Matoleo mengi ya kamusi ni ithibati lugha inakua

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, June 28  2016 at  10:20

Kwa Muhtasari

Ukweli ni kwamba, katika taaluma ya elimu, mikabala ya kutaja jambo lile lile ni mingi jinsi ilivyo idadi ya watu ulimwenguni.

 

UKWELI ni kwamba, katika taaluma ya elimu, mikabala ya kutaja jambo lile lile ni mingi jinsi ilivyo idadi ya watu ulimwenguni.

Kauli hii inanipa idhini ya kutoa mtazamo wangu kuhusu makala ya mwandishi Enock Nyariki, 'Hakuna kamusi faafu ya Kiingereza – Kiswahili’ (Taifa Leo, Juni 23, 2016).

Kwenye makala hayo, Bw Nyariki anahisi kwamba idadi ya kamusi za Kiswahili ambazo zimekwisha kuchapishwa katika karne ya 21 ni ishara ya maendeleo ya Kiswahili.

Mwandishi huyu hata hivyo alitahadharisha wachapishaji wa kamusi hizo dhidi ya kuingiza 'msamiati uchwara (?)’ kwenye kamusi mpya kwa kisingizio kwamba msamiati wenyewe umekolea katika matumizi ya kila siku.

Onyo

Alionya pia kwamba kutofanya hivyo kutazua hali ambapo mashirika ya uchapishaji yataishia kuchapisha 'kamusi za Sheng’ yakidhani kwamba ni kamusi sanifu za Kiswahili.

Mwandishi alisema kwamba baadhi ya maneno ya Sheng yaliyoingizwa kwenye baadhi ya kamusi ni msamiati 'poa’.

Kadhalika, Bw Nyariki anaonekana kukerwa na hali ambayo msamiati unahusu watu au makabila ambayo hayahusiani kwa damu wala usaha na historia ya Kiswahili umeingizwa kwenye baadhi ya kamusi.

Kufikia hapa, mwandishi Nyariki anaonekana kutamatisha awamu ya kwanza ya Makala yake na kuingia katika awamu ya pili ambapo anasema lengo la Makala yake – kuangazia umuhimu wa kuwepo kwa kamusi mwafaka ya Kiingereza – Kiswahili.

Mwandishi Nyariki anashangaa kwamba Mmishenari, Fredrick Johnson aliwapiku wazawa wa lugha ya Kiswahili kwa kuandika A Standard English- Swahili Dictionary (Oxford, 1939).

Matini

Nimenukuu kwa marefu matini ya Bw Nyariki kwa lengo la kuyachokonoa na kutoa mtazamo kuhusu suala hili zima.

Kwanza, kulihitajika muumano kati ya sehemu mbili za makala yake.

Pili, nahisi kwamba kauli ambazo nimezitilia alama (?) si za kweli.

Hakuna msamiati 'uchwara’ katika lugha yoyote iwayo. Haiyumkiniki kamusi yoyote iwayo kuweza kusheheni kila neno, istilahi au msamiati katika lugha.

Badilika

Hii inatokana na sababu ya kimsingi kwamba lugha inabadilika kila uchao na kuna dhana ngeni zinazozuka. Ndiposa wanaleksikografia wanajitahidi kuboresha kamusi na kutoa matoleo mbalimbali.

Ukweli ni kwamba, mchakato wa uandishi wa kamusi daima huwa ni kama mzunguko wa dunia na hakuna siku utawahi kukoma. Mwandishi alitaja kuwepo kwa matoleo ya kwanza na pili ya English-Swahili Dictionary (TUKI).

Kauli hiyo ni ithibati tosha ya kuonesha kwamba lugha zinakua kwa kasi mno na ni shughuli ghali mno kuandaa kamusi.

Utunzi wa kamusi si jambo rahisi watu wengi wanavyofikiria.

Tatu, neno 'poa’ ni la Kiswahili sanifu na hulka ya Sheng ni kwamba, ina maneno ya Kiswahili sanifu na maneno ya lugha nyingine kutoka lugha nyingine.

Nne hakuna hatia ya mashirika ya uchapishaji kuchapisha Kamusi za Sheng. Kwa hakika, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI) ambayo sasa inaitwa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili imechapisha Sheng-English Dictionary : Deciphering Africa’s Underworld Language iliyotungwa na msomi wa Kiswahili Ireri Mbaabu na Nzuga Kibande.

Mapengo

Kwamba Kamusi ya Johnson ina mapengo mengi ni kauli ya kawaida kwa sababu Fredrick Johnson hakuwa mwanaleksikografia na hivyo basi si ajabu kwamba kamusi yake ina matatizo.

Isitoshe, lengo lake la kutunga kamusi lilikuwa ni kumwezesha kufanikisha shughuli zake za kueneza injili wala haikuwa shughuli ya kiakademia.

Nilikuwa mmoja wa wahariri wa Kamusi ya Karne ya 21 (Longhon, 2011) na ninafahamu fika changamoto zinazoikumba taaluma ya leksikografia ya Kiswahili.

Vilevile, maneno katika kamusi za Kiswahili si lazima yawe ya makabila yanayohusiana na Waswahili tu.

Kiswahili kimepasua kingo zake na kuwa lugha ya dunia.

'Vuvuzela’

'Vuvuzela’ kwa mfano si msamiati wa kabila linalohusiana na Waswahili.

Kwamba Kiswahili kinatohoa sana, utohozi ni jambo la kawaida kwa lugha ambayo haina dhana zile katika utamaduni wake; kuwepo kwa vivuli vya maneno (hakuna usawe katika lugha yoyote iwayo na vivuli vya maneno ni jambo la kawaida) na kadhalika.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka na alikuwa mhariri msaidizi wa Kamusi ya Karne ya 21 (Longhorn, 2011)

 

 

Uandishi wa kazi za kibunifu hauhitaji nguvu za uchawi

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, June 23  2016 at  14:47

Kwa Muhtasari

Kwa takriban kipindi cha miaka mitano ambacho nimefundisha nimekuwa nikishuhudia 'utasa’ wa waandishi chipukizi waliopitia katika mikono yangu – kwa misingi kwamba, hapajakuwapo hata mwanafunzi wangu mmoja ambaye amechapisha kazi ya kubuni.

 

MOJAWAPO ya kozi ambazo ninafundisha katika chuo kikuu ni 'uandishi wa kubuni katika Kiswahili’.

Kwa takriban kipindi cha miaka mitano ambacho nimefundisha nimekuwa nikishuhudia 'utasa’ wa waandishi chipukizi waliopitia katika mikono yangu – kwa misingi kwamba, hapajakuwapo hata mwanafunzi wangu mmoja ambaye amechapisha kazi ya kubuni.

Nilipokuwa nikiajabia hali hii na kuelekea kukata tamaa; kwamba 'huwezi kumfunza mtu kuwa mwandishi wa kubuni’ (kwa kuwa waandishi huzaliwa wala hawaandaliwi), mmoja wa wanafunzi wangu wa zamani, Bw Samuel Mwenda alinipigia simu akiniambia kwamba amekwisha kuchapisha riwaya inayoitwa Mvuvi na kampuni ya Nsemia Inc., Toronto, Canada.

Iwapo mwandishi wa kubuni huzaliwa akiwa na uwezo wa kuandika au anaweza kufundishwa kuandika – hilo ni suala la mjadala.

Hata hivyo, katika makala ya leo ninaangazia jinsi ambavyo mwandishi wa kubuni anavyoweza kupata au kuzua visa vya kutungia.

Ninapotanguliza somo hili katika vipindi vyangu chuoni, huwafahamisha wanafunzi kwamba 'uandishi wa kubuni si uchawi’.

Je, waandishi wa kubuni hutoa wapi visa wanavyovitungia? Swali hili ni muhimu kwa sababu haiwezekani mtunzi yeyote awaye kutunga kwenye ombwe.

Sharti pawe na chemchemi ambayo kutoka kwayo, waandishi wa tungo za kibunifu huteka visa vya kutungia. Kazi yoyote inayozingatia uyakinifu wa kijamii ina kiwango fulani cha ubunifu na kiwango cha uhalisia wa maisha.

Yaani, tungo zote za kibunifu zina ukweli fulani unaoakisi hali halisi anamokulia mwandishi.

Kwa mfano, ili tumwelewe Ebrahim Hussein (yaani maana ya kifasihi katika tungo zake), tunaweza kujikita kwenye matini ya kazi zake pekee, tunaweza kurejelea mazingira na tajriba zake maishani, muktadha, au msomaji akatumia tajriba zake binafsi kusimbua msimbo katika kazi za Hussein au tukaangalia mwingiliano-matini.

Mwandishi yeyote yule wa tungo za kubuni hutegemea hisi, moyo na mikono yake katika kutekeleza jukumu la uandishi.

Kwa hivyo, mwandishi wa kubuni huweza kuona, kusikia, kuonja, kuhisi na kunusa mambo mbalimbali ambayo hatimaye anayaandikia.

Mbinu

Kimsingi, kuna njia nyingi ambazo mwandishi anaweza kufuata ili kuzalisha matini za kiubunifu.

Njia hizi ni pamoja na fikra, matembezi, mazungumzo na watu wengine au wataalamu, vyombo vya habari (magazeti, redio, runinga, mtandao wa intaneti au wavuti, fasihi nyinginezo au hata ndoto.

Tukio la hivi majuzi la kuuawa kwa mfanyabiashara Jacob Juma kwa njia isiyoeleweka ni msingi mzuri sana kwa mwandishi anayetaka kuandika riwaya ya kiupelelezi.

Ingawa nimekwisha kutaja kwamba uandishi wa kubuni si uchawi, mtu yeyote anayepania kuwa mwandishi atakayeacha taathira katika jamii sharti awe tayari kusoma kwa marefu na mapana fasihi za watu wengine pamoja na kazi nyingine katika taaluma mbalimbali kama vile falsafa, elimu, fizikia, kemia, biolojia na kadhalika.

Kwa kuwa malighafi ya mwandishi na nyenzo anayotumia kuwasilisha mawazo yake ni lugha, mtu yeyote anayetaka kuwa mwandishi ni sharti awe mjuzi na mweledi wa lugha.

Watunzi wazuri wa kazi za kifasihi wana uwezo wa kuifanya lugha iwatumikie jinsi wapendavyo.

Baada ya kupata kisa cha kutungia na kuimudu lugha ya kusimulia kisa chenyewe, mwandishi sharti aketi chini na kutunga.

Siri ya kufanikiwa katika uandishi ni kuandika – wala hakuna njia nyingine ya kufanikiwa katika fani hii. Labda kabla ya kujitosa katika bahari ya uandishi, ni muhimu kwanza mtu ajifunze kuogelea katika bahari hiyo kwa sababu ni shughuli inayowahitaji watu wenye mioyo ya chuma – wasiokata tamaa na wala wasioandika kwa malengo ya kujipatia hela.

Ni vigumu sana kupata shilingi hata moja kutokana na uandishi wa kazi za kubuni.

Ikiwa unataka kupata hela kutokana na uandishi, basi ningependekeza kwamba uandike vitabu vya kiada. Huko ndiko kuna hela.

Aidha, isichukuliwe kwamba kila kazi inayochapishwa ni bora.

Katika taaluma ya uandishi wa kubuni hasa katika Kiswahili, kuna watu wanaong’ang’ania kutunga hata pale ambapo hakuna kipawa.

Mimi huwaita waandishi wa aina hii 'waandishi wa masafa mafupi’. Wala idadi ya vitabu anavyotunga mtu haimaanishi kwamba inamfanya kuwa mwandishi bora.

Kuna watunzi kama Mohamed Suleiman Mohamed waliotunga kazi tatu tu – yaani riwaya za Nyota ya Rehema, Kiu na mkusanyo wa hadithi fupi wa Kicheko cha Ushindi, basi.

Lakini huwezi kuizungumzia fasihi ya Kiswahili bila angalau kumtaja mwandishi huyu.

 

 

Kuna haja ya kufufua leksikoni ambayo ilikufa?

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, April 7  2016 at  09:49

Kwa Muhtasari

Jukumu kubwa la vyombo vilivyotwikwa mamlaka ya kustawisha lugha katika mataifa mbalimbali limekuwa ni kubuni istilahi kukidhi mahitaji ya elimu na mawasiliano.

 

JUKUMU kubwa la vyombo vilivyotwikwa mamlaka ya kustawisha lugha katika mataifa mbalimbali limekuwa ni kubuni istilahi kukidhi mahitaji ya elimu na mawasiliano.

Baadhi ya asasi zinazotekeleza jukumu hili ni Kituo cha Istilahi za Ufundi cha Uswidi, Baraza la Lugha ya Taifa [Dewan Bahasa dan Pustaka] nchini Malaysia, Akademia ya Kihibrania ya Uyahudi na Baraza la Lugha la Taifa la Tanzania (BAKITA).

Asasi nyingine zinazochangia katika maendeleo ya istilahi au msamiati ni vyombo visivyo vya serikali ambavyo huunda istilahi zinazohusiana na shughuli zavyo.

Katika kundi hili tuna vyombo vya habari kwa mfano Taifa Leo.

Mtaalamu Hermans Mwansoko anasema pia kwamba huko Malaysia, Kampuni ya Shell imejishughulisha sana katika uundaji wa istilahi zinazohusu uchimbaji na usafishaji wa mafuta katika lugha ya Kimalaysia.

Vyombo vingine vya kimataifa vinavyojishughulisha na uundaji wa istilahi ni Shirika la Uchumi la Ulaya, Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Ubora wa Viwango.

Mwansoko anasisitiza kwamba mchango wa vyombo hivi mara nyingi hujikita katika istilahi zinazohusu shughuli zao katika lugha kuu za ulimwengu au lugha za wanachama wao.

Kwa bahati mbaya, Kenya haina chombo cha kiserikali kinachoshughulikia mchakato wa uundaji, usanifishaji na usambazaji wa istilahi.

Kutokana na pengo hili, watu binafsi wamejitokeza kufidia hali hii. Baadhi ya wataalamu wanaotumia raslimali zao kuchangia katika maendeleo ya leksikoni nchini Kenya ni pamoja na Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa, Profesa Rocha Chimerah (Chuo Kikuu cha Pwani) na Profesa Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi.

Mkabala

Katika makala haya, ninaangazia mkabala wa Mzee Sheikh Nabhany wa 'ufufuaji wa msamiati chakavu’ na kuurejesha tena katika matumizi ya lugha ya Kiswahili. Makala pia yatautathmini mkabala huu na kutoa maoni iwapo unafaa au haufai.

Tasnifu ya Mzee Sheikh Nabhany inauma kuwili.

Kwanza, anahisi kwamba Kiswahili kinakopa sana msamiati kutoka lugha nyingine (hasa za kigeni) – hata pale ambapo maneno hayo ama tayari yapo katika Kiswahili au lugha za Kibantu zinazokurubiana na Kiswahili.

Pili, mtaalamu huyu anahisi kwamba mkondo wa ukopaji kiholela unafanya Kiswahili kipoteze upekee wake.

Kwa hivyo, anapendekeza kwamba upanuzi wa leksikoni ukuzwe 'mumo kwa mumo’ katika kuegemea kanzi lugha za kiasili kabla ya kukimbilia ukopaji kutoka kwa lugha za kigeni.

Wataalamu wanakisia kwamba asilimia 60 ya msamiati wa Kiswahili ni maneno ya Kibantu; Kiarabu (asilimia 30) na asilimia 10 (msamiati kutoka kwa lugha nyingine).

Katika Kandi ya Kiswahili (2012) Mzee Sheikh Nabhany ameorodhesha takriban maneno 60 ya Kiswahili cha kale na visawe vyake vya Kiarabu na lugha nyingine ambayo yanatumiwa katika Kiswahili sanifu.

Baadhi ya mameno hayo ni: Alfajiri (Kiarabu), Mshekuu (Kiswahili cha kale); Ami (Kiarabu); Bakulu (Kiswahili cha kale), Damu (ngeu), hofu (kicho); jahazi (sambo); kiburu (ndeo), bara (tinene), asali (uki), picha (uyoo); jabali (mwamba); mfalme (makame) n.k. Maneno kwenye mabano ni ya Kiswahili cha kale.

Anachopendekeza Mzee Sheikh Nabhany ni kwamba Kiswahili kisikubali ukopaji wa maneno ambayo tayari yamo katika utamaduni wa Waswahili au lugha nyingine za Kibantu ambazo zinakurubiana mno na Kiswahili.

Ukopaji

Swali tunalofaa kujiuliza ni hili; Je, ukopaji wa aina hii ni wa pekee katika Kiswahili?

Tathmini inaonesha kwamba Kiingereza – ambayo ni mojawapo ya Lingua Franca maarufu ulimwenguni ina visawe vingi vya maneno yaliyokopwa kutoka kwa lugha nyingine ulimwenguni.

Kiingereza kwa hakika ndiyo lugha yenye idadi kubwa ya visawe kuliko lugha nyingine yoyoye ile ulimwenguni.

Kwa hivyo, mbali na kwamba mkabala wa Mzee Sheikh Nabhany kuhusu uendelezaji wa leksikoni ya Kiswahili unakubalika kinadharia, hauna mashiko kiutekelezaji.

Kwa nini? Kwa sababu lugha daima zinabadilika kila uchao kutokana na mitagusano ya tamaduni.

Hali kadhalika, dhana ya 'visawe’ katika lugha mara nyingi haipo kwa sababu msamiati fulani hufumbata dhana fulani vizuri zaidi kuliko nyingine.

Hata hivyo, michango na maoni ya watu binafsi na vyombo vya habari kuhusu kuendeleza leksikoni ya Kiswahili haipaswi kupingwa bali kuungwa mkono pale inapochangia kukiendeleza Kiswahili.

 

 

Kuua lugha asili ni sawa na kuteketeza maktaba

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, March 24  2016 at  14:07

Kwa Muhtasari

LUGHA na utamaduni ni mambo yanayokurubiana. Lugha ni kibebeo cha utamaduni mbali na kuwa chombo kinachosheheni fikra, imani na matamanio ya watu.

 

Lugha na utamaduni ni mambo yanayokurubiana. Lugha ni kibebeo cha utamaduni mbali na kuwa chombo kinachosheheni fikra, imani na matamanio ya watu.


Kwa sababu hiyo, juhudi za kimakusudi zinapaswa kufanywa kuihifadhi kwa kuhimiza matumizi ya lugha hizo.

Ingawa kumekuwapo na malalamishi kwamba uhuru wa vyombo vya habari miaka ya tisini – ambao ulichangia mlipuko wa vituo vya Redio za FM vinavyotangaza kwa lugha za kiasili 'umechochea ukabila’, sikosei kudai kwamba kuna manufaa tumbi nzima ya hali hii.


Lugha zetu asili zimepata fursa ya kuhuishwa. Hata hivyo, licha ya lugha asili kupata nafasi ya kutumiwa katika vyombo vya habari, bado kuna baadhi yazo ambazo zinakabiliwa na hatari ya kuangamia na kutoweka ulimwenguni.


Je, chanzo cha 'vifo’ vya lugha ni kipi? Tatizo kuhusu tishio la kufa kwa lugha limekwisha kutambuliwa ulimwenguni kote. Takriban nusu ya ndimi au lugha 6,000 (asilimia 50) zinazokisiwa kuzungumzwa ulimwenguni huenda zikatoweka.

Wataalamu wa masuala ya 'vifo’ vya lugha wamedai kwamba lugha hizo zinazungumzwa na watu wazima ambao hawafundishi kizazi chipukizi lugha hizo.


Isitoshe, asilimia arobaini (40) zaidi ya lugha hizo huenda zikatoweka kwa sababu idadi ya watoto wanaojifunza lugha hizo inapungua kila uchao. Hii ina maana kwamba asilimia 90 ya lugha zinazozungumzwa duniani kwa sasa huenda zikatoweka au zikaangamia katika karne ijayo.


Nchini Kenya, ambapo tuna zaidi ya lugha 45 – sawa na mataifa mengine duniani, hatujasazwa na tatizo hili la kufa kwa lugha za kiasili.

Kwa muda mrefu, Kenya imekuwa ikitumia Kiingereza kuwa lugha rasmi na Kiswahili kuwa lugha ya taifa hadi mwaka 2010 ambapo Katiba ilikikweza hadhi Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kwanza sambamba na Kiingereza.

Tishio la 'kufa'
Baadhi ya lugha zinazokabiliwa na tishio la 'kufa’ nchini Kenya ni pamoja na El-Molo au Ndorobo, Fura au Dehes, Seng’wer, Yaaku, Waata au Boni, Terik, Burji, Dahalo au Bong’omeek, Suba na Sagall.

Lugha ya Olusuba (Suba) kwa mfano inafifia kwa sababu ya kukandamizwa kiisimu na Dholuo. Utangamano na mitagusano kati ya Waluo na Abasuba imesababisha Dholuo 'kumeza’ Kisuba.


Hali ya vifo vya lugha nchini Kenya imechangiwa zaidi na ukosefu wa juhudi za kimakusudi katika kuzitafitia lugha za kiasili, na kuziandikia vitabu.

Hatua za dharura zisipochukuliwa, wazungumzaji wachache wanaozifahamu lugha hizo huenda wakafariki bila maarifa yao kuhifadhiwa kwa njia ya maandishi au njia nyingine murua.


Waandishi na wasomi wakiwemo Ngugi wa Thiong’o, Grace Ogot, Okoth Okombo, Kennedy Momanyi Bosire na Gladys Kwamboka Machogu walikwisha kufanya juhudi za kuziandikia lugha za asili za makabila yao – ingawa juhudi zao hazijafanikiwa sana.

Bw Kennedy Momanyi Bosire na Bi Gladys Kwamboka kwa mfano wamekwisha kuandika na kuchapisha kamusi ya Ekegusii (Endabaro Endasaba Y’Ekegusii). Profesa Ngugi wa Thiong’o na marehemu Grace Ogot wamekwishatoa mchango wao kwa kuandika kazi za fasihi kwa lugha za Kikikuyu na Dholuo mtawalia.

Neema ya Redio
Nilivyotaja mwanzoni mwa makala haya, mlipuko wa vituo vya Redio za FM ulioshuhudiwa nchini Kenya mapema miaka ya 2000 unapaswa kuchukuliwa kuwa neema badala ya balaa. Juhudi za watu binafsi katika kuzitetea lugha asili hazipaswi kupingwa bali kuungwa mkono.


Halikadhalika, Kenya inahitaji kuimarisha sera yake ya lugha ili kukabiliana na wimbi lenye dhoruba kazi la 'vifo’ vya lugha.

Kuna hasara gani lugha 'inapokufa’? Lugha ifapo, huwa ni kana kwamba maktaba nzima ya jamii imeteketezwa. Kuna maarifa yanayofumbatwa na lugha zetu za asili- ambayo hayawezi kamwe kuelezwa kwa lugha nyingine yoyote ile.


Sura ya Pili, Kifungu cha 7, Ibara (3) ya Katiba ya Kenya inasema: Serikali (a) Itakuza na kulinda lugha tofauti za wananchi wa Kenya; na (b) Italinda na itastawisha matumizi ya lugha za kiasili, Lugha Ishara ya Kenya, Breli na njia nyingine za mawasiliano na teknolojia zinazoweza kufikiwa na watu wenye ulemavu.

Tamko hili linapaswa kuwa kichocheo cha kuzithamini lugha zote asili nchini Kenya.

 

 

Ipo haja ya dharura ya kukisanifisha upya Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, March 10  2016 at  15:43

Kwa Muhtasari

Mtaalamu Abdalla Khalid katika The Liberation of Swahili from European Appropriation anahisi kwamba uteuzi wa Kiunguja ulikuwa ni njama ya chini kwa chini iliyoendelezwa na Wazungu ili kuendeleza utumwa.

 

KABLA ya mataifa ya Afrika ya Mashariki kujipatia uhuru, palizuka haja ya kusanifishwa kwa Kiswahili mnamo 1930.

Usanifishaji kimsingi ni utaratibu wa kuondoa tofauti zote zisababishwazo na wingi wa lahaja, maeneo, matabaka kwenye maandishi au othografia, msamiati, matamshi na sarufi.

Mtaalamu Ireri Mbaabu anasema kwamba usanifishaji wa Othografia unanuiwa kupata mtindo mmoja wa kuendeleza kila neno katika lugha kulingana na matamshi.

Wataalamu wa Kiswahili wameanza kutilia shaka kuwapo kwa Kiswahili sanifu. Je, nchini Kenya watu huzungumza Kiswahili au 'Viswahili?’.

Mtaalamu Dkt Ayub Mukhwana wa Chuo Kikuu cha Nairobi aliwahi kuuliza miaka ya 1990; Kiswahili sanifu, Je kipo? Swali la Dkt Mukhwana labda lilichochewa na mabadiliko mengi kwenye nyanja na taaluma mbalimbali yanayojiri katika jamii ya sasa ambayo Kiswahili hakina budi kuyakidhi. Ni kwa nini Kiswahili kilisanifishwa?

Kwanza, kulikuwapo na lahaja nyingi za Kiswahili – na hali hii ilitatiza mawasiliano katika nyanja za dini, elimu na shughuli za utawala.

Kwa hivyo, ili kufanikisha mawasiliano katika nyanja hizo, nchi za Afrika ya Mashariki zilianzisha Kamati ya Kiswahili ya Afrika ya Mashariki mnamo 1930. Kamati hii ilitwikwa jukumu la kukisanifisha Kiswahili.

Kamati hii iliteua lahaja ya Kiunguja kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili kwa sababu mbalimbali.

Kwanza, lahaja hii ilikuwa imesambaa mno kuliko Kimvita ambacho kilikuwa pia kinawania nafasi hiyo.

Pili, asemavyo Ireri Mbaabu katika Historia ya Usanifishaji wa Kiswahili ni kwamba, Kiunguja kilikuwa rahisi kufahamika kuliko Kimvita kwa kuwa matamshi yake hayakuwatatanisha wasemaji wengi.

Tatu, Kiunguja kilikuwa kimekwisha kufanyiwa utafiti mwingi na wataalamu kama vile kina Askofu Edward Steere, mbali na kutumiwa kwa marefu na mapana katika mahubiri na uandishi wa vitabu.

Mwisho, Kiunguja kilikuwa lugha ya biashara na vilevile lugha ya kisiwa cha Zanzibar – ambacho wakati huo kilikuwa kitovu cha Biashara Afrika ya Mashariki.

Mtaalamu Abdalla Khalid katika The Liberation of Swahili from European Appropriation anahisi kwamba uteuzi wa Kiunguja ulikuwa ni njama ya chini kwa chini iliyoendelezwa na Wazungu ili kuendeleza utumwa.

Kimvita kilistahili

Anadai kwamba Kimvita ndicho kilichostahili kuteuliwa kwa kuwa lahaja hiyo ni rahisi kueleweka kuliko lahaja nyingine na vilevile kuwa ni lahaja yenye historia ndefu ya maandishi ya fasihi inapolinganishwa na lahaja nyingine.

Khalid anadai kuwa Kiunguja ni lahaja ya 'kijingajinga’ iliyochafuliwa na Kiarabu. Kwa sababu hiyo, Khalid anapendekeza Kiswahili kisanifishwe upya kwa kutumia Kimvita kama lahaja ya Kimsingi.

Hisia za kupinga Kiswahili sanifu zimewahi kuibuka hata miaka ya hivi karibuni. Katika kongamano la wadau wa elimu jijini Mombasa miaka michache iliyopita, Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa alipendekeza kwamba kila mojawapo wa lahaja zaidi ya 16 za Kiswahili itahiniwe kivyake katika mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).

Hata hivyo, mbali na kwamba mwengo wa usanifishaji upya wa Kiswahili unazibiwa masikio, ukweli uliopo ni kwamba kuna 'Viswahili’ vingi vinavyotofautiana katika matamshi, maendelezo sarufi na hata msamiati.

Mkabala huu unapaswa kuwaziwa upya na wataalamu wa Kiswahili nchini Kenya – hasa ikifahamika kwamba Kenya hadi leo haina chombo cha kiserikali kinachoweza kutwikwa shughuli za uratibu wa maendeleo ya Kiswahili.

Shughuli hii imeparaganywa na watu binafsi – wengine wanaojitafutia makuu. Hata hivyo, juhudi hizo haziwezi kupingwa bali kuungwa mkono.

Mchakato wa usanifishaji wa lugha hauwezi kufanywa mara moja na kukamilika – bali unapaswa kuendelezwa kadri Kiswahili kinavyoendelea kukua na kupanuka kila uchao.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka na mtunzi wa kazi nyingi za kifasihi.

mwagechure@gmail.com

 

 

Udhanaishi katika riwaya na tungo za Kezilahabi

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, February 4  2016 at  19:36

Kwa Muhtasari

Udhanaishi ni falsafa ambayo inamulika kwa kina masuala ya maudhui ya kifo, uhuru wa mtu binafsi, wajibu wa binadamu duniani, ubinafsi, kukata tamaa, udhaifu wa binadamu, furaha, ukengeushi na kuwepo au kutokuwepo kwa Mungu.

 

WAHAKIKI wa fasihi ya Kiswahili wamekwisha kukubaliana kwamba mwandishi Euphrase Kezilahabi ni mtunzi anayeegemeza tungo zake katika nadharia ya udhanaishi (existentialism).

Tatizo la maisha ya mwanadamu (existence) linaonekana kumshughulisha Kezilahabi katika takriban tungo zake zote – mathalan Kichomi na Dhifa (ushairi), Rosa Mistika, Kichwamaji, Dunia Uwanja wa Fujo, Nagona na Mzingile (riwaya).

Euphrase Kezilahabi labda ndiye mtunzi wa kazi za kubuni kwa Kiswahili ambaye amezungumzwa sana na wahakiki wa fani hizi katika karne hii.

Mwandishi huyu alizaliwa katika kijiji cha Ukerewe – Tanzania mwaka 1943.
Alielimishwa katika seminari ya kikatoliki ya Nyegezi, ambako alijifunza falsafa za kidhanifu za dini, lugha ya Kilatini na masomo mengine ya Kawaida.

Mtaalamu Mugyabuso Mulinzi Mulokozi anadai kwamba, baada ya kidato cha sita, Kezilahabi ambaye sasa ni profesa wa fasihi ya Kiswahili alitimuliwa katika seminari kwa sababu walimu wake walifikiri hakuwa na ‘wito’ wa kutosha kwa kazi ya upadre. Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo alisomea ualimu, lugha na fasihi.

Onesha

Tathmini ya jicho kali ya tungo za Euphrase Kezilahabi inaonesha kwamba kazi zake zinaweza kuwekwa katika awamu mbili pana. Awamu ya kwanza inajumuisha kazi alizozitunga miaka ya sabini – Rosa Mistika (1971), Kichwamaji (1974), Dunia Uwanja wa Fujo (1975) na Gamba la Nyoka (1979). Awamu ya pili inahusisha tungo zake za miaka ya tisini – Nagona (1990) na Mzingile (1991).

Katika tungo zake zote – hasa riwaya, Kezilahabi hulitazama suala la maisha katika viwango viwili. Kiwango cha kwanza ni cha mtu binafsi – ilihali cha pili ni kile cha mtu huyohuyo katika jamii pana. Mtunzi huyu chambilecho Mulokozi humchukua mtu binafsi katika hatua zote za maisha yake: uzazi na ujana, malezi, ndoa, uzee na hatimaye kifo.

Hadithi ya Kichwamaji inasimuliwa pakubwa na Deusdedit Kazimoto bin Mafuru ambaye ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Anatuhadithia kisa hiki anapokuwa likizo ya miezi mitatu nyumbani kwao Ukerewe.

Hadithi hii inahusu uhasama kati ya Kazimoto na Manase Kabenga.

Uhasama

Uhasama huo unasababishwa na hatua ya Manase kumpachika mimba Rukia, dada yake Manase. Licha ya uadui baina ya wahusika hao wawili, mambo yanageuka kuwa kinyume. Kazimoto hatimye anamuoa Sabina.

Manase na Kazimoto wanajipata katika njia panda kwa sababu ya kuambukizwa maradhi ya zinaa ambayo matokeo yake ni kuwa, watoto wanaozaliwa wana vichwa vikubwa – yaani vichwamaji. Mwishowe, Kazimoto anajiua na hatua hiyo inazua hisia mbalimbali katika jamii.

Mtazamo

Vyombo vya habari vinawasilisha tanzia hiyo katika maoni na mitazamo tofauti – Uonaji wa mambo kwa mtazamo wa Kimagharibi na ‘Naizi Kachoka na Maisha’.

Aidha, kuna gazeti moja lililomtazama Kazimoto kama kiwakilishi cha bara la Afrika na kuandika kichwa cha habari chenye anwani, ‘Kutokuwa kwa Afrika katika ujadiliano’.

Udhanaishi ni falsafa ambayo inamulika kwa kina masuala ya maudhui ya kifo, uhuru wa mtu binafsi, wajibu wa binadamu duniani, ubinafsi, kukata tamaa, udhaifu wa binadamu, furaha, ukengeushi na kuwepo au kutokuwepo kwa Mungu.

Kazimoto kwa mfano haamini kwamba Mungu yupo. Anazua mjadala huo kwenye kikao cha kunywa pombe alipomtembelea rafiki yake Kamata aliyekuwa katika kijiji cha Sakwa.

Mjadala huo unazua mihemko, hamaki na makasiriko na kutishia kuharibu kikao. Tahakiki ya jicho pevu ya kazi za mwandishi huyu inaonesha bayana jinsi alivyobwia na kuathiriwa na masomo yake ya seminari.

Motifu hiyo inajidhihirisha katika tungo zake zote – huku ikipea mno katika tungo zake za Nagona na Mzingile.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka
mwagechure@gmail.com

 

 

Mbinu za uundaji wa istilahi katika Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, January 7  2016 at  10:38

Kwa Muhtasari

Lugha huundiwa istilahi ili utamaduni wake ukidhi dhana ambazo hapo awali zilikuwa hazimo katika utamaduni huo.

 

LUGHA huundiwa istilahi ili utamaduni wake ukidhi dhana ambazo hapo awali zilikuwa hazimo katika utamaduni huo.

Aidha, maendeleo ya kasi ya sayansi na teknolojia ndiyo kichocheo cha kimsingi katika uundaji wa istilahi – ingawa sicho kiini cha pekee.

Katika makala ya leo, tutajadili mbinu ambazo wanaleksikoni hutumia katika kuunda istilahi za lugha.

Mwandishi Enock Nyariki alitaja baadhi ya mbinu hizo (Taifa Leo, Desemba 30, 2015).

Wanaleksikoni wa Kiswahili kama vile Patricia Mbughuni, Zubeida –Tumbo Masabo, Hermans Mwansoko na John Gongwe Kiango (wote kutoka Tanzania), Mzee Sheikh Ahmad Nabhany, Rocha Mzungu Chimerah na Kyallo Wadi Wamitila (wa Kenya) wametumia mbinu zifuatazo katika kukiundia Kiswahili istilahi na msamiati mpya.

Hizi ni pamoja na takriri au uradidi, upanuzi wa maana, utohozi, tafsiri, ufupishaji, uhulutishaji, uambatanishaji, ubunifu na uingizaji wa maneno ya lahaja ya lugha za Kibantu katika Kiswahili.

Mwandishi Enock Nyariki alitaja mbinu za uradidi na upanuzi wa maana.

Neno 'nyokonyoko’ alivyosema Bw Nyariki limetokana na uradidi wa neno 'nyoko’ ambalo maana yake ni mzazi wa kike au nina.

Katika Kiswahili, kuna misemo ya 'kumanyoko’ na 'kumanina’ ambayo aghalabu ni matusi.

Mzee Jomo Kenyatta alipenda sana kutumia neno 'nyokonyoko’ kwa maana iliyozua fahiwa ya kuwakomesha watu wasilete mchezo au wasithubutu - au kitu kama hicho.

Kuna msamiati kama vile 'kimbelembele’ 'kijingajinga’ na kadhalika ambao umetokana na uradidi.

Katika mbinu ya upanuzi wa maana, maana ya awali ya neno hupanuliwa na kuhusishwa na maana nyingine.

Maana ya kileksika ya neno 'sakata’ kwa mfano: ni kufanya jambo kwa umahiri au hali ya mgogoro au ghasia.

Hata hivyo nchini Kenya, vyombo vya habari vimepanua maana ya neno hili na kulitumia kutajia kashfa kama vile Goldenberg, Anglo-Leasing au hata Eurobond.

Mbinu ya utohozi huhusisha kuyapatia maneno yaliyokopwa kutoka kwa lugha nyingine matamshi na maandishi ya lugha inayokopa.

Kwa mfano 'wakti (Kiarabu) huwa 'wakati’ (Kiswahili); 'Television’ (Kiingereza) huwa 'televisheni’ (Kiswahili) na kadhalika.

Mbinu ya kutafsiri

Katika mbinu ya kutafsiri, neno lililokopwa huelezwa kwa lugha nyingine; kwa mfano. 'secondary school’ huwa 'shule ya upili’.

Katika mbinu ya ufupishaji, wanaleksikoni hutumia akronimu za sehemu ya kwanza ya maneno mawili au zaidi na kuziunganisha ili kupata neno jingine.

Mfano mzuri ni: Upungufu wa Kinga Mwilini (Ukimwi).

Nayo mbinu ya uhulutishaji (hybdidisation) huhusisha uunganishaji wa visehemu mbalimbali vya maneno mawili au zaidi ili kubuni neno moja mahuluti.

Mzee Sheikh Nabhany wa Mombasa amebuni neno 'runinga’ kutokana na maneno Rununu + Maninga.

Katika Kiswahili cha zamani kwa mujibu wa Mzee Nabhany, 'Rununu’ ni sauti inayosikika kutoka mbali’ ilhali 'Maninga’ ni macho.

Aidha wanaleksikoni huambatanisha maneno mawili ili kuunda neno moja.

Kwa mfano 'isimu’ + 'Jamii’ tunapata 'isimujamii’.

Kiswahili na lugha nyingine za Kibantu ni lugha 'ambishibainishi’ (agglutinative language).

Kwa sabababu hiyo, viambishi huweza kupachikwa mwanzoni au mwishoni mwa mizizi ya maneno ili kuunda maneno tofauti.

Kutokana na neno 'utandawazi’ tunaweza kupata maneno kama vile 'tandawazisha’, 'utandawazishaji’ miongoni mwa mengine.

Katika mbinu ya kubuni, wataalamu wa istilahi huangalia sifa za kimaumbile, sifa za kitabia na sifa za kimatumizi ambazo huwaongoza katika kubuni maneno na istilahi mpya.

Mwandishi Enock Nyariki anaonekana kuwa na tatizo na mbinu hii – ingawa sababu alizotoa katika makala yake kutoridhishwa na mbinu hii hazikuwa za kitaalamu.

Mwisho, tuna mbinu ya uingizaji wa maneno ya lugha nyingine za Kiantu katika Kiswahili.

Maneno yafuatayo yemeingizwa katika Kiswahili kutoka kwa lahaja za Kiswahili pamoja na lugha nyingine za Kibantu: 'njeo’ (Kiamu, Kenya), 'ngeli’ (Kihaya, Tanzania), 'kitivo’ (Kipare, Tanzania), 'Bunge’ (Ha, Tanzania), 'githeri’ (Kikuyu, Kenya) na kadhalika.

Mzee Sheikh Ahmad Nabhany ni mmoja wa wataalamu wa Kiswahili wanaounga mkono mbinu hii.

Enock Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

 

 

Matatizo ya uainishaji wa tanzu za kifasihi

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, February 19  2015 at  09:17

Kwa Muhtasari

Makala haya yanalenga kuangalia upande wa pili wa sarafu ambao mwandishi Alex Ngure hakuumulika katika makala yake. Mitazamo na ufafanuzi wa dhana  ‘riwaya’ (Taifa Leo, Februari 16, 2015) labda kwa sababu ya ukosefu wa nafasi. Nitaangazia chanzo cha mtafaruku wenyewe kwa kutumia Nadharia ya Tanzu (Genre Theory) kwa mujibu wa Fowler Alaistair katika kazi yake ya Kinds of Literature (1982).

 

MSUKUMO wa kuandika makala haya unatokana na makala ya Mwalimu Alex Ngure  -  ‘Mitazamo na ufafanuzi wa dhana  ‘riwaya’ (Taifa Leo, Februari 16, 2015). Mwandishi alijaribu kuangazia mtafaruku ulio(kuwe)po baina ya wataalamu katika kutoa fasiri ya ‘riwaya’. Makala yangu yanalenga kuangalia upande wa pili wa sarafu ambao mwandishi hakuumulika kwa sababu ya labda ukosefu wa nafasi. Kwa usemi mwingine, ninalenga kuangazia chanzo cha mtafaruku wenyewe kwa kutumia Nadharia ya Tanzu (Genre Theory) kwa mujibu wa Fowler Alaistair katika kazi yake ya Kinds of Literature (1982). Nadharia ya Tanzu ni utaratibu wa kuainisha fasihi katika misingi ya aina mbalimbali kwa kuegemea miundo na maumbo. Umbo ni sifa za nje zinazoipa kazi ya fasihi sura za kutambilika. Sura hizi ni pamoja na  sura, matendo, maonyesho, vina, mizani n.k. Muundo nao ni jumla ya uhusiano unaokuwepo kati ya vijisehemu mbalimbali vinavyounda kitu kamili au kwa jumla.

Muundo wa tamthilia kwa mfano una maana ya matendo yake pamoja na maonyesho mbalimbali na jinsi visehemu vyote vinavyohusiana kuunda kazi nzima inayoitwa tamthilia. Nadhatia ya tanzu ina misingi yake katika Kipindi cha  Urasmi ambapo fasihi ya Ugiriki na Urumi ilifana. Katika Poetics kwa mfano, Aristotle  anaeleza maana na sifa za tamthilia ya kitanzia. Kwa hiyo, kazi hii ni kiwakilishi cha Nadharia ya Tanzu.  Sifa hizi zinafaa kuwaelekeza na kuwaonesha jinsi kazi za utanzu fulani zinavyopaswa kuwa; urefu, idadi ya matukio ambayo mtazamaji anaweza kuyakumbuka n.k. Kwa hiyo, nadharia ya tanzu katika kipindi cha urasmi ililenga kuwekea  tanzu mipaka. Aidha, tuna nadharia ya tanzu ya kisasa.

Mara nyingi, nadharia ya kipindi hiki ni ya kimaelezo tu. Inaeleza tanzu zilizopo, sifa zao – bila kuziwekea sheria zozote au mipaka yoyote. Inatambua kuwa tanzu za kifasihi zinazotambulika  zinaweza kuchanganywa na vilevile zinaweza kuzaa tanzu mpya (umahuluti wa tanzu). Kwa mfano, tamthilia inaweza kuwa mseto wa tanzia na  futuhi na tukawa na futuhi ya kitanzia – kwa mfano Mkaguzi Mkuu wa Serikali (Nikolai Gogol). Riwaya ya kibarua kwa mfano Barua Ndefu kama Hii (Mariama Ba) imeandikwa katika mtindo wa barua. Waandishi wengine wamechanganya nathari na ushairi – kwa mfano Maisha yangu na Baada ya Miaka Hamsini (S. Robert). Katika kipindi cha urasmi ambacho tumekigusia, jambo hili halingeweza kutokea kamwe kwa sababu kila utanzu ulifuata kanuni fulani. Hakuna mtunzi aliyethubutu  kuchanganya tanzu.

Badala ya kusisitiza upekee wa kila utanzu, nadharia ya  tanzu ya kisasa inaangalia sifa za jumla za kila utanzu, kunga zake na lengo lake kifasihi. Kwa mfano, iwapo ni riwaya, badala ya kusisitiza upekee wa riwaya, itaelezea sifa zake za kimsingi (k.m inatumia usimulizi wa kubuni kimfululizo) na vilevile lengo lake la kijumla – kutoa picha halisi ya maisha katika jamii – hasa riwaya za kiuhalisia. Hata hivyo, nadharia ya tanzu haijasaidia sana katika sana katika kutoa uainishaji thabiti wa tanzi zilizopo. Imeshindwa. Je, ni vipi utambuzi wa aina mbalimbali za tanzu unavyosaidia katika kufasiri tungo za kifasihi? Fowler anasema, thamani kuu ya nadharia ya tanzu haitokani na suala la uainishaji; inatuwezesha tu kueleza jinsi tunavyoweza kuweka kazi fulani katika  tanzu mahususi ili tuweze kuifasiri na kuishughulikia. Kwa hiyo, uainishaji unapaswa kuwa  hatua ya kwanza katika uhakiki. Kwa mfano, Kwaheri Iselamagazi (B. Mapalala) ni riwaya. Ni riwaya ya aina gani? Ni ya kihistoria. Je, riwaya ya kihistoria ina sifa gani? Tukikwisha kujubu maswali haya tunaanza kuihakiki kwa kubainisha ni kwa kiwango gani inatimiza sifa za riwaya za kihistoria.

 Uhakiki wa kiutanzu

 Kuzitalii kazi za fasihi, kuziweka katika makundi ya tanzu na kutathmini ni zipi zinakiuka kanuni za tanzu husika, kwa kiasi gani na kwa sababu gani ni uhakiki wa kiutanzu. Kwa mfano, tunapouangalia utanzu wa riwaya, tunaweza kurejelea kazi ya Edward Morgan Forster, Aspects of The Novel ambapo ameeleza baadhi ya sifa za kimsingi za utanzu wa riwaya. Kwa mfano Forster anasema kwamba riwaya inapaswa kuwa na maneno 120,000 au takriban kurasa 403.  Forster ni Mwingereza kwa hiyo mifano au vigezo anavyotoa ni vya riwaya na kiulaya au Kiuingereza. Riwaya nyingi za Kiafrika hazina urefu huu. Kwa nini? Kwa sababu, kwanza, riwaya za Kiafrika inafanana sana na ngano za fasihi simulizi ambazo si ndefu. Pili utamaduni wa kusoma na kuandika haujakita sana Afrika – na hivyo basi hakujawa na mazoea ya kuandika kazi ndefu. Uhakiki wa kiutanzu unamwezesha mhakiki kutambua mchango wa kila kazi husika katika utanzu husika. Hii ina maana kwamba, kinadharia, kila kazi mpya inayotungwa huchangia utanzu husika kwa njia moja au nyingine. Mchango huu unaweza kuwa katika upande wa fani au maudhui.

Uhakiki wa kiutanzu humwezesha mhakiki kupambanua kazi bora au duni kwa kurejelea kanuni kuu za utanzu unaohusika. Kwa mfano, drama ya kitanzia na sifa zake zinaweza kutumika kutathminia kazi za aina hiyo – na kazi hizo zinapopungukiwa na vigezo vya drama ya kitanzia, inaweza kudaiwa kuwa ni duni. Hata hivyo, tatizo mojawapo linalojitokeza katika uhakiki wa kiutanzu ni kuzuka kwa fasihi mpya inayozua tatizo la istilahi na lugha ya kuielezea. Kazi mpya hutatiza kwa muda katika kutafuta istilahi za kuielezea kitaalamu – hasa inapokuwa imekiuka aina za fasihi zilizopo. Kwa mfano, bado wahakiki wanatatizika katika kuhakiki kazi mbili za Euphrase Kezilahabi – Nagona na Mzingile. Kwa nini? Kwa sababu hazina fani ya riwaya, hazina upana wa masimulizi wala ukuzaji wa wahusika – licha kwamba zina uzito kimaudhui. Je, kazi hizi ni riwaya? Je, ni hadithi fupi? Kwa hiyo, kazi hizi mbili bado zinawakanganya watu wengi kwa sababu ya tofauti yao na utanzu wa riwaya kwa jinsi inavyozoeleka.

Vilevile, Kezilahabi na wanamapinduzi wengine walipotunga mashairi yasiyofuata vina na mizani, ushairi huo huru uliwatatiza wahakiki hasa kuhusiana na jina lake. Je, ni macue? Mashairi ya mtiririko? Masivina? Au ni mashairi huru? Tanzu pia hukua na hatimaye kuchakaa au ‘kufa’ hasa pale ambapo mazingira yanayolea utanzu husika yanapotoweka. Katika fasihi ya Kiswahili, utanzu wa utendi/ tenzi unaweza kudaiwa kwamba ‘umekufa’. Hatuoni watu wengi wakitunga tenzi siku hizi. Hata hivyo, tunachoshuhudia ni usimilishwaji wa baadhi ya hizi tenzi na baadhi ya watunzi kuzisimulia tendi zilezile katika maumbo au tanzu nyingine. Kwa mfano novela ya Bitugi Matundura, Mkasa wa Shujaa Liyongo imesimilisha Utenzi wa Liyongo (Mohamed Kijumwa). Tamthilia ya Kifo  Kisimani ya Kithaka wa Mberia imetokana na utenzi huo – huku riwaya ya Siri Sirini 1,2 & 3 ya Rocha Chimerah imetumia kiunzi cha tenzi za Fumo Liyongo na Mwanakupona.

Msingi huu kuhusu  nadharia ya tanzu na uhakiki wa kiutanzu unatupatia mwanga wa kuweza kuona kitaalamu ni kwa nini wataalamu aliowataja Mwalimu Ngure kwenye makala yake wana mitazamo mbalimbali kuhusu dhana ya ‘riwaya’. Inategemea mkabala na vigezo anavyochukua mtaalamu katika  kufikia kauli zake. Mtaalamu akiegemea vigezo vya Forster kwa mfano katika kuainisha riwaya ya za Shaaban Robert – kuna uwezekano wa kuhitimisha kwamba  tungo kama vile  Kusadikika, Kufikirika  na Adili na Nduguze si riwaya.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

 

 

 

Mawanda ya taaluma ya  isimujamii

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, February 17  2015 at  11:25

Kwa Muhtasari

Isimujamii ni tawi la isimu linalochunguza uhusiano na mtagusano au mwingiliano baina ya lugha na jamii, matumizi ya lugha hiyo pamoja na miundo na mikondo ambayo kwayo watumizi wa lugha hiyo huishi. Kwa hivyo inahusu eneo la kijeografia, umri wa matumizi na jinsia, matabaka za watumizi wa lugha.

 

MOJAWAPO wa masomo yanayofundishwa katika Kiswahili  kwenye ngazi ya shule za upili na vyuo vikuu ni isimujamii. Isimujamii ni tawi la isimu linalochunguza uhusiano na mtagusano au mwingiliano baina ya lugha na jamii, matumizi ya lugha hiyo pamoja na miundo na mikondo ambayo kwayo watumizi wa lugha hiyo huishi. Lugha ni nyenzo muhimu sana katika mawasiliano na ni chombo kinachosheheni fikra, maarifa, utamaduni na mbeko za binadamu. Mumo kwa mumo katika lugha ya binadamu mna utamaduni wake.

Utamaduni unafumbata maisha ya mtu na jinsi anavyoyaishi. Inapotokea kwamba watu wananyimwa lugha yao, huwa kwa hakika ni kana kwamba watu hao huwa wameachwa uchi. Lugha hivyo basi hutumiwa kwa mitindo tofauti, mahali tofauti kama vile mahakamani, kwenye vyombo vya habari, misikitini na makanisani  -au maeneo ya maabadi, sokoni na kadhalika. Lakini ikumbukwe kwamba, lengo la matumizi ya lugha – licha ya kutumika katika mazingira na miktadha tofauti huwa ni kuwasiliana.

Lugha pia inaweza kutumika kwa namna ambayo inatinga mawasiliano. Kwa hivyo ni bayana kwamba  hapana njia moja mahususi ya kutumia lugha. Mtu mmoja hutumia lugha kwa mtindo wa pekee anapolinganishwa na mtu mwingine, lugha hutumika kama chombo cha kijitambulisha katika ngazi za ukabila, taifa na maeneo ya kijiografia. Lugha kwa upande mwingine ina uwezo wa kuwaunganisha watu au hata kuwatenganisha kabisa. Lugha vipindi za Sheng na Engsh kwa mfano ni kitambulisho kikubwa sana miongoni mwa vijana nchini Kenya.

Kiswahili  sanifu kwa upande mwingine ni lugha ambayo inaaminika kuwa na uwezo wa kuleta umoja na mshikamano miongoni mwa taifa la Kenya lenye zaidi ya ndimi 42. Tanzania ambayo ina makabila zaidi ya 100 imefanikiwa kuibua mshikamano na utaifa wa namna fulani.Si mara zote ambapo nchi yenye lugha moja inaleta mshikamano wa taifa. Nchi ya Somalia ina lugha moja tu – Kisomali. Hata hivyo, nchi hiyo haijakuwa na utaifa wowote kwa zaidi ya miongo miwili. Hii ina maana gani? Ina maana kwamba mumo kwa mumo katika taifa moja, kuna makundi yanayopigania maslahi mbalimbali ambayo huzua mikinzano na tofauti ambazo haziwezi kusuluhishwa kwa urahisi kwa matumizi ya lugha. Mara nyingi mikinzano hii huwa ni ya siasa, uchumi na jamii.

Maswali

 Kwa hiyo, isimujamii ni taaluma ambayo huuliza maswali yafuatayo ya kimsingi: Je, eneo fulani kijiografia (wilaya, mkoa, nchi au bara) lina lugha ngapi na lugha hizo ni zipi? Je, watu wa umri  na jinsia tofauri hutumia lugha kwa  njia sawa au kuna tofauti. Je, lugha katika nchi au eneo fulani zimepangiwa vupi? Kuna zile zilizoteuliwa na kuendelezwa au kustawishwa kimakusudi? Je, lugha zilizopo zinaimarika au zinafifia au kufa? Je, kuna taasisi maalumu za serikali zinazojishughulisha na shughuli za ustawishaji wa lugha? Je, lahaja husababishwa na nini? Je, kuna mpaka upi baina ya lugha na lahaja?

Haya na mengine mengi ni maswali ya kimsingi ambayo mtaalamu wa isimujamii hujiuliza. Baadhi ya majibu ya  maswali haya humwelekeza  mtaalamu wa isimujamii kwenye ukweli kwamba, katika uhalisia wa mambo, lugha husawiri matabaka katika jamii, mitindo ya lugha hudhibitiwa na mahitaji ya jamii, lugha ndiyo kibebeo cha mitazamo na falsafa za jamii, kuna misimbo mbalimbali katika matumizi ya lugha katika jamii na hata  mabadiliko katika jamii hushurutisha lugha kubadilika pia.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuka

mwagechure@gmail.com

 

 

 

Mwandishi alipotosha wasomaji kuhusu matbaa

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Friday, January 30  2015 at  18:13

Kwa Muhtasari

Nilivunjika moyo baada ya kukamilisha kusoma makala ya Alex Ngure na kugundua kwamba ilikuwa inapwaya na kwa maoni yangu kuonekana chapwa. Mwandishi alipotosha wasomaji kwa kuwasilisha fahiwa kwamba ‘matbaa’ ni sawa na kampuni ya uchapishaji.

 

NILISOMA makala ya mwalimu Alex Ngure ‘Umuhimu wa hisi na ubunifu katika uandishi’ (Taifa Leo, Januari 29, 2015 kwa jicho kali sana kwa sababu  nimekuwa katika taaluma hii kwa  takriban zaidi ya mwongo mmoja sasa. Kwa hiyo, nilitarajia kwamba mwandishi  (ambaye pia ni mtunzi wa kazi za fani hizi) angefumbata kwa uketo mawazo na taswira murua inayoweza kuwapa mwongozo maridhawa waandishi chipukizi ambao daima wanatapatapa katika kujaribu kupata dira ya kutunga kazi zinazoweza kuchapishika.

Hata hivyo, nilivunjika moyo baada ya kukamilisha kusoma makala hayo na kugundua kwamba ilikuwa inapwaya na kwa maoni yangu kuonekana chapwa. Kwa usemi mwingine, makala yake iliishia kusomeka kwa toni ya ‘bora makala’ na ‘si makala bora’.

Nitatoa sababu zifuatazo. Kwanza, mwandishi alipotosha wasomaji kwa kuwasilisha fahiwa kwamba ‘matbaa’ ni sawa na kampuni ya uchapishaji. Hii si kweli hata kidogo. Msamiati ‘matbaa’ aghalabu umekuwa ukitumika vibaya na baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya waandishi kama Bw Ngure. Maana sahihi ya ‘matbaa’ ni  mitambo au mashine  ya kupiga chapa.  Kwa hiyo, haiyumkiniki dhana ‘matbaa’ ikawa kisawe cha kampuni ya uchapishaji.

Nchini Kenya, kampuni ya uchapishaji ambayo ina matbaa yake ni Kenya Literature Bureau (KLB) ambayo ni shirika la Serikali. Kwa sababu hiyo, kitabu ambacho kimechapishwa na  KLB kitaandikwa katika mojawapo ya sehemu za  matini kwenye ukurasa tangulizi: ‘Kimetayarishwa na kupigwa chapa na Kenya Literature Bureau. Aidha kampuni ya Nation Media Group pia ina matbaa yake. Kwa hiyo, katika ukurasa wa nyuma wa Taifa Leo, huandikwa taarifa hizi :  “Hutayarishwa katika Nation Centre, Kimathi Street, na kuchapishwa  Mombasa Road, Nairobi na kampuni ya Nation Media Group.” Aidha, kampuni nyingi za uchapishaji hazina matbaa zao binafsi. Phoenix Publishers Ltd kwa mfano  hutumia matbaa kama vile Kenya Litho, Ramco Printing Works, Printpak Ltd na kadhalika kupiga chapa vitabu vyao.

Vigezo

Pili, si kweli kwamba wachapishaji wengi  chambacho Bw Ngure  hawaweki wazi vigezo na viwango  wanavyovitaka wenyewe. Katika enzi hii ya dijitali, kampuni nyingi za uchapishaji zina nyavuti (websites) ambapo hubainisha vigezo ambavyo mwandishi chipukizi au yule aliyekomaa anapaswa kufuata katika kuwasilisha mswada. Maelezo haya aghalabu huwa ni maagizo ya kimsingi yanayoweza kuwa dira kwa mwandishi. Kwa hiyo nafikiri watunzi hasa chipukizi wanaoandika kwa papara huenda wasiwe na habari kuwa kuna tovuti za aina hiyo.

Tatu, akimnukuu S.A. Mohamed, Bw Ngure alidai kwamba  ‘mwaandishi aandikapo  huanza yeye mwenyewe  kufumwa na hisi fulani ambazo hujaribu kuzitoa na kuziwasilisha  kwa njia ya maandishi kwa  hadhira yake’. Ingawa ninakubaliana kwa kiasi fulani na rai hii, sikubaliani nayo pia kwa kiasi fulani. Nilimtarajia Bw Ngure kupanua mawanda ya rai hii ya hisi kwa labda kumulika aina za hisi au misukumo ambayo inaweza kuwaongoza watunzi katika kuchukua kalamu ili kutunga kazi za kifasihi.

Ingawa waandishi wenye vipawa huongozwa na hisi za kutunga ili kujiliwaza, pana pia watunzi wengine wanaotunga kwa sababu ya hisi za kujipatia hela. Waandishi wanaoongozwa na hisi za kujipatia hela mara nyingi huishia kuwa waandishi wa ‘masafa mafupi’. Vipi? Kazi za sanaa  zinazotokana na mkabala wa aina hii huishia kuwa chapwa – na nafikiri watunzi wengi wa fasihi ya Kiswahili nchini Kenya wamo katika pote hili.

Bitugi Matundura, mfasiri wa tungo za Barbara Kimenye za Moses series ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

 

 

Mazrui awataka wataalamu waunde msamiati unaofaa karne ya 21

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, January 29  2015 at  15:08

Kwa Muhtasari

Prof Alamin Mazrui anatoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kujifungata masombo kuunda msamiati na istilahi za Kiswahili ambazo zitatufaa zaidi katika Karne ya 21.

 

MNAMO 2010, nilihudhuria kongamano la kimataifa la Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kaunti ya Kilifi.

Kikao hicho kilichowaleta pamoja wasomi, wakereketwa na  maashiki wa Kiswahili kutoka pembe mbalimbali za ulimwengu kiliandaliwa na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Pwani. Mada kuu ya kongamano hilo ilikuwa ni  tafsiri na ukalimani.

Miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Prof Alamin Mazrui  (Chuo Kikuu cha Rutgers), Prof Mohamed Hassan Abdulaziz (Chuo Kikuu cha Nairobi ), Prof Rocha Mzungu Chimerah,  ambaye alikuwa mwenyeji wa kongamano hilo na Prof Kimani Njogu.

Nilikuwa makini sana kusikiza mijadala ya wasomi hao kwa sababu mbili. Kwanza, baadhi yao, kwa mfano Prof Abdulaziz  walikuwa walimu wangu katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Inakuwa ni tajriba nzuri wakati ambapo mtu anapokutana na  walimu wake kwenye vikao kama hivyo.

Pili, hiki ni kizazi cha wasomi ambacho kimetoa mchango mkubwa  na kuacha taathira mno katika taaluma ya Kiswahili. Wataalamu wengi wamepitia katika mikono yao.

Prof Alamin Mazrui ndiye aliyetwikwa heshima ya kutoa hotuba ya kuchochea mjadala kuhusu mada ya kongamano hilo. Alitoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kujifungata masombo kuunda msamiati na istilahi za Kiswahili ambazo zitatufaa zaidi katika Karne ya 21.

Alisema, kulikuwepo na haja ya kufanywa  juhudi za kimakusudi kusayansisha lugha za Kiafrika ili ziweze kukidhi maendeleo ya kasi yanayojiri ulimwenguni kila uchao.

Alikariri kwamba ubunifu wa kisanaa na sayansi unapaswa kupewa uzito sawa kwa sababu unatokana na kipawa kilekile kimoja. Alitahadharisha dhidi ya  ukasuku wa kukopa istilahi kutoka kwenye lugha za kigeni kupita mipaka kwa sababu kufanya hivyo kunachangia katika kusambaa kwa aina mpya ya ubeberu.

Prof Mazrui hali kadhalika alionya kwamba ipo hatari ya kutafsiri tu maandishi yanayotoka uzunguni.

Alipendekeza kuwa wataalamu wanapaswa kuwazia kutafsiri matini za Uarabuni, Uchina – kama vile kazi za Confucius na pia tungo za mwandishi kama vile Gabriel Garcia Marquez wa Colombia.

Naye Prof Mohamed Hassan Abdulaziz  aliukweza mjadala na kuuingiza katika viwango vya juu kabisa alipotoa changamoto kwamba, mataifa ya bara Afrika hayawezi kupiga hatua kubwa katika maendeleo kwa kutegemea lugha za kigeni tu.

Alitoa mifano ya mataifa ya Japan, Korea na Uchina ambayo yamepiga hatua kubwa sana katika mwana wa sayansi na teknolojia bila kuegemea lugha za kigeni. Abdulaziz aliushutumu mfumo wetu wa elimu unaopendelea watu wachache tu ambao ni wasomi teule.

Kupuuza lugha za kiasili

Alilalamika kuhusu hali ambapo licha ya  alisimia  90 ya uchumi wetu kuendeshwa kwa kutumia lugha za kiasili hususan Kiswahili na asilimia 10 pekee ikiendeshwa kwa  kutumia lugha za kigeni, lugha za asili zingali zinapuuzwa na kuonewa aibu.

Alisema, bila kutumia lugha zetu asili, 'uchumi utasalia tu kwenye mabenki’.

Alitahadharisha pia kwamba tafsiri za istilahi zinaweza kufanywa alini tukakosa mahali pa kuzitumia.

Alisema, huku lugha ya Kiingereza ikiwa ni lugha itumiayo sana muundo wa unominishaji – na lugha za Kibantu zikiwa zinaegemea sana vitenzi, pana changamoto au ndaro kubwa kwa wanataaluma wa Kiswahili kuibuka na mbinu murua za kiisimu zinazoweza kutumiwa kubuni istilahi au maneno zalishi.

Alitoa mfano wa istilahi infrastructure  - ambayo kwa Kiswahili ni amara, muundomsingi au muundombinu. Infrared itaitwaje kwa Kiswahili?” Akauliza Prof Abdulaziz.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

 

 

Kiswahili na maazimio ya hadi mwaka 2030

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Saturday, January 24  2015 at  12:18

Kwa Muhtasari

Lugha ni mojawapo wa raslimali kubwa ambayo inaweza kutumiwa na jamii yoyote ile iwayo katika kutekeleza na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

 

LUGHA ni mojawapo wa raslimali kubwa ambayo inaweza kutumiwa na jamii yoyote ile iwayo katika kutekeleza na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Lugha  ndiyo chanzo cha maisha na mamlaka aliyo nayo mwanadamu.

Kutokana na ukweli huu, lugha ndio wenzo na ufunguo wa maendeleo ya jamii na chombo madhubuti kinachoweza kutumiwa kuiwezesha Kenya kuafikia  Rajua yake ya 2030.

Iwapo raia watajihusisha kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa katika nyanja zinazopewa kipaumbele kwenye maazimio husika ya maendeleo kufikia 2030 – hususan  kilimo, maendeleo ya viwanda, biashara, utalii na sekta nyingine za fedha hasa benki, watahitajika kupata maarifa na ujuzi.

Kwa bahati mbaya, maarifa haya hayamo katika lugha zinazozungumzwa na  idadi kubwa ya Wakenya. 

Hali hii inatulazimu sisi wasomi kusaka na kuonesha kiungo kilichoko baina ya lugha na maendeleo hasa kuhusiana na Rajua ya Kenya ya kupiga hatua kubwa katika maendeleo kufikia 2030.

Ni bayana kwamba Kiswahili na Kiingereza  ndizo lugha zinazotumiwa kwa mapana katika maisha ya Wakenya ya kila siku.

Hata hivyo, raia wengi huelewa Kiswahili zaidi kuliko Kiingereza.

Kwa hivyo, tunatarajia kwamba lugha  itakayofanikisha mawasiliano ya raia na wanavijiji katika  ngazi za Taifa na utawala ujao wa kaunti itakuwa ni Kiswahili.

Maafisa na wafanyakazi  wa serikali katika ngazi hizo wana uhuru wa kutumia lugha zao za asilia – lakini kuendesha shughuli za maendeleo katika ngazi hizo kwa Kiswahili  kutaleta natija kubwa sana.

Kiswahili kimekwezwa hadhi sawa na Kiingereza

Kwa hivyo, tunatarajia kwamba mifumo ya utawala wa kaunti itakapoanza kutekelezwa, Serikali itahakikisha kwamba Mipango ya Maendeleo inapatikana katika lugha hizi mbili; yaani Kiswahili na Kiingereza.

Kwa kuwa Kiswahili kimekwisha kwezwa hadhi na kuwa lugha rasmi sambamba na Kiingereza, uamuzi huu wa kisera unamaanisha kwamba nyaraka na stakabadhi zote za Serikali  zenye taarifa kuhusu ukuaji wa uchumi zitahitajika kuwa katika lugha hizo – Kiswahili na Kiingereza.

Stakabadhi ambazo kwa sasa zinapatikana katika Kiingereza zitahijajika kutafsiriwa kwa Kiswahili.

Kadhalika, Serikali itahitajika kuhakikisha kwamba huduma za nyanjani na vifaa – hasa stakabadhi za kutoa mafunzo hayo kwa umma zinaandikwa kwa Kiswahili na katika lugha nyingine za asili.

Vilevile, Serikali itahitajika kuwasilisha kwa Kiswahili mafunzo kwa umma kuhusu mikakati na mbinu za maendeleo katika lugha wanayoielewa na kuifahamu kwa urahisi – ambayo ni Kiswahili.

Kitatumiwa kuboresha utendakazi

Watumishi wa umma watakuwa na haki; kulingana na majukumu wanayoyatekeleza kutumia Kiswahili au Kiingereza katika kufanikisha utendakazi wao.

Ili kuhakikisha kwamba raia wanashiriki kikamilifu katika maendeleo, serikali italazimika kuanzisha vitengo vya Kiswahili katika ngazi za kaunti na taifa.

Mitazamo hii inatuchochea kuanza kuona Kiswahili kama raslimali inayoweza kutumiwa kufanikisha ajenda za maendeleo ya taifa hili.

Mataifa mengi yaliyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya viwanda kama vile Uchina, Japani na hata Malaysia hayategemei pakubwa sana matumizi ya lugha za kigeni katika kusukuma gurudumu la maendeleo yao.

Sekta ya juakali nchini Kenya kwa mfano ina watu wanaounda magari na vifaa vingine ingawa hawajui Kiingereza.

Je, lugha inayotumiwa katika harakati za kukarabati magari kwa mfano ni ipi? Bila shaka ni Kiswahili.

Kwa hivyo, ipo haja ya dharura ya Kenya kuanza kutafakari upya kuhusu nafasi ya lugha – hasa Kiswahili katika kufanikisha Rajua yake ya 2030.

Bila kutilia maanani suala la lugha, huenda ufanisi wa haja usiwahi kupatikana.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu  cha Chuka

mwagechure@gmail.com

 

 

Kenya yahitaji asasi ya kudhibiti istilahi mpya

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, January 13  2015 at  15:39

Kwa Muhtasari

Mojawapo ya juhudi kuu  zinazoendelea kufanywa hivi  leo na wataalamu wa Kiswahili ni ukuzaji wa istilahi. Mawanda ya matumizi ya Kiswahili, sawa na lugha nyingine yoyote ulimwenguni yanaendelea kupanuka kila uchao - hasa kwa sababu ya maendeleo ya kasi yanayojiri katika nyanja za sayansi  na teknolojia.

 

MOJAWAPO ya juhudi kuu  zinazoendelea kufanywa hivi  leo na wataalamu wa Kiswahili ni ukuzaji wa istilahi. Mawanda ya matumizi ya Kiswahili, sawa na lugha nyingine yoyote ulimwenguni yanaendelea kupanuka kila uchao - hasa kwa sababu ya maendeleo ya kasi yanayojiri katika nyanja za sayansi  na teknolojia.

Jukumu la ukuzaji wa istilahi na usambazaji zinafanywa na mashirika kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) nchini Tanzania na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (zamani ikijulikana kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – nchini Tanzania.

Hadi sasa, Kenya bado haina chombo mahususi cha kitaaluma au kiserikali kinachotwikwa  wajibu huu.  Jukumu la kubuni istilahi na kuzisambaza ama limeachiwa watu binafsi, vyombo vya habari au watu binafsi.

Baadhi ya wanataaluma ambao wanatajika kwa urahisi katika ulingo wa kubuni istilahi mpya za Kiswahini ni pamoja na Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa, Profesa Rocha Mzungu Chimerah wa Chuo Kikuu cha Pwani, Profesa Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi miongoni mwa wataalamu wengine.

