisha, nilikuwa mtazamaji, au niseme nilikuwa mwanahabari aliyeshuhudia wasomi wenzangu wakila uhondo wa taaluma. Safari hii hata mimi nimo.

Nilikuwa katika rubaa ya wajumbe kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Afrika waliowasili Jumapili jioni katika uwanja wa jiji kuu la Senegal Dakar.

Punde tulilakiwa na wenyeji wetu na wengi wao hawazungumzi Kiswahili wala Kiingereza. Wao ni weledi wa Kiwolof na Kifaransa, hasa dereva wa basi lililotutoa uwanja wa ndege mpaka katikati ya jiji.

Nilikaa mbele na dereva ili nione vizuri mandhari ya nchi hii ya Sadio Mane wa Liverpool. Nikimuuliza swali dereva kwa Kiingereza ananijibu kwa Kifaransa au Kiwolof.

Potelea pote, nikaamua kusema naye Kiswahili!  Hata siku moja sijawazia kufanya kazi ya kuchekesha watu, (au uchale), lakini unaweza kukisia jinsi abiria wote garini walivyoangua kicheko, hata dereva mwenyewe.

Yaani kumbe hiki Kiswahili tunakijua na kukienzi lakini mara nyingine kinachekesha tu, hakiwezeshi mawasiliano kila pahali na kwa kila mtu. Kiswahili changu kilikuwa kikwazo kwa mawasiliano na dereva ambaye labda ni mtu wa nasaba wa Alhajj Diouf wa zamani Liverpool. Naye kashindwa kufanikisha mawasiliano kwa Kiwolof au Kifaransa chake.

Ndipo alipotokea ndugu yetu mmoja msomi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, akaokoa jahazi.

Msomi huyo alikuwa mweledi wa Kifaransa cha dereva na Kiswahili changu. Mara moja akalitwaa jukumu la kuwa mkalimani na kuwezesha mawasilino kati yangu na dereva wetu. Ndipo wiki hii niliamua sharti niandike kuhusu uwingilugha, yaani kuwapo na lugha nyingi au mtu kuwa na umilisi wa lugha nyingi. Nawazia ndugu yetu Mkongo anayezungumza Kilingala, Kifaransa, Kiswahili na Kiingereza. Baadaye kongomano lilipoanza, tulijulishwa kwa msomi mmoja anayezungumza Kibambara, Kihausa, Kiarabu, Kifaransa, Kiingereza na lugha nyingine nyingi.

Sote wajumbe katika kongomano tuliachama kwa hilo na kumshangilia msomi huyu si haba.

 

Vipaji

Usicheze watu wana vipaji ati. Na hata kwetu Afrika Mashariki kuna watu wenye vipaji vya kujua lugha nyingi. Mfano mtangazaji wa mpira Benardo Otieno niliyewahi kufanya naye kazi KBC, na NTV, ambaye akikijua Kijaluo, Kiingereza, Kikamba, Kifaransa, Kijerumani, Kitaliano, Kikikuyu na lugha nyingine nyingi.  Wengine ni msanii na mwanahabari Lolani Kalu na marehemu rafiki yangu Omar Babu maarufu kwa jina Abu Marjan.

Nawahusudu hawa. Tukipende Kiswahili na hata wengi wetu tuwe tuko tayari kukifia ikibidi, lakini tusiachwe tupitwe na umuhimu wa wingilugha.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"

 

 

Baadhi ya shule zakosea kuharamisha matumizi ya Kiswahili nje ya darasa la somo la lugha hii ashirafu

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Thursday, December 13  2018 at  08:15

Kwa Muhtasari

Sikumbuki kuwahi kuona rubaa kubwa namna ile ya wanahabari na kamera na kalamu zao kama nilivyowaona huku Embu kwa ajili yangu!

 

GAZETI la Daily Nation la Desemba 4, 2018 limebeba habari ya tamko langu kuhusu marufuku dhidi ya kuzungumza Kiswahili shuleni Kenya.

Limetoa tamko hilo nikiwa ziarani Embu nilipoalikwa na Dkt Timothy Kinoti kwa niaba ya Chuo Kikuu cha Embu kuhutubu.

Marafiki zangu wengine kama vile Enock Bitugi Matundura wamenitaarifu kwamba tamko langu limesikika pia katika runinga moja muhimu humu nchini.

Hilo la kupewa umaarufu kwa kauli yangu niliyoitoa katika unyonge wangu sikutarajia. Nilifikiria kwamba ziara yangu ya Embu ilikuwa ziara ndogo ya mtu mdogo katika Chuo Kikuu chenye ukubwa wa kutisha.

Nilikuwa nikifikiria kuhusu polisi wa trafiki walionihangaisha karibu na mji wa Embu kwa madai kwamba leseni yangu ya kuendesha gari ilikuwa imepitwa na wakati.

Ilikuwa leseni ya miaka mitatu na tarehe yake ya kuongezwa muda ilipita kwa siku chache.

Sikuwa na habari. Lakini waliniruhusu kuenda chuoni nitoe hotuba yangu. Hata hivyo, niliamua kukata leseni upya mjini Embu ili kuondokana na bughudha.

Kama ni hatia kwa dereva kuendesha gari bila leseni au na leseni ambayo muda wake umepita hilo, linakubalika.

Na hili la mwanafunzi Mkenya kuambiwa ni hatia kuzungumza Kiswahili ni dhambi, si hatia tu.

Ndiyo maana nilitamka nilivyotamka kwa wanahabari walionisakama Embu punde baada ya hotuba yangu iliyosikilizwa na hadhira kubwa sana ya jumuiya ya Chuo Kikuu cha Embu.

Swali

Sikumbuki kuwahi kuona rubaa kubwa namna ile ya wanahabari na kamera na kalamu zao kama nilivyowaona huku Embu kwa ajili yangu! Hata ninapokwenda kwetu kijijini ambako sina jina jingine ila “Mtoto wa Mwalimu!” mapokezi kamwe hayawi kama haya ya Embu.

Basi hapo ndipo mwanahabari mmoja mkakamavu aliponiuliza kuhusu sheria ya baadhi ya shule nchini kuharamisha matumizi ya Kiswahili nje ya darasa la somo la lugha hii.

Hii kwa kweli ni tanzia.

Kwa nini Kiswahili kiharamishwe ilhali ni somo la lazima katika mfumo wetu wa elimu? Mbona kizungumzwe tu wakati wa somo la Kiswahili? Kiingereza kinatumika hata nje ya mawanda ya ufundishaji wa Kiingereza. Walimu wa Historia, Hesabati, Kemia, Jiografia, Bayolojia, wote wanatumia Kiingereza.

Kwenye gwaride viranja na walimu wa zamu na walimu wakuu wanatoa hotuba zao aghalabu kwa Kiingereza. Wanafunzi wengine wanasemezana wao kwa wao kwa Kiingereza hicho hicho. Labda wengine wanapolala wanaota kwa Kiingereza.

Huku kukwezwa kwa Kiingereza kunachusha na kuchosha. Aidha kunaenda kinyume na katiba na mwelekeo wa maendeleo endelevu ya kanda na utandawazi.

Katiba inasema Kiswahili ni lugha ya taifa na lugha rasmi ya Kenya. Mwafaka wa kuundwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki unakipa Kiswahili hadhi ya kuwa lugha ya mawasiliano mapana. Hivi karibuni bunge la Afrika Mashariki limekipisha Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jumuiya.

Kuna mantiki gani kuharamisha shuleni kama si ucharamu?

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"

 

 

Nakisi ya misamiati mwafaka kuhusu dhana fulani husukuma wazungumzaji kutumia maneno yasiyofaa

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, November 28  2018 at  08:06

Kwa Muhtasari

  • Mtu hawezi kuwa na habari moja tu; ana nyingi

  • Nduma ni najimbi au magimbi

 

MPWA wangu alinipigia simu majuzi yale kutoka kaunti ya Trans Nzoia. Baada ya salamu akanidokezea kwamba wakulima kwa sasa wanaanza kuvuna zao la mahindi. Majira ya janguo kama mwalimu wangu Salim Bakhresa alivyokuwa akiniambia katikati ya miaka ya themanini. Wakati huu wa janguo ndipo wakulima wa Trans Nzoia hudiriki kuhesabu gharama- wanatathmini tija, hasara na nakisi ya shughuli zao za mashambani. Kwa miaka michache iliyopita wamekuwa  wakililia bei duni ya zao lao. Naibu wa rais William Ruto amewashauri waanze hivi karibuni wawekeze katika maparachichi na matunda mengine. Kama watu wa Trans Nzoia wana tatizo la kushuka kwa zao lao la mahindi basi pia wana nakisi  nyingine ya maneno mwafaka kuelezea baadhi shughuli zao.

Mathalan wakishavuna mahindi wao husema “wanayakongoa.” Je mahindi hukongolewa? Hilo waulize watu wa Trans Nzoia.  Kamusi Kuu inasema kwamba kongoa ni “toa kwa nguvu kitu kilichopigiliwa au kuchomekwa mahali fulani; ng’oa, chomoa. Je, baada ya kuvuna wakulima hung’oa mahindi au kuyachomoa? . Misumari iliyogongomelewa inaweza kukongolewa au kung’olewa. Mahindi hayakongolewi.  Hiyo hiyo Kamusi Kuu inasema kitenzi “kokoa” kinamaanisha “pukuchua mahindi ili upate punje.”  Nadhani hili ndilo watakalolifanya watu wa Trans Nzoia katika msimu huu wa janguo.

Zingatia kwamba nimesema “misumari iliyogongomelewa,” wala sio misumari iliyogongwa kama baadhi yetu tusemavyo mara nyingine. Siku zote katika Kiswahili sanifu  tunasema misumari  inagongomelewa.  

Mpwa wangu aliendelea kunieleza kuhusu mji wa kwao na namna mifugo wanavyoendelea kunawiri.  Akataja kwamba kuna ng’ombe jike amezaa “njau.” Njau ni nini? Njau ndilo neno wanalotumia watu wa Trans Nzoia kuelezea ndama, yaani mtoto wa ng’ombe. Hilo wamelitoa wapi? Sijui ila nafikiria labda kwa lugha mojawapo za humu nchini kama vile Kikikuyu. Wanahitaji mtu wa kuwaambia katika Kiswahili sanifu, huwa tunasema ndama sio njau.

Isitoshe, mpwa wangu ukimsalimu “habari zako?”  hujibu “mzuri.”

Trans Nzoia sharti pawe pahali pa watu wengi wazuri. Kila unayemsalimu “habari zako?” kama mpwa wangu, anataja kwamba yeye mzuri. Walakini swali lile “habari zako?” linalenga habari, sio yeye msalimiwa. Aghalabu wa wajuao hujibu nzuri au njema, maana habari ndizo zinazozungumziwa.  Wala si habari moja kama watu wa Trans Nzoia wanavyopenda kuuliza wanapowasilimu watu: “Habari yako?”  Mtu hawezi kuwa na habari moja tu; ana nyingi. Hili ni swali linajumuisha masuala mengi si suala moja. Kwa hiyo hapa tena, si sahihi kumsalimu mtu: “Habari yako wewe?

Na nakisi ya msamiati mwafaka inayowakumba watu wa Trans Nzoia, ndiyo nakisi inayowakumba hali kadhalika Wakenya wengi. Kama hawakusema njau basi watapachika neno jingine la kikwao. Mathalani utawasikia wakisema “odede” badala ya panzi. 

Au inakuwa kama nilivyoambiwa na mhudumu wa mkahawani Mwea mapana Novemba kwamba palikuwa na “nduma” mkahawani, badala ya majimbi au magimbi.

 

 

Usiivyoge lugha kimatumizi iwapo huimanyi barabara

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, November 21  2018 at  10:38

Kwa Muhtasari

Waandishi chipukizi wasijisumbue kuisarifu lugha wasioitalii ipasavyo.

 

NINAPENDA kusikiliza idhaa ya Kiingereza ya BBC sio tu kwa sababu ya kuarifiwa, kuburudishwa, na kufundishwa bali pia kwa sababu ya lugha nzuri ya watangazaji wake.

Watangazaji hao aghalabu husarifu lugha kwa heba na mvuto wa aina yake. Mpenzi wa lugha hapa nilipo, siwezi kukichukia Kiingereza kwa sababu ya kukipenda Kiswahili.

Hata hivyo, mapema wiki hii nimechukia Kiingereza cha BBC.

Alitokea ripota mmoja akawa anaripoti kuhusu masaibu ya mazeruzeru katika Kisiwa cha Ukerewe.

BBC walimbebesha mzigo mkubwa wa kuwasilisha ripoti yake kwa Kiingereza.

Katika dakika mbili au tatu alizowasilisha ripoti yake, hakuna hata sentensi moja ya Kiingereza iliyokuwa sahihi. Mwanahabari huyu maskini kalazimika kuaibisha Afrika Mashariki duniani kwa Kiingereza cha ajabu ajabu.

Mara “They come from different part of the country” mara “The government operate in this area,” n.k.

Mimi nasema kama lugha huiwezi achana nayo.

Mimi leo ukiniambia nizungumze Kifaransa siwezi, maana sikijui mbele wala nyuma yake.

Ndivyo ilivyo ukiniambia nizungumze Kikerewe, Kikamba, Kihausa, Kichina au Kirusi. Kiingereza naweza kidogo, kwa hiyo nitajitahidi niseme mawili matatu.

Sidhamirii kujitanua kifua, lakini Kiingereza nilichokisikia kutoka kwa yule ripota kilinishtua. Nilijiuliza maswali mengi sana. Mwanzo, je ilikuwa lazima awasilishe ripoti yake kwa Kiingereza? Amelazimishwa au amejilazimisha?

Hilo lanikumbusha mdahalo wa tangu jadi wa lugha ya uandishi kwa waandishi wa Kiafrika.

Vigezo

Ni vigezo gani anavyopaswa kuvitumia mwandishi kuchagua lugha ya maandishi yake? Mhakiki wa Kinaijeria, Obi Wali alisema kwamba fasihi ya Kiafrika ilikuwa haina mustakabali kwa vile waandishi wengi wamekimbilia kuandika lugha za kigeni.

Alidai fasihi ya Kiafrika inaelekea kudumaa kutokana na uteuzi mbaya wa lugha.

Ingawa waandishi kama vile Chinua Achebe waliibuka na kutetea matumizi yao ya Kiingereza kubeba tajiriba yao ya Kiafrika, suala la uteuzi wa lugha bado halijapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Ukweli ni kwamba waandishi wa Kiafrika wanaoandika kwa kutumia lugha asilia kama vile Kiswahili, Kiigbo, Kisomali na Kizulu, hawajulikani nje ya mipaka ya lugha zao na vijiji vyao.

Kuhusu Kiswahili hata wapo wanaodai si lugha ya Kiafrika bali inayotokana na Kiarabu. Watu wameandika hata vitabu na kuwafundishia mamilioni ya wanafunzi katika mifumo ya elimu kwamba ndivyo ilivyo asili ya Kiswahili. Kiswahili kimekoseshwa Uswahili na Uafrika wake na kuarabishwa.

Ushauri wangu kwa waandishi chipukizi siku zote huwa ni kwamba ni heri kuandika katika lugha inayokutirikia kwa mazoea.

Lugha ambayo ukiyaita maneno yanaitika kwa urahisi. Kwa baadhi ya waandishi lugha hiyo inaweza kuwa ni lugha yao asilia au lugha ya mawasiliano mapana kule wanakotokea.

Ilimuradi lugha anayoichagua mwandishi inakuwa chombo cha kuwasilishia ujumbe wa sanaa yake, si hoja kama yeye ni mzawa au si mzawa wa lugha hiyo.

Tatizo linazuka wakati anakosa ujuzi wa kukitumia chombo hiki kama mwanahabari aliyetuborongea Kiingereza.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"

 

 

Kiswahili cha kitaaluma si kigumu kama tunavyodhani

Na MGENI WETU

Imepakiwa - Tuesday, November 20  2018 at  10:43

Kwa Muhtasari

Baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu kuliko hata za Kiingereza.

 

Na ERASTO DUWE

KATIKA mijadala mingi iliyohusisha matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia, baadhi ya watu wamekuwa na mtazamo kwamba istilahi za Kiswahili ni ngumu kuliko hata za Kiingereza.

Watu hao wamekuwa na mtazamo kuwa ni vyema Kiingereza kikaendelea kutumika kwa kuwa wanakiona ni rahisi katika ufundishaji na ujifunzaji kuliko Kiswahili.

Hata hivyo, katika makala hii, lengo si kuibua mjadala wa Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia katika viwango mbalimbali ya elimu, la hasha, hilo limeshalijadiliwa sana katika mijadala mingi na watu mbalimbali wametoa maoni.

Katika makala hii lengo hasa ni kujadili ikiwa kweli Kiswahili cha kitaaluma ni kigumu au la.

Awali ya yote tunapozungumzia Kiswahili cha kitaaluma tunamaanisha aina ya lugha (msamiati na istilahi maalumu) itumikayo kufundishia masomo mbalimbali kama vile Biolojia, Kemia, Hisabati, Jiografia na masomo mengineyo katika ngazi mbalimbali za elimu.

Jibu la mtazamo huo kwamba Kiswahili hicho ni kigumu linaweza kuwa na sura mbili tofauti. Ikumbukwe kwamba, watumiaji wengi wa Kiswahili wamezoea kutumia Kiswahili cha kawaida kwa ajili ya kukidhi mawasiliano yao.

Kiswahili cha mawasiliano, kinajichomoza katika sura mbili. Wapo watumiaji wa Kiswahili wanaokitumia katika mawasiliano bila kujali urasmi wake.

Kwa maneno mengine, wao huongea tu bila kujali wanazingatia taratibu za lugha hiyo au la. Kwa sababu hiyo, hata kama wanabananga kwao si tatizo ilimradi tu wakidhi mawasiliano yao.

Kwa upande mwingine, wapo watumiaji wa Kiswahili wanaokitumia huku wakijali sana uzingativu wa taratibu au sarufi ya lugha.

Miongoni mwa hao ni pamoja na wasomi katika uga huo wa Kiswahili na baadhi ya vyombo vya habari.

Lugha yoyote ya kufundishia, kwa kawaida inaangukia katika kundi la lugha rasmi.

Urasmi huo hujitokeza katika kufuata taratibu mbalimbali (sarufi ya lugha) na kuwa na istilahi maalumu za taaluma husika tofauti na lugha ya kawaida ya mawasiliano.

Ikumbukwe pia kwamba hata Kiingereza ambacho baadhi ya watu hukiona kuwa ni rahisi kama lugha ya kufundishia na kujifunzia, dai lao si la kweli.

Kuna tofauti kati ya Kiingereza cha kawaida kitumikacho katika mawasiliano na kile kitumikacho katika ufundishaji wa masomo mbalimbali. Tofauti yake ni kwamba, Kiingereza kitumikacho kufundishia, kina istilahi nyingi na pengine kina mfumo maalumu kutegemeana na somo husika.

Haiyumkiniki wasemao Kiingereza cha kufundishia ni rahisi kuliko Kiswahili, wanaongea hivyo kwa sababu tu ya mazoea, yaani Kiingereza wamekizoea kufundishia na kujifunzia hususan katika kiwango cha sekondari na vyuo.

Kiswahili kinaonekana kigumu kwa kuwa hakitumiki kama lugha ya kufundishia katika viwango tajwa. Istilahi zake zinaonekana ngumu kwa kuwa hakijazoeleka.

Endapo kingekuwa kinatumika tangu muda mrefu uliopita kama ilivyo kwa Kiingereza, wasemao hivyo wangekizoea na kukiona rahisi kama wakionavyo Kiingereza.

Hata hivyo, ifahamike kuwa, lugha ya kutolea taaluma mbalimbali ni tofauti na lugha ya kawaida ya kimawasiliano.

Utofauti huo hutokana na sababu tulizokwisha zitaja kwamba, lugha ya kufundishia ina istilahi zake kutegemeana na somo husika; ina mfumo wake maalumu na nduni nyinginezo.

Istilahi kutotumika sana

Kwa hivyo, tunaweza kusema kuwa, Kiswahili cha kufundishia kinatazamwa kuwa kigumu kwa kuwa istilahi zake hazitumiwi sana.

Kwa upande mwingine, Kiswahili cha namna hiyo si kigumu kwa kuwa tayari zana kama kamusi zipo na endapo ufundishaji kwa Kiswahili utafanyika, kitazoeleka na kuonekana cha kawaida kama Kiingereza kinavyochukuliwa na watu wenye mtazamo huo.

Kilicho muhimu ni Watanzania kujikubali kuwa tuna Kiswahili kama tunu yetu ya kujivunia. Ugumu au urahisi wa maneno katu usiwe sababu ya kukidunisha Kiswahili kikakosa nafasi yake stahiki.

Kilicho chako hakiwezi kuwa kigumu na itoshe tu kusema kuwa hata hicho Kiingereza tunachokikumbatia nacho kina maneno lukuki magumu

Lakini haya hayaonekani, yanaonekana maneno magumu ya Kiswahili. Tafadhalini Watanzania tupende kilicho chetu.

