Lugha ya Kiswahili itafaa Afrika Mashariki

Imepakiwa Thursday October 31 2013 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Si suala la mjadala tena kwamba lugha inayofumbata hisia za wenyeji wengi wa Afrika ya Mashariki ni Kiswahili. Kwa hiyo, ni upumbavu wahakiki kuifumbia macho fasihi ya Kiswahili ambayo inazidi kupanuka kila uchao.

KATIKA kongamano la wataalamu wa lugha  lililofanyika jijini Nairobi mnamo Septemba mwaka huu, mwandishi mahashumu, Prof Euphrase Kezilahabi wa Tanzania alishangaa kwamba, ingawa Kiswahili ni lugha iliyochangia sana katika  kuenea kwa dini, elimu na kufanikisha biashara Afrika ya Mashariki na kati kwa muda mrefu, haijasaidia sana kuleta umoja na muumano maridhawa katika eneo hili. Kadhalika, kwenye kongamano hili, wataalamu wawili na watunzi wapevu wa fasihi ya Kiswahili – Prof John Hamu Habwe na  Prof Kithaka wa Mberia, wa Chuo Kikuu cha Nairobi walilalamika kwamba, wahakiki wa fasihi kwa muda mrefu wamekuwa wakiipuuza fasihi ya Kiswahili na kuiweka pembezoni katika taaluma nzima ya uhakiki. Mdahalo anaouzua Prof Euphrase Kezilahabi si mgeni – bