Uwazi unahitajika katika tuzo ya fasihi

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Thursday, October 3  2013 at  12:06

Kwa Muhtasari

Ingawa tuzo ya Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta imekuwa ikitolewa kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, pana haja ya kuanza kuuliza maswali fulani ya kimsingi ambayo labda majibu yake yatatusaidia kuirejeshea hadhi tuzo hiyo.

 

MAKALA ya kumi na sita ya Maonyesho ya Kimataifa ya Vitabu yalimalizika jijini Nairobi juma lililopita. Maonyesho hayo huandaliwa na Chama  cha Wachapishaji cha Kenya  (KPA) kila mwaka. Ingawa makala ya mwaka huu yaliwavutia wachapishaji wengi, wakereketwa wa wapenzi wa vitabu hawakufika kwa wingi kutokana na shambulizi la ugaidi majuma mawili yaliyopita.

Kilele cha maonyesho hayo  kilikuwa ni utuzaji wa waandishi bora wa vitengo mbalimbali vya fasihi ya Kiswahili na Kiingereza kwa kuwapa Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta 2013.

Tuzo hii iliyoasisiwa mnamo miaka ya 1970 ndiyo tuzo ya kifahari ya kifasihi Afrika Mashariki na Kati. Vitengo ambavyo huwaniwa kila baada ya miaka miwili ni pamoja na fasihi ya watu wazima (Kiswahili na Kiingereza), fasihi ya vijana (Kiswahili na Kiingereza) na kitengo cha fasihi ya watoto  katika lugha hizo mbili.

Ingawa tuzo hii imekuwa ikitolewa kwa zaidi ya miongo mitatu sasa, pana haja ya kuanza kuuliza maswali fulani ya kimsingi ambayo labda majibu yake yatatusaidia kuirejeshea hadhi tuzo hiyo ambayo imepewa jina la mwanzilishi wa taifa hili – hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Je, mchakato mzima wa uteuzi, tathmini na uwasilishwaji wa tuzo hii unafanywa kwa njia ya haki?

Mbona ripoti za jopo la majaji  wanaotathmini na kutoa maamuzi ya tuzo hiyo hayatolewi hadharani?

Je, jopo hilo lina majaji wanaoelewa barabara fasihi ya Kiswahili? Ikiwa jibu ni ndio, mbona vitabu vizuri vya fasihi  ya Kiswahili ambavyo huwasilishwa  kuwania tuzo hiyo huishia hata kutoteuliwa kuwa kwenye orodha fupi ya kazi bora?

 

Heri subira

Mfano wa riwaya nzuri ambayo iliwasilishwa kuwania tuzo hiyo mnamo 2011 ni Heri Subira ya Omar Babu (Oxford University Press).

Ajabu ni kwamba, riwaya hiyo hata haikuteuliwa na majaji. Je, sababu ziliwahi kutolewa kuhalalisha hatua hiyo. Heri Subira kwa maoni yangu ni mojawapo wa riwaya bora za Kiswahili kuwahi kuandikwa. Je, mbona vitabu vingi ambavyo vimewahi kushinda  Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta    havichangamkiwi  na wasomaji – kuakisi ubora wao kifasihi?

Ni muhimu pia kutaja kwamba ipo haja ya fedha za Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta kuongezwa kutoka Sh75,000 anazotuzwa mshindi katika vitengo vya fasihi ya watoto na ya vijana kufikia kiwango kizuri cha fedha kinachoweza kumliwaza mwandishi ambaye huchangia sana katika maendeleo ya jamii.

Aidha, kiwango cha hela kwenye kitengo cha fasihi ya watu wazima kwenye tuzo hiyo kinapaswa kuongezwa na kuzidi Sh150,000.

Ni jambo la kukatisha tamaa kwamba waandishi ambao ni viungo muhimu katika utamaduni na maendeleo ya jamii hawanufaiki mno kutokana na jasho lao.

Vilevile ni kinaya kwamba ingawa Tuzo hii inahusishwa na jina la rais wa kwanza wa taifa hili – Mzee Jomo Kenyatta, kiasi hicho cha fedha ni kidogo mno kuhusishwa na jina kubwa kama hilo.

Kwa hiyo, ili Tuzo ya Fasihi ya Jomo Kenyatta iweze kudumisha hadhi yake stahiki katika eneo la Afrika Mashariki na Kati, ipo haja ya mchakato mzima wa utoaji wa tuzo yenyewe kufanywa kwa njia ya uwazi, haki na ukweli.

La sivyo, waandishi wanaotuzwa  bila maadili haya ya kimsingi kufuatwa watakuwa wanadanganywa kwamba wanachangia maendeleo ya fasihi – ilhali kazi zao ni chapwa na za masafa mafupi.

Uandishi sawa na tanzu nyingine za sanaa una viwango. Kazi zinazotuzwa basi baada ya kila miaka miwili lazima zionekane na kujidhihirisha wazi kustahili tuzo hii.

Aidha, wachapishaji wa vitabu wanapaswa kuwa katika msitari wa mbele kudhibiti na kudumisha viwango vya fasihi bora ili kuweza kuakisi hali halisi ya uandishi katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa fasihi ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

ematundura@chuka.ac.ke