 

Ukosefu wa chombo cha kiserikali

Wataalamu wanaojishughulisha na tathmini ya istilahi na leksikoni za Kiswahili wamewahi kulalamika kwamba, ukosefu wa chombo cha kiserikali na hata jopo la wataalamu wanaoweza kutwikwa jukumu la kudhibiti mchakato mzima wa kubuni, kusawazisha na kusambaza istilahi za Kiswahili nchini Kenya ni hatari.

Kwa nini? Kwa sababu mchakato huu unaweza kutekwa nyara na watu wachache wanaojitakia makuu na kuuvuruga au kupotosha shughuli nzima. Kwa bahati nzuri, nchini Kenya, hali hiyo bado haijatokea. Hadi sasa, istilahi zilizokwisha kubuniwa na Mzee Sheikh Nabhany kama vile 'tarakilishi’ na 'runinga’ zimekwisha kubalika.

Hata hivyo, Mzee Nabhany kwa muda mrefu amekuwa na wasiwasi kwamba Kiswahili kinakopa mno istilahi kutoka kwa lugha nyingine za kigeni na kuzifanyia marekebisho ili zichukue muundo wa Kiswahili.

Mapandekezo ya mtaalamu huyu aghalabu ni kuwa, aghalabu wataalamu wa Kiswahili wanapaswa kwanza kupekuapekua na kusaka lahaja zote za Kiswahili pamoja na lugha nyingine za Kiafrika kubaini iwapo dhana fulani zipo katika lugha hizo kabla ya kukimbilia kukopa.

Anachopendekeza Mzee Sheikh Nabhany ni kwamba Kiswahili kinapaswa kukuzwa mumo kwa mumo kwa kutumia kanzi ya misamiati na dhana za lugha zetu za kiasili badala ya kukopa mno kiasi kwamba lugha hii inaweza kupoteza upekee wake. Baadhi ya misamiati iliyokopwa kutoka lugha zetu za kiasili na ambayo imekubalika katika Kiswahili sanifu ni pamoja na  'ikulu’, 'kabwela’ na 'bunge (Kinyamwezi), 'kitivo’ (Kipare), na kadhalika.

 

Mapendekezo ya Nabhany

Hata hivyo, mapendekezo ya Mzee Nabhany – ingawa yana mashiko, haiyumkiniki yatekelezwe kwa urahisi. Sababu ni kwamba katika ulimwengu huu ambao umegeuka kuwa kijiji kwa sababu ya utandawazi, mipaka ya kijiografia imekwisha kufutwa. Maendeleo makubwa na ya kasi yanajiri katika sayansi na teknolojia hivi kwamba vifaa na dhana nyingi zinazuka kila uchao.

Kwa hivyo, dhana hizi zinahitaji kutafutiwa istilahi haraka mno. Na njia ya haraka ya kuzua istilahi hizi ni kwa njia ya ukopaji na utohozi.  Lugha zetu za asili huenda zisiwe na dhana ngeni kama vile kompyuta – ambazo hapo awali hazikuwa katika utamaduni wetu. Lugha huweza tu kuwa na majina na msamiati wa dhana zinazopatikana katika utamaduni wake.

Kwa sababu ya mtafaruku unaoweza kuzuka katika matumizi ya istilahi miongoni mwa vyombo vya habari na hata baina ya wataalamu wa Kiswahili, ipo  haja ya dharura ya Kenya kuwa na asasi inayoweza kutwikwa jukumu la kudhibiti mchakato mzima wa kubuni, kusawazisha na kusambaza istilahi mpya.

 

Matundura ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

 

 

Abdulaziz ana ndoto kuu kuhusu Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, July 1  2014 at  18:21

Kwa Muhtasari

Prof Abdulaziz anatabiri kwamba, miaka ishirini hivi ijayo, Kiswahili kitakuwa kimefikia hadhi ya kutekeleza mambo yote ya taifa letu ikiwemo elimu, sayansi na kadhalika.

 

MTAALAMU wa lugha na mhadhiri mkongwe wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Mohamed Hassan Abdulaziz Mkilifi ni mmoja wa wasomi wanaoheshimika sana barani Afrika. Aliasisi Idara ya Isimu na Lugha za Kiafrika katika kiwango cha Chuo Kikuu nchini Kenya mapema miaka ya 1970. Somo la Kiswahili lilianza kuwa maarufu katika idara hiyo na wataalamu wengi wamekwisha kupitia katika mikono yake.

Je, mtaalamu huyu ana maoni na fikra zipi kuhusiana na masomo ya Kiswahili katika vyuo vikuu? Je, ana maoni gani kuhusu Kiswahili katika utambulisho na maendeleo nchini Kenya na kwingineko, Kiswahili katika maendeleo ya kisasa ikiwemo tafsiri na Teknohama? Mnamo Novemba 9, 2009,  mtaalamu wa tafasiri marehemu Profesa Naomi Luchera Shitemi alifanya mahojiano na Profesa Abdulaziz.

Kwa bahati nzuri, mtaalamu huyo alichapisha mahojiano hayo kwenye kitabu chake, Kubidhaaisha na Kuwezesha Lugha kama Sarafu ya Kiuchumi na Kijamii: Kielelezo cha Taaluma za Kiswahili na Tafsiri (Moi University Press, 2011) ambacho nimekwisha kumaliza kukisoma. Mwandishi wa kitabu hiki ameambatisha mahojiano baina yake na Profesa Abdulaziz ambapo anazungumzia kwa uketo na kina kikubwa sana masuala tuliyokwisha kuyataja katika mwanzo wa makala haya. Profesa Abdulaziz anavuta taswira ya hali ilivyokuwa tangu enzi ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki iliyokuwa na Idara ya Kiswahili na Isimu na wanafunzi wa kwanza  aliowafundisha  - mathalan Ebrahim Hussein, Euphrase Kezilahabi, Ruth Mfumbwa Besha (marehemu), Clement Maganga na Mugyabuso Mulinzi Mulokozi.

Anasema kwamba wanafunzi hawa walikuwa na ari kubwa sana – na kwa kweli wengi waliishia kuwa maprofesa wa fasihi na isimu ya Kiswahili, huku wengine wakiishia kuwa waandishi  hodari sana wa tamthilia na riwaya. Ebrahim Hussein kwa mfano alitunga tamthilia zilizoleta mabadiliko makubwa sana katika utanzu huo. Hizi ni pamoja na Kinjeketile na Mashetani. Euphrase Kezilahabi kwa upande mwingine anadaiwa na wahakiki kuwa mmoja wa watunzi mahashumu wa riwaya ya Kiswahili Afrika Mashariki na Kati. Tungo zake  ni pamoja na Kichwamaji, Rosa Mistika, Gamba la Nyoka, Nagona na Mzingile. Profesa Abdulaziz anasema kwamba wataalamu hawa walitoa fasihi ambazo mtu anaweza akachukulia kuwa fasihi za kilimwengu.

Anakiri kwamba profesa mmoja kutoka Ufini aliwahi kumwambia kwamba fasihi ya Kiswahili ilikuwa imeafikia viwango vya fasihi ya kilimwengu kwa sababu ina kiwango cha juu sana katika habari za wahusika, ploti na hata maudhui. Kauli hii ni ya kweli – hata bila kusubiri mtaalamu wa nje kutambua jambo hilo. Baada ya kuondoka katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki mnamo miaka ya 1970, Profesa Abdulaziz alianzisha Idara ya Isimu la Lugha za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi – na mwanafunzi wake wa kwanza aliyefanya shahada ya uzamili ni Profesa Chacha Nyaigotti Chacha ambaye alikuwa wa kwanza kuandika tasnifu yake kwa kutumia Kiswahili.

Maarifa

Hatua hiyo ilifungua milango ambapo wataalamu wa baadaye walianza kuandika tasnifu zao za viwango vya uzamili na uzamifu kwa kutumia Kiswahili. Hii inadhihirisha kwamba, Kiswahili kinaweza kutumika kuelezea maarifa yoyote yale yawayo kikamilifu. Profesa Abdulaziz anakariri kwamba asilimia tisini ya shughuli za uchumi nchini Kenya zinaendelezwa kwa lugha za kiasili na Kiswahili.

Katika maeneo ya viwandani na jua kali na hata polisi kwa mfano, wafanyakazi huongea Kiswahili. Kiingereza – ambayo ndiyo lugha inayotumiwa na wasomi teule hutumika katika uchumi wa juu kama vile kwenye mabenki. Prof Abdulaziz anatabiri kwamba, miaka ishirini hivi ijayo, Kiswahili kitakuwa kimefikia hadhi ya kutekeleza mambo yote ya taifa letu ikiwemo elimu, sayansi na kadhalika.

Ukweli ni kwamba Kiswahili ni sasa ni lugha ya kimataifa inayozungumzwa na takriban watu milioni 200  wengi wao wakiwa wakazi wa Afrika Mashariki na mataifa ya Maziwa Makuu. Lugha hii inazidi kupata imaarufu kila uchao katika teknohama na mawasiliano mengine ya aina hiyo.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

 

 

Mandela ametufunza jinsi ya kuandika historia

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Friday, December 13  2013 at  12:21

Kwa Muhtasari

Watakapohesabiwa basi watu walioacha taathira kubwa mno ulimwenguni, Mzee Nelson Mandela hatakosa kuhesabiwa. Atatoka wapi mwingine kama yeye?

 

KWA muda wa miezi mitatu hivi, ulimwengu ulisubiri kwa hamu na ghamu kifo cha  shujaa wa Afrika kusini – Nelson Mandela Madiba. Mzee Mandela alilazwa hospitalini baada ya kupata maambukizi ya mapafu. Waganga waliposhindwa na hatimaye kuinua mikono, alirudishwa nyumbani kwake ambako hatimaye alijiondokea ulimwenguni kimyakimya wakati ambapo ulimwengu ulikuwa umekwisha ‘kusahau’  kusubiri kifo chake kilichokuwa kinasubiriwa.

Vyombo vya habari – ambayo vilikuwa vinatarajia kuondoka kwa jagina huyu duniani viliandaa mapema taarifa kuhusu maisha ya jagina huyu na kuzichapisha mara moja pindi tu tanzia hiyo iliposambaa ulimwenguni mithili ya moto kwenye biwi la nyasi kavu wakati wa kiangazi. Ulimwengu uliamkia taarifa za tanzia za Mzee Mandela kwa mshangao mkubwa hali iliyoonyesha kwamba haukutosheka na muda wa miaka 95 aliyoishi Mandela.

Pembe zote za dunia – wakiwemo makaburu wanafiki waliowatesa raia wa Afrika kunisi wanaelekea kukubaliana kwamba Mzee Mandela hakuwa mtu wa kawaida. Je, ni mhimili upi mkuu au ni kiunzi gani kilichomfanya Mzee Nelson Mandela  kuacha taathira kubwa kuwahi kuonekana mpaka sasa katika siku za hivi karibuni? Katika kitabu chake, No Easy Walk to Freedom (1965), Mzee Mandela anasema hivi kwenye blabu: “Katika maisha yangu, nimejitolea kwenye mapambano haya ya Waafrika. Nimekwisha kupigana dhidi ya  utawala na ubaguzi wa rangi dhidi ya Wazungu na vilevile ule wa watu Weusi.

Nimeishi na matumaini makubwa ya kujiri kwa jamii huru yenye demokrasia ambapo watu wote wanaishi kwa amani na utengamano na wakiwa na nafasi sawa. Ni azma ambayo ninatumainia  kuishi na kuitimiza. Lakini ikiwa kutakuwa na haja, ni azma ambayo niko tayari kuifia.” Mzee Mandela sasa amekwisha kufa. Je, azma ndoto hii yake ilikwisha kutimia? Jibu la swali hili ni ndio na la. Ni ndio kwa sababu kwa kiasi fulani, aliweza kuikomboa Afrika ya kusini, akatawala kwa miaka mitano – kisha sawa na hayati Mwalimu Kambarage Nyerere, akang’atuka kutoka uongozini. Licha ya kuchukua hatua hii ya kistaarabu, bado kuna viongozi wengine katika bara hili jeusi ambao wamekwamilia madaraka kwa minajili ya kutosheleza maslahi yao ya kibinafsi.

Mifano inayotajika kwa urahisi ni Yoweri Museveni wa Uganda na Robert Mugabe wa Zimbabwe. Jibu ni hapana kwa sababu mataifa mengi barani Afrika yanakabiliwa na tisho la utawala mbovu wa ukandamizwaji wa wanyonge na wachache matajiri pamoja na wasomi teule.

Kifo cha Mzee Nelson Mandela hivyo basi kinapaswa kuwa mwamko mpya kwa viongozi wengi barani Afrika ambao bado hawajazinduka na kufahamu kwamba siku moja, wataporomoshwa na wimbi la wakati. Mzee Mandela, sawa na mhusika Kinjeketile wa tamthilia ya Ebrahim Hussein, Mashetani alizaa neno  ambalo lilikuwa kubwa kuliko aliyelizaa.

Kusameheana

Katika utu wake na udhaifu wake, kiongozi huyu alidhihirisha wazi kwamba ulimwengu unaweza kuwa bora zaidi iwapo watu watasameheana na kuishi pamoja na kukirimiana kwa hali na mali; kwamba inawezekana mtu akaleta mabadiliko makubwa kwa kushirikiana na watu wengine na kupigana dhidi ya dhuluma bila kutarajia manufaa yoyote ya kibinafsi.

Historia itakapoandikwa hatimaye, itabainika wazi kwamba watu sampuli ya Mzee Mandela ni adimu sana kutokea katika sayari hii yetu iitwayo dunia. Lakini pia tunapomweka kiongozi huyu kwenye mizani ya majagina katika jamii zetu za Kiafrika na yingine ulimwenguzi inabainika wazi kwamba watu sampuli ya Mandela huzuka katika mazingira ya kutetea Wanyonge na kwamba vifo vyao vinapotokea, hutikisa utando wa kijamii kwa namna moja au nyingine.

Katika jamii ya Uswahilini, tuna Fumo Liyongo; katika jamii ya Wayahudi, tuna Yesu na akina Musa. Katika Mashariki ya Kati, tuna majagina kama Gilgamesh. Watakapohesabiwa basi watu walioacha taathira kubwa mno ulimwenguni, Mzee Nelson Mandela hatakosa kuhesabiwa.

Atatoka wapi mwingine kama yeye? Ni matumaini yangu kwamba kifo cha Mzee Nelson Mandela hakitasimamisha kamwe gurudumu la mapambano ya haki na usawa ulimwenguni. Ikiwa mapambano hayo hayakufua dafu katika uhai wake; yatakuja kunanikiwa siku moja. Mradi tusikate tama.

ematundura@chuka.ac.ke

 

 

Lugha ya Kiswahili itafaa Afrika Mashariki

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, October 31  2013 at  12:13

Kwa Muhtasari

Si suala la mjadala tena kwamba lugha inayofumbata hisia za wenyeji wengi wa Afrika ya Mashariki ni Kiswahili. Kwa hiyo, ni upumbavu wahakiki kuifumbia macho fasihi ya Kiswahili ambayo inazidi kupanuka kila uchao.

 

KATIKA kongamano la wataalamu wa lugha  lililofanyika jijini Nairobi mnamo Septemba mwaka huu, mwandishi mahashumu, Prof Euphrase Kezilahabi wa Tanzania alishangaa kwamba, ingawa Kiswahili ni lugha iliyochangia sana katika  kuenea kwa dini, elimu na kufanikisha biashara Afrika ya Mashariki na kati kwa muda mrefu, haijasaidia sana kuleta umoja na muumano maridhawa katika eneo hili. Kadhalika, kwenye kongamano hili, wataalamu wawili na watunzi wapevu wa fasihi ya Kiswahili – Prof John Hamu Habwe na  Prof Kithaka wa Mberia, wa Chuo Kikuu cha Nairobi walilalamika kwamba, wahakiki wa fasihi kwa muda mrefu wamekuwa wakiipuuza fasihi ya Kiswahili na kuiweka pembezoni katika taaluma nzima ya uhakiki. Mdahalo anaouzua Prof Euphrase Kezilahabi si mgeni – bali umewahi kuwavutia wasomi, wanasiasa, wanahistoria na hata wanahabari.

Si swala la mjadala tena kwamba lugha inayofumbata hisia za wenyeji wengi wa Afrika ya Mashariki ni Kiswahili. Ingawa watu wa mataifa haya waligawanywa kwa kuwekewa mipaka na wakoloni kwa minajili ya wakoloni hao kukidhi mahitaji yao ya kisiasa na kiuchumi, kimsingi watu wa eneo hili wana historia na tamaduni zilizokurubiana.

Sina hakika iwapo Prof Kezilahabi amekwisha kusoma vitabu vitatu ambavyo nafikiri vinaweza kujibu swali lake. Vitabu hivyo ni Swahili State and Society: The Political Economy of ana African Language (Alamin Mazrui na Ali Mazrui), The Power of Babel (Mazrui na Mazrui), Kiswahili: Past, Present and Future Horizons (Rocha Chimerah), na Language Policy in East Africa (Ireri Mbaabu). Katika Swahili State and Society, Prof Ali Mazrui na Prof Alamin Mazrui wanahoji kwamba ufuasi watu katika makabila yao bado ni mkubwa sana Afrika kwa jumla na hasa Afrika ya Mashariki.

Hali hii ilidhihirika katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Machi mwaka huu – ambapo tuliona watu wakiamini sana vyama vya kisiasa kwa misingi ya ukabila bila kutilia maanani sera za vyama hivyo. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw Raila Odinga alikuwa na wafuasi wengi kutoka watu wa Kabila lake, huku rais Uhuru Kenyatta akiwa na wafuasi wengi kutoja jamii yake ya Agikuyu, naye naibu wake Wiliam Ruto akiwa na wafuasi wengi kutoka kwa jamii yake ya Wakalenjin.

Huku Prof Kezilahabi akiwa ana wasiwasi kwamba Kiswahili bado hakijafanikiwa kuunganisha watu wa Afrika ya Mashariki, Prof Chimerah ana mtazamo tofauti. Ameipanulia mawanda lugha hii na kuipigia upatu iwe lingua franka ya bara la Afrika. Mtazamo wa Prof Ireri Mbaabu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta kuhusu suala hili ni kwamba, mikakati ya kisera kuhusiana na lugha  katika mataifa ya Afrika Mashariki ni tofauti. Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Tanzania.

Hivi majuzi, serikali ya Kenya ilikikweza hadhi Kiswahili kuwa lugha rasmi  sambamba na Kiingereza – licha kwamba bado Kiswahili ni lugha ya taifa. Nchini Uganda, Kiswahili bado hakijapokelewa vizuri kwa sababu kinaendelea kupata ushindani mkubwa kutokana na lugha ya Luganda. Isitoshe, kwa muda mrefu, Kiswahili nchini humo kimekuwa kikipigwa vita kwa sababu kilihusishwa na ukatili wa wanajeshi. Hatua ya Kenya kurasimisha Kiswahili sambamba na Kiingereza ni tamko la kisera.

Kuendeleza Kiswahili

Hadi sasa, hatujaona hatua za kimakusudi za kulifanyia kazi tamko hili. Kenya, haina chombo rasmi cha kiserikali kinachoweza kutekeleza majukumu ya kuendeleza Kiswahili kimakusudi. Jukumu hili limeachiwa watu binafsi na vyombo vya habari kama vile gazeti la Taifa Leo.  Kuhusu suala la kuwekwa pembezoni kwa fasihi ya Kiswahili na wahakiki wa fasihi wanaozingatia mno fasihi ya Kiingereza, ni hali ya kusikitisha mno. Wasichokifahamu wahakiki hawa ni kwamba, fasihi ya Kiswahili imepiga hatua mno hasa kuhusiana na utuzi wa kimajaribio.

Kwa hiyo, ni upumbavu wahakiki kuifumbia macho fasihi ya Kiswahili ambayo inazidi kupanuka kila uchao. Kimsingi, kinachozuia Afrika Mashariki kuungana na kuwa na mshikamano anaoutaka Prof Kezilahabi ni tofauti za kisiasa, kiuchumi na kisera ambazo hazijawianishwa. Muungano wa Afrika ya Mashariki utakapoimarika, labda ndipo mataifa ya eneo hili yatakapofikia mshikamano wa kuridhisha utakaofanikiswa kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

ematundura@chuka.ac.ke

 

 

Uwazi unahitajika katika tuzo ya fasihi

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, October 3  2013 at  12:06

Kwa Muhtasari

Ingawa tuzo ya Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta imekuwa ikitolewa kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, pana haja ya kuanza kuuliza maswali fulani ya kimsingi ambayo labda majibu yake yatatusaidia kuirejeshea hadhi tuzo hiyo.

 

MAKALA ya kumi na sita ya Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu yalimalizika jijini Nairobi juma lililopita. Maonyesho hayo huandaliwa na Chama  cha Wachapishaji cha Kenya  (KPA) kila mwaka. Ingawa makala ya mwaka huu yaliwavutia wachapishaji wengi, wakereketwa wa wapenzi wa vitabu hawakufika kwa wingi kutokana na shambulizi la ugaidi majuma mawili yaliyopita.

Kilele cha maonyesho hayo  kilikuwa ni utuzaji wa waandishi bora wa vitengo mbalimbali vya fasihi ya Kiswahili na Kiingereza kwa kuwapa Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta 2013.

Tuzo hii iliyoasisiwa mnamo miaka ya 1970 ndiyo tuzo ya kifahari ya kifasihi Afrika Mashariki na Kati. Vitengo ambavyo huwaniwa kila baada ya miaka miwili ni pamoja na fasihi ya watu wazima (Kiswahili na Kiingereza), fasihi ya vijana (Kiswahili na Kiingereza) na kitengo cha fasihi ya watoto  katika lugha hizo mbili.

Ingawa tuzo hii imekuwa ikitolewa kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, pana haja ya kuanza kuuliza maswali fulani ya kimsingi ambayo labda majibu yake yatatusaidia kuirejeshea hadhi tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwanzilishi wa taifa hili – hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Je, mchakato mzima wa uteuzi, tathmini na uwasilishwaji wa tuzo hii unafanywa kwa njia ya haki?

Mbona ripoti za jopo la majaji  wanaotathmini na kutoa maamuzi ya tuzo hiyo hayatolewi hadharani?

Je, jopo hilo lina majaji wanaoelewa barabara fasihi ya Kiswahili? Ikiwa jibu ni ndio, mbona vitabu vizuri vya fasihi  ya Kiswahili ambavyo huwasilishwa  kuwania tuzo hiyo huishia hata kutoteuliwa kuwa kwenye orodha fupi ya kazi bora?

 

Heri subira

Mfano wa riwaya nzuri ambayo iliwasilishwa kuwania tuzo hiyo mnamo 2011 ni Heri Subira ya Omar Babu (Oxford University Press).

Ajabu ni kwamba, riwaya hiyo hata haikuteuliwa na majaji. Je, sababu ziliwahi kutolewa kuhalalisha hatua hiyo. Heri Subira kwa maoni yangu ni mojawapo wa riwaya bora za Kiswahili kuwahi kuandikwa. Je, mbona vitabu vingi ambavyo vimewahi kushinda  Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta    havichangamkiwi  na wasomaji – kuakisi ubora wao kifasihi?

Ni muhimu pia kutaja kwamba ipo haja ya fedha za Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta kuongezwa kutoka Sh75,000 anazotuzwa mshindi katika vitengo vya fasihi ya watoto na ya vijana kufikia kiwango kizuri cha fedha kinachoweza kumliwaza mwandishi ambaye huchangia sana katika maendeleo ya jamii.

Aidha, kiwango cha hela kwenye kitengo cha fasihi ya watu wazima kwenye tuzo hiyo kinapaswa kuongezwa na kuzidi Sh150,000.

Ni jambo la kukatisha tamaa kwamba waandishi ambao ni viungo muhimu katika utamaduni na maendeleo ya jamii hawanufaiki mno kutokana na jasho lao.

Vilevile ni kinaya kwamba ingawa Tuzo hii inahusishwa na jina la rais wa kwanza wa taifa hili – Mzee Jomo Kenyatta, kiasi hicho cha fedha ni kidogo mno kuhusishwa na jina kubwa kama hilo.

Kwa hiyo, ili Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta iweze kudumisha hadhi yake stahiki katika eneo la Afrika Mashariki na Kati, ipo haja ya mchakato mzima wa utoaji wa tuzo yenyewe kufanywa kwa njia ya uwazi, haki na ukweli.

La sivyo, waandishi wanaotuzwa  bila maadili haya ya kimsingi kufuatwa watakuwa wanadanganywa kwamba wanachangia maendeleo ya fasihi – ilhali kazi zao ni chapwa na za masafa mafupi.

Uandishi sawa na tanzu nyingine za sanaa una viwango. Kazi zinazotuzwa basi baada ya kila miaka miwili lazima zionekane na kujidhihirisha wazi kustahili tuzo hii.

Aidha, wachapishaji wa vitabu wanapaswa kuwa katika msitari wa mbele kudhibiti na kudumisha viwango vya fasihi bora ili kuweza kuakisi hali halisi ya uandishi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

ematundura@chuka.ac.ke

 

 

Daya yetu ni haki na maridhiano

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, September 19  2013 at  12:16

Kwa Muhtasari

Mkabala wa ukweli na maridhiano ambao ulifanikiwa Afrika Kusini na Rwanda – ambazo zilikuwa na tatizo sawa na la Kenya ndio utakaonasua Kenya kutokana na lindi la masaibu tunayoyashuhudia hivi sasa.

 

NILIFUATILIA kwa makini ushahidi wa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka katika Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa – ICC ambaye aliwasilishwa na prosekiuta  Bi Fatou Bensouda. Kwa vyovyote vile, ushahidi huo uliibua hofu na huruma katika moyo wangu.

Masimulizi ya shahidi huyo  ambaye kwa wakati mmoja alishindwa kusimulia masaibu yaliyomsibu alilia kwa kite kwa kuwa aliyokuwa anayasimulia ni maovu ambayo yanaonyesha jinsi moyo wa binadamu unaweza kusitini na kusheheni uovu wa binadamu.

Nilihisi kwamba nilikuwa ninaota, na kwamba tukio  hilo lililosababisha zaidi ya watu 35 kuteketezewa ndani ya Kanisa katika eneo la Kiambaa lilikuwa ni kama sinema. Ushahidi wa shahidi huyu umenichochea kuanza kutafakari na kujiuliza msururu wa maswali. Je, inawezekana vipi  shahidi huyu kusimulia kwa mguso mambo ambayo hakuyashuhudia yeye? Ingawa upande wa utetezi umekwisha kudai kwamba mashahidi wengi walilipwa ili kubuni ushahidi wa uwongo, haiyumkiniki shahidi huyu wa kwanza anasimulia mambo ambayo hakuyaona kwa kina na uketo mkuu kwa jinsi alivyoelezea.

Je, haya ndiyo mambo tunayotaka kuyasahau na kuendelea kana kwamba hakuna lolote lililotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa  2007? Je, ni shahidi huyu tu aliyeyashuhudia mambo haya au kuna wengine sawa nay eye ambao waliona na kujinyamazia?

Inakera zaidi kwamba hivi  sasa tumeanza kushuhudia   hali ya kujipendekeza na kujikomba kwa viongozi wetu kuhusiana na suala zaima la kesi ya Kenya katika mahakama ya ICC.

Kwa maoni yangu, suala zima la kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta,  naibu wake  Wiliam Ruto na mwanahabari Joshua arap Sang huenda isiwe na manufaa makubwa kwa taifa hili – hata pale ambapo ama wote watapatikana na hatia, au wote wachiliwe huru – au mmoja apatikane na hatia au hata kesi itupiliwe mbali kwa sababu ya 'ukosefu wa ushahidi’ au ushahidi wa uwongo.

Kwa nini? Nitatoa sababu zifuatazo. Mwanzo, tangu hapo mbeleni, Kenya haijachukua hatua za kimakusudi za  kuleta uwiano na mshikamano unaoweza kuibua hali ya msamaha kwa waathiriwa wa ghasia za baada ya Uchahuzi Mkuu  wa 2007. Kufikia sasa, mikakati ya kuleta pamoja makabila yanayozozana  imeonekana tu katika kiwango cha  kisiasa. Mapema mwaka huu, Bw Uhuru Kenyatta na Wiliam Ruto waliungana  kwa misingi kwamba walitaka kuunganisha jamii za Agikuyu na Kalenjin – ambazo kwa hakika zilikuwa zainazozana katika Uchaguzi Mkuu wa  2007.

Karata yao ilikuwa nzito kiasi kwamba ilimbwaga Wazizi Mkuu wa zamani – Bw Raila Odinga. Je, hilo limetosha?  Viongozi hawa watawahi kuanzisha mchakato wa watu kusameheana katika ngazi ya mashinani baada ya kuungana katika ngazi ya kisiasa? Je, kiini cha mzozo huo ambacho ni masuala ya kihistoria na ukosefu wa usawa katika ugavi wa raslimali kitawahi kushughulikiwa kikamilifu?

Mnamo 2002, Wakenya waliungana kumchagua rais mstaafu, Bw Mwai Kibaki ili kuondolea mbali utawala dhalimu wa Bw Moi ambaye alikosa kuitendea haki nchi hii kwa zaidi ya miongo miwlili ambayo aliitawala Kenya.

Mshikamano

Bw Kibaki alikuwa na fursa nzuri ya kuibua mshikamano wa kitaifa ninaouzungumzia katika muktadha huu – kwamba yeye alipigiwa kura na takriban watu wa makabila yote nchini.

Ikiwa basi Bw Kibaki alishindwa kuleta mshikamano wa kitaifa baada ya kuchaguliwa kwa kauli moja na makabila zaidi ya 42  ya Kenya, Uhuru Kenyatta na Bw Ruto watafanikiwa kufanya hivyo hasa ikizingatiwa kwamba kura zao nyingi zilitokana na muungano wa jamii mbili pekee? Kwa maoni yangu, suala zima la kuunganisha makabila yaliyozozana 2007/2008 baada ya Uchaguzi Mkuu litatatuliwa vyema na kwa ufanisi mkuu kwa njia ya kuwadara watu waliyotekeleza maovu hayo wajitokeze hadharani, wakiri kwamba walifanya unyama huo na wasamehewe.

Kwa hiyo, mkabala wa ukweli na maridhiano ambao ulifanikiwa Afrika Kusini na Rwanda – ambazo zilikuwa na tatizo sawa na la Kenya ndio utakaonasua Kenya kutokana na lindi la masaibu tunayoyashuhudia hivi sasa. Kujiondoa katika Mkataba wa Roma na hali ya kujikomba kwa wanasiasa wetu kamwe hakutatusaidia chochote. Hizi ni njia za mkato ambazo zitatutia taabani katika siku za usoni.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

ematundura@chuka.ac.ke

 

 

Makosa katika matumizi ya Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Monday, June 17  2013 at  11:32

Kwa Muhtasari

Ili kuepuka makosa ambayo yanakiparaganya Kiswahili, wanafunzi, watumiaji wa lugha hii, walimu na hata wanahabari wanapaswa ama kufanya utafiti wanapokuwa na shaka kuhusu neno fulani, kuangalia kamusi inasema nini au hata kuwauliza wataalamu.

 

JAMBO ambalo aghalabu limekuwa likinishangaza mara kwa mara ni juhudi za kimakusudi ambazo hufanywa na watu nchini ili kuzungumza na hata kuandika Kiingereza 'safi’.

Watu wengi wakiwemo wanafunzi huaibika pale wanapogundua kwamba 'wamevunja’ Kiingereza ama kwa kutotumia msamiati unaofaa au hata kutamka maneno visivyo. Hata hivyo, hali ni kinyume katika matumizi ya lugha zetu za kiasili – hasa Kiswahili. Vyombo vya habari pia havimakiniki ipasavyo katika matumizi sahihi ya baadhi ya msamiati wa Kiswahili. Hali hii hutokana na ama kuipuuza lugha hii au hata kutojua.

Hii ni hatari kwa sababu mbili. Mosi mbali na kupotosha umma,vyombo vya habari vinavyoparaganya Kiswahili huwa vinaupiga mhuru msamiati unaotumika vibaya kukubalika miongoni mwa umma kwa sababu ya ushawishi wao mkubwa. Katika makala hii, nitaangazia baadhi ya maneno ambayo hutumiwa vibaya  na vyombo vya habari pamoja na wazungumzaji wengine wa Kiswahili. Watu wengi kwa mfano – wakiwemo wanahabari hutumia msamiati  'jambazi’ na jangili kama visawe au maneno yenye maana sawa.

Fauka ya hayo, maneno haya hutumia maneno haya nje ya maana zao sahihi. Kwa mfano, utamsikia mtu akisema, “Majangili yamevamia mkahawa jijini Mombasa”. Au watu wengine husema, “Majangili yameiba nguo zilizokuwa zimeanikwa nje ya nyumba.” Matumizi ya neno jangili katika mifano hii miwili sio sahihi.

Jambazi  maana yake ni jitu janja sana linalowalaghai watu  na kuwaibia, ni jitu lisilokuwa na huruma ambalo aghalabu hutumia mabavu katika kuiba na si mdokozi au mwizi yeyote. Maana sahihi ya neno 'jangili’ ni mwindaji haramu kwenye mbuga za kuhifadhia wanyama ambaye lengo lake ni kuwinda bila kibali kwa matumaini ya kupata ngozi, pembe au nyama ya wanyama hao ili kufanyia biashara. Kosa jingine ni matumizi ya maneno 'nona’ na 'nenepa’.

Watu wengi husikika wakisema kwamba,’ “Siku hizi Juma Namlola amenona sana.” Kwa kweli iwapo kauli hii sio ya utani, kumwambia mtu kuwa amenona sio vizuri. Binadamu hunenepa na ni wanyama ambao kunona. Msamiati mwingine unaotumiwa vibaya na vyombo vya habari ni 'tetesi’. Watangazaji wengi hudhania kuwa tetesi ni malalamiko.

Kwa mfano, “Ufujaji wa fedha za mpango wa elimu bila malipo umesababisha tetesi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanaharakati.” Kauli hii sio sahihi iwapo wanahabari wanamaanisha kwamba kufujwa kwa fedha za mpango huo zimesababisha hali ya kutoridhika. 'Tetesi’ kwa hakika ni uvumi.

Kwa mfano, kulikuwa na tetesi kwamba  rais wa Marekani, Barak Obama alikataa kuzuru Kenya kwa sababu ya viongozi wa serikali ya muungano kutowajibika katika kutekeleza ajenda ya nne ya marekebisho nchini. Vilevile vyombo vya habari na hata wazungumzaji hutumia visivyo neno 'jihami’.

Kwa mfano, 'Majambazi waliojihami (?) kwa bunduki walivamia benki ya Equity mjini Maua na kutoweka na bunda la noti’.Neno jihami hapa limetumika visivyo – huku anayelitumia kwa njia hii akimaanisha kuwasilisha fahiwa ya 'majambazi wenye silaha’. Aidha, baadhi ya vyombo vya habari hutumia dhana ya 'mkurupuko’ wa maradhi  kumaanisha 'mlipuko’ wa maradhi.

Utamaduni

Neno 'kukurupuka’ lina fahiwa ya dhana ya Kiingereza ya 'stampede’. Isitoshe, neno 'utamaduni’ hutumiwa na watu wengi  kwa maana ya  'asilia’ au 'kienyeji’.

Imekuwa kawaida kuwasikia watu wakisema au kuzungumza kuhusu ngoma za utamaduni  wakiwa na maana ya ngoma za kiasili. Utamaduni kwa hakika maana yake ni ustaarabu, maendeleo ya kijumuia na fani mbalimbali zinazohusiana na mambo hayo – tabia, mila, desturi,lugha, mapishi, imani, matamanio, mbeko, mavazi na kadhalika.

Ili kuepuka makosa haya ambayo yanakiparaganya Kiswahili tulivyotaja awali, wanafunzi, watumiaji wa lugha hii, walimu na hata wanahabari wanapaswa ama kufanya utafiti wanapokuwa na shaka kuhusu neno fulani, kuangalia kamusi inasema nini au hata kuwauliza wataalamu.

Ni salama kila mara kukaa kimya kuhusu jambo usilolielewa na watu wakachukulia kwamba hulijui kuliko kuzungumza au kuandika kitu usichokijua na kuondolea mbali shaka ya watu hao. Isitoshe, kuuliza si ujinga!

bitugi@yahoo.com

 

 

Makabila mengi ni baraka au laana?

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Monday, May 20  2013 at  12:13

Kwa Muhtasari

Mataifa mengi barani Afrika yameshindwa kubuni na kutekeleza sera za lugha zinazotambua umuhimu wa lugha za Kiafrika. Lugha za kigeni kama vile Kiingereza hutumika pakubwa katika kuendesha masuala ya bara hili umefanikiwa katika kubuni tabaka la wasomi teule mijini ambao wamejitenga mno na wakazi wa mashambani ambao ni wengi na maskini.

 

KONGAMANO la Saba la Kimataifa Kuhusu Lugha na Maendeleo lilifanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia mnamo Oktoba 2005. Kikao hicho kilikuwa cha kihistoria kwa sababu mbili zinazohusiana.

Mosi, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mkutano wa kiwango hicho kufanyiwa barani Afrika tangu misururu ya makongamano ya daraja hiyo yalipoanza kuandaliwa mjini Bangok, Thailand mnamo 1993.

Pili, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa kongamano la kiwango hicho pia kuangazia suala nyeti na tata kuhusu hali ya lugha barani Afrika. Miongoni mwa washiriki katika mkutano huo walikuwa ni pamoja na wataalamu wa lugha,elimu na maendeleo.Aidha, kikao hicho kilihudhuriwa na wawakilishi wa makundi ya kijamii na maafisa wa serikali.

Washiriki hao waliozidi mia moja walitoka pembe mbalimbali ulimwenguni. Kongamano hilo liliandaliwa na Baraza la Uingereza kwa ushirikiano na Shirika la Marekani kuhusu Ufadhili wa Maendeleo ya Kimataifa (USAid), Idara ya Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Uingereza na Wizara ya Elimu ya Ethiopia. Ingawa mada iliyopewa kipaumbele katika kikao hicho ilikuwa ni lugha na maendeleo, midahalo mbalimbali ya kuvutia kuhusu masuala hayo ilichipuka kwenye kongamano hilo.

Mojawapo suala lilizozuka lilihusu wingi wa lugha balani Afrika. Wanataaluma katika kikao hicho walipigia darubini suala hili huku wakitathmini iwapo hali ya bara hili kuwa na ndimi nyingi ni balaa au neema? Wanakongamano hilo walihoji iwapo lugha hizo ni muhimu katika maendeleo au ni vikwazo vya maendeleo.

Wawasilishaji kadha walielezea kwa marefu na mapana kuhusu hali ya lugha kwenye mataifa yao. Ilibainika kwamba, mataifa mengi Kusini mwa Jangwa Sahara yana lugha nyingi katika hali ambayo haijawahi kuonekana kwingineko ulimwenguni. Huku likiwa na jumla ya mataifa 53, bara Afrika ndilo bara lenye nchi nyingi. Mataifa kadhaa yana mamia ya lugha mbalimbali.

Hali ambapo mataifa yana watu wachache lakini wa lugha tofauti ilifumbatwa vizuri na kauli 'Watu wachache, lugha nyingi’. Kwa usemi mwingine, ikilinganishwa na sehemu nyingine ulimwenguni, mataifa ya Afrika yana idadi ndogo ya watu lakini wa makundi ya makabila mbalimbali.Mfano mzuri ni Cameroon ambayo ina takriban watu milioni kumi lakini zaidi ya lugha 250. Wataalamu katika kikao hicho pia walihoji ni kwa namna gani mataifa ya Afrika yametumia lugha zinazozungumzwa ndani ya mipaka yao.

Kwa mfano, licha ya ukweli kwamba mataifa ya Afrika yalitawaliwa na koloni mbalimbali za Ulaya kaika karne ya 20, ahari za utawala huo zinaonekana kufanana kutoka taifa moja hadi jingine.

Mataifa yote barani Afrika yamezipa kipaumbele lugha za kigeni katika masuala yao ya kitaifa.Kuanzia kaskazini hadi kusini, mashariki hadi magharibi, lugha za bara Ulaya ndizo zinatumika kama lugha rasmi huku lugha za Kiafrika zikiwekwa pambezoni. Lugha hizi hutumika sana na watu ingawa hazitambuliwi rasmi.Aghalabu lugha za kigeni hutumiwa kufundishia katika mifumo mingi ya elimu.

Uhuru

Mojawapo ya sababu bayana zinazochangia lugha za kigeni kuendelea kutawala masuala mengi ya mataifa mengi 'huru’ barani Afrika ni kwamba, mchakato wa kupata uhuru kamili haukuwahi kukamilishwa. Wasomi wa Kiswahili kwa mfano wametumia dhana ya 'uhuru wa bendera’ kuelezea hali duni ya aina ya uhuru tuliopata.

Kwamba, bendera ni ishara ya uhuru tu – na hakuna kingine cha mno. Miundomsingi na mifumo ya uhuru ilisalia vivyo hivyo baada ya wakoloni kuondoka. Hii ni pamoja na uchumi, mifumo ya kiutawala,ulinzi, elimu muhimu mno – lugha. Uhuru kamili ungeleta mabadiliko kamili kutuwezesha kuktumia raslimali za kiasili ikiwemo lugha katika kuangazia mahitaji ya watu wengi.

Watu wanapozungumzia ukosefu wa maendeleo katika mataifa mengi ya Afrika,huwa wanarejelea sana suala la uchumi. Huku ni kuangalia mambo kwa njia nyepesi mno. Mumo kwa mumo katika umaskini wetu kuhusiana na umilisi wa mali ni umaskini wa utamaduni ambao unadhihirika wazi katika hali yetu ya kuendelea kutegemea lugha za kigeni.

Hali hii inabainika wazi kutokana na ukweli kwamba, mataifa mengi barani Afrika yameshindwa kubuni na kutekeleza sera za lugha zinazotambua umuhimu wa lugha za Kiafrika.

Lugha za kigeni kama vile Kiingereza hutumika pakubwa katika kuendesha masuala ya bara hili umefanikiwa katika kubuni tabaka la wasomi teule mijini ambao wamejitenga mno na wakazi wa mashambani ambao ni wengi na maskini. Aidha suluhisho kwa hali hiyo katika eneo la Afrika ya Mashariki ni kuchukua hatua za kimakusudi wa kuwa na mfumo wa uwili lugha.

bitugi@yahoo.com