 

Erasto Duwe anapatikana kwa simu namba +255713646322

 

 

Wanahabari mahiri wanaokitetea Kiswahili kwa uvumba na ubani

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Tuesday, November 6  2018 at  07:04

Kwa Muhtasari

Zama zile redio ikisema basi ni hivyo.

 

ZAMANI za utoto wangu redio ilitawala. Redio ilikuwa mali ya umma. Ukiwa na redio, unasikiliza na wengine, sio peke yako. Na kama redio imesema kitu basi ni hivyo.

Redio ikisema mtu amefariki basi amefariki. Mpaka leo nakumbuka vipindi mahsusi vilivyorushwa hewani kuchangia ukuzaji wa Kiswahili.

Kuna kipindi cha lugha kilichokuwa kinarushwa na Redio Tanzania, Dar es Salaam. Wazee mikota wa lugha kama Hamisi Akida, Salim Kibao na Jumanne Mayoka walikuwa wakijadili masuala anuwai ya lugha.

Nilikuwa sipitwi na vipindi hivyo. Vilinifundisha mengi katika lugha ya Kiswahili.

Walikuwa wakishatamka wazee hao basi redio imesema, na redio ikisema basi ni kweli.

Nchini Kenya Sauti ya Kenya ilikuwa na wazee kama vile Abdalla Barua, Abdalla Mwasimba, Hassan Mwalimu Mbega, Jay Kitsao, Karega Mutahi na Mohamed Bakari.

Wazee hawa walijadili fani mbali mbali za lugha na kutufumbua macho kuhusu usahihi wa kusema na kuandika. Miaka ilipopita majina mapya nayo yakaingia katika jopo la mabingwa.

Wakaibuka magwiji kama Kyallo Wadi Wamitila, Kazungu Kadenge, John Habwe, Rayya Timammy na Said A. Mohamed na Mwenda Mbatiah ambao walichangia kunogesha kipindi na kutufundisha Kiswahili. Walipozungumza, redio ilikuwa imesema, na redio ikisema basi ni hivyo.

Nimekumbuka historia hii yote kwa sababu nimeona hivi karibuni kama redio inatawala bado ingawa inatawala sambamba na vyombo vingine vya ushawishi mkubwa kama vile runinga na mitandao ya intaneti. Ilikuwa furaha ilioje kuona redio na runinga zimeunganishwa katika kurusha mbashara kipindi cha Kamusi ya Changamka katika enzi ya QTV na QFM.  Munene Nyaga na Nuhu Zuberi Bakari waliwafundisha wengi Kiswahili katika kipindi hicho. Isitoshe, Redio Citizen nayo ilikuwa pia na kipindi cha Bahari ya lugha ambapo Ali Hassan Kauleni na Jilani Wambura walikuwa wakizamia lulu na wakiwafundisha wasikilizaji kuhusu maswala mbalimbali ya lugha. Katika kipindi hiki cha baada ya kutoweka kwa QTV na QFM, na kipindi cha Bahari ya Lugha angalao bado kuna majukwaa ya kukiendeleza Kiswahili.

Mathias Momanyi yupo mstari wa mbele katika kipindi chake cha kila Jumamosi katika Redio Taifa. Naye Ali Hassan Kauleni na wenzangu kama Mwalimu Abubakar Tsalwa na Mwalimu Titus Sakwa na guru Ustadh Wallah bin Wallah, wanaendelea kutupa nuru ya Kiswahili katika kipindi cha Nuru ya Lugha kwenye Redio Maisha.

Mabingwa wawili

Isitoshe, nilifurahi sana kuwaona mabingwa wawili wa QTV na QFM, Munene Nyaga na Nuhu Bakari wakitumia runinga nyingine kutetea na kufundisha lugha.  Hata TBC nao huku Tanzania wamejitahidi kurushwa runingani vipindi vya Kiswahili kila Jumamosi.

Ninafarijika kuona kwamba mambo yaliyotekelezwa na wazee wa zamani, hayakupotea wala kwenda arijojo. Kipo kizazi kingine cha wakeretwa kilichopokezwa mikoba na kinaendeleza ufundishaji na utetezi wa Kiswahili kwa kutumia vyombo vya habari.

Nasema heko kwenu mabingwa nyote kwa juhudi zenu.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"

 

 

Wanahabari mahiri wanaokitetea Kiswahili kwa uvumba na ubani

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Tuesday, November 6  2018 at  07:04

Kwa Muhtasari

Zama zile redio ikisema basi ni hivyo.

 

ZAMANI za utoto wangu redio ilitawala. Redio ilikuwa mali ya umma. Ukiwa na redio, unasikiliza na wengine, sio peke yako. Na kama redio imesema kitu basi ni hivyo.

Redio ikisema mtu amefariki basi amefariki. Mpaka leo nakumbuka vipindi mahsusi vilivyorushwa hewani kuchangia ukuzaji wa Kiswahili.

Kuna kipindi cha lugha kilichokuwa kinarushwa na Redio Tanzania, Dar es Salaam. Wazee mikota wa lugha kama Hamisi Akida, Salim Kibao na Jumanne Mayoka walikuwa wakijadili masuala anuwai ya lugha.

Nilikuwa sipitwi na vipindi hivyo. Vilinifundisha mengi katika lugha ya Kiswahili.

Walikuwa wakishatamka wazee hao basi redio imesema, na redio ikisema basi ni kweli.

Nchini Kenya Sauti ya Kenya ilikuwa na wazee kama vile Abdalla Barua, Abdalla Mwasimba, Hassan Mwalimu Mbega, Jay Kitsao, Karega Mutahi na Mohamed Bakari.

Wazee hawa walijadili fani mbali mbali za lugha na kutufumbua macho kuhusu usahihi wa kusema na kuandika. Miaka ilipopita majina mapya nayo yakaingia katika jopo la mabingwa.

Wakaibuka magwiji kama Kyallo Wadi Wamitila, Kazungu Kadenge, John Habwe, Rayya Timammy na Said A. Mohamed na Mwenda Mbatiah ambao walichangia kunogesha kipindi na kutufundisha Kiswahili. Walipozungumza, redio ilikuwa imesema, na redio ikisema basi ni hivyo.

Nimekumbuka historia hii yote kwa sababu nimeona hivi karibuni kama redio inatawala bado ingawa inatawala sambamba na vyombo vingine vya ushawishi mkubwa kama vile runinga na mitandao ya intaneti. Ilikuwa furaha ilioje kuona redio na runinga zimeunganishwa katika kurusha mbashara kipindi cha Kamusi ya Changamka katika enzi ya QTV na QFM.  Munene Nyaga na Nuhu Zuberi Bakari waliwafundisha wengi Kiswahili katika kipindi hicho. Isitoshe, Redio Citizen nayo ilikuwa pia na kipindi cha Bahari ya lugha ambapo Ali Hassan Kauleni na Jilani Wambura walikuwa wakizamia lulu na wakiwafundisha wasikilizaji kuhusu maswala mbalimbali ya lugha. Katika kipindi hiki cha baada ya kutoweka kwa QTV na QFM, na kipindi cha Bahari ya Lugha angalao bado kuna majukwaa ya kukiendeleza Kiswahili.

Mathias Momanyi yupo mstari wa mbele katika kipindi chake cha kila Jumamosi katika Redio Taifa. Naye Ali Hassan Kauleni na wenzangu kama Mwalimu Abubakar Tsalwa na Mwalimu Titus Sakwa na guru Ustadh Wallah bin Wallah, wanaendelea kutupa nuru ya Kiswahili katika kipindi cha Nuru ya Lugha kwenye Redio Maisha.

Mabingwa wawili

Isitoshe, nilifurahi sana kuwaona mabingwa wawili wa QTV na QFM, Munene Nyaga na Nuhu Bakari wakitumia runinga nyingine kutetea na kufundisha lugha.  Hata TBC nao huku Tanzania wamejitahidi kurushwa runingani vipindi vya Kiswahili kila Jumamosi.

Ninafarijika kuona kwamba mambo yaliyotekelezwa na wazee wa zamani, hayakupotea wala kwenda arijojo. Kipo kizazi kingine cha wakeretwa kilichopokezwa mikoba na kinaendeleza ufundishaji na utetezi wa Kiswahili kwa kutumia vyombo vya habari.

Nasema heko kwenu mabingwa nyote kwa juhudi zenu.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"

 

 

Kiingereza ni tishio kwa lugha nyingine kote ulimwenguni?

Ken Walibora Na KEN WALIBORA

Imepakiwa - Wednesday, October 31  2018 at  07:37

Kwa Muhtasari

  • Suala zima la ukoloni wa lugha ya Kiingereza limejadiliwa.

  • Si Kiswahili tu, hata Kijerumani, Kifaransa na Kireno, lugha zote hizi zinatishiwa na uwepo duniani kote kwa Kiingereza kinachosambaa kama ugonjwa wa ebola.

 

UKOLONI wa Kiingereza ni wazo la kutisha ingawa kwa wengine ni jambo lisilofikirika. Wanakienzi Kiingereza kana kwamba kwenda ahera au mbinguni kunategemea kukifahamu.

Hili suala limejadiliwa hivi karibuni katika kongomano la School of Oriental and African Studies (SOAS) nchini Uingereza.

Kongomano liliandiliwa kumuenzi Prof Farouk Topan aliyestaafu zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Wamefanya vizuri sana kumuenzi Topan mwandishi na msomi aliyetopea na aliyefundisha kwingi, tokea kwao Zanzibar na London. Linalonishangaza ni vile wanavyokumbuka umuhimu wa kuwa na kongomano la kumuenzi miaka 15 baada ya yeye kustaafu. Ila hilo silo linalonichochea kuandika makala leo.

Aidha bora niseme sikualikwa kwenye kongomano hili la London. Wapo baadhi ya marafiki zangu walialikwa na kuwepo kwao kulitosha. Sina shaka walifanya kazi kubwa katika hafla hiyo ya ya kumuenzi Mzee Topan Farouk kwa mchango wake katika taaluma za Kiswahili. Isipokuwa niseme tu kwamba rafiki yangu mmoja walimwalika pasina kumpa ufadhili, imebidi marafiki kuchanga ili kumwezesha kufika London.

Muhimu hapa kufanyika mkutano Uingereza na suala zima la ukoloni wa lugha ya Kiingereza limejadiliwa. Yaani vidokezi nilivyopewa, maana sikuwapo, ni kwamba wanakongomano walijasiria kuongelea tishio la Kiingereza kwa maenezi ya lugha nyingine duniani.

Si Kiswahili tu, hata Kijerumani, Kifaransa na Kireno, lugha zote hizi zinatishiwa na uwepo duniani kote kwa Kiingereza kinachosambaa kama ugonjwa wa ebola. Utalielewa hili vizuri ukiwatazama vijana wa Kichina wanashindania usemaji fasaha wa Kiingereza katika vipindi vya redio nchini China au vile watoto wa Kifaransa na Kijerumani wanavyowania kukimanya Kiingereza yaani “Kiswahili cha dunia,” chambilecho hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Utaelewa hili ukasikiliza maneno kama yale ya mama mmoja aliyepiga simu katika Radio Citizen au Radio Maisha majuzi yale na kusema yupo Lodwar anasomea masomo ya ngumbaro, “masomo ya baada ya chamcha” kama alivyosema mwenyewe. Na ingawa lengo lake lilikuwa kuwatakia watahiniwa wa mitihani ya kitaifa heri njema na mafanikio, na kuwaomba wasiibe mitihani, alijitahidi kupita kiasi kuonesha kwamba kweli anasoma kisomo cha watu wazima. Vipi? Alihamisha ndimi mara moja na kuanza “How are you? Good Morning? Good Afternoon?

Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia

Kasumba kwamba mtu hakusoma kama hawezi kuzungumza Kiingereza inatawala, sio Lodwar au Kenya tu, bali dunia nzima kwa kiasi fulani. Na kama tulivyomnukuu Nyerere akisema Kiingereza ndicho Kiswahili cha dunia.

Hili tunaweza kuliona kiutumwa kuwa jambo zuri au tulione lilivyo hasa katika uhasi wake kama ithibati ya ukoloni wa Kiingereza. Mbona yule mama hawezi kuchagua kutusabahi kwa Kiturkana chake, “Ejokh?” au kwa Kiswahili na bado athibitishe kwamba kasoma bila kugeukia Kiingereza.

Sikualikwa katika kongomano la Uingereza ila nawapongeza waandalizi na wajumbe kwa ujasiri wao wa kuukemea ukoloni wa Kiingereza duniani. Siku nyingine wakinialika nitawapa maoni yangu ya mlalahoi kama yaliyomo katika makala hii.

"Kwa sasa Ken Walibora ni mkurugenzi wa Kituo cha Taaluma za Lugha na Ulimwengu katika Chuo Kikuu cha Riara"