Makosa katika matumizi ya Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Monday, June 17  2013 at  11:32

Kwa Muhtasari

Ili kuepuka makosa ambayo yanakiparaganya Kiswahili, wanafunzi, watumiaji wa lugha hii, walimu na hata wanahabari wanapaswa ama kufanya utafiti wanapokuwa na shaka kuhusu neno fulani, kuangalia kamusi inasema nini au hata kuwauliza wataalamu.

 

JAMBO ambalo aghalabu limekuwa likinishangaza mara kwa mara ni juhudi za kimakusudi ambazo hufanywa na watu nchini ili kuzungumza na hata kuandika Kiingereza 'safi’.

Watu wengi wakiwemo wanafunzi huaibika pale wanapogundua kwamba 'wamevunja’ Kiingereza ama kwa kutotumia msamiati unaofaa au hata kutamka maneno visivyo. Hata hivyo, hali ni kinyume katika matumizi ya lugha zetu za kiasili – hasa Kiswahili. Vyombo vya habari pia havimakiniki ipasavyo katika matumizi sahihi ya baadhi ya msamiati wa Kiswahili. Hali hii hutokana na ama kuipuuza lugha hii au hata kutojua.

Hii ni hatari kwa sababu mbili. Mosi mbali na kupotosha umma,vyombo vya habari vinavyoparaganya Kiswahili huwa vinaupiga mhuru msamiati unaotumika vibaya kukubalika miongoni mwa umma kwa sababu ya ushawishi wao mkubwa. Katika makala hii, nitaangazia baadhi ya maneno ambayo hutumiwa vibaya  na vyombo vya habari pamoja na wazungumzaji wengine wa Kiswahili. Watu wengi kwa mfano – wakiwemo wanahabari hutumia msamiati  'jambazi’ na jangili kama visawe au maneno yenye maana sawa.

Fauka ya hayo, maneno haya hutumia maneno haya nje ya maana zao sahihi. Kwa mfano, utamsikia mtu akisema, “Majangili yamevamia mkahawa jijini Mombasa”. Au watu wengine husema, “Majangili yameiba nguo zilizokuwa zimeanikwa nje ya nyumba.” Matumizi ya neno jangili katika mifano hii miwili sio sahihi.

Jambazi  maana yake ni jitu janja sana linalowalaghai watu  na kuwaibia, ni jitu lisilokuwa na huruma ambalo aghalabu hutumia mabavu katika kuiba na si mdokozi au mwizi yeyote. Maana sahihi ya neno 'jangili’ ni mwindaji haramu kwenye mbuga za kuhifadhia wanyama ambaye lengo lake ni kuwinda bila kibali kwa matumaini ya kupata ngozi, pembe au nyama ya wanyama hao ili kufanyia biashara. Kosa jingine ni matumizi ya maneno 'nona’ na 'nenepa’.

Watu wengi husikika wakisema kwamba,’ “Siku hizi Juma Namlola amenona sana.” Kwa kweli iwapo kauli hii sio ya utani, kumwambia mtu kuwa amenona sio vizuri. Binadamu hunenepa na ni wanyama ambao kunona. Msamiati mwingine unaotumiwa vibaya na vyombo vya habari ni 'tetesi’. Watangazaji wengi hudhania kuwa tetesi ni malalamiko.

Kwa mfano, “Ufujaji wa fedha za mpango wa elimu bila malipo umesababisha tetesi kutoka kwa makundi mbalimbali ya wanaharakati.” Kauli hii sio sahihi iwapo wanahabari wanamaanisha kwamba kufujwa kwa fedha za mpango huo zimesababisha hali ya kutoridhika. 'Tetesi’ kwa hakika ni uvumi.

Kwa mfano, kulikuwa na tetesi kwamba  rais wa Marekani, Barak Obama alikataa kuzuru Kenya kwa sababu ya viongozi wa serikali ya muungano kutowajibika katika kutekeleza ajenda ya nne ya marekebisho nchini. Vilevile vyombo vya habari na hata wazungumzaji hutumia visivyo neno 'jihami’.

Kwa mfano, 'Majambazi waliojihami (?) kwa bunduki walivamia benki ya Equity mjini Maua na kutoweka na bunda la noti’.Neno jihami hapa limetumika visivyo – huku anayelitumia kwa njia hii akimaanisha kuwasilisha fahiwa ya 'majambazi wenye silaha’. Aidha, baadhi ya vyombo vya habari hutumia dhana ya 'mkurupuko’ wa maradhi  kumaanisha 'mlipuko’ wa maradhi.

Utamaduni

Neno 'kukurupuka’ lina fahiwa ya dhana ya Kiingereza ya 'stampede’. Isitoshe, neno 'utamaduni’ hutumiwa na watu wengi  kwa maana ya  'asilia’ au 'kienyeji’.

Imekuwa kawaida kuwasikia watu wakisema au kuzungumza kuhusu ngoma za utamaduni  wakiwa na maana ya ngoma za kiasili. Utamaduni kwa hakika maana yake ni ustaarabu, maendeleo ya kijumuia na fani mbalimbali zinazohusiana na mambo hayo – tabia, mila, desturi,lugha, mapishi, imani, matamanio, mbeko, mavazi na kadhalika.

Ili kuepuka makosa haya ambayo yanakiparaganya Kiswahili tulivyotaja awali, wanafunzi, watumiaji wa lugha hii, walimu na hata wanahabari wanapaswa ama kufanya utafiti wanapokuwa na shaka kuhusu neno fulani, kuangalia kamusi inasema nini au hata kuwauliza wataalamu.

Ni salama kila mara kukaa kimya kuhusu jambo usilolielewa na watu wakachukulia kwamba hulijui kuliko kuzungumza au kuandika kitu usichokijua na kuondolea mbali shaka ya watu hao. Isitoshe, kuuliza si ujinga!

bitugi@yahoo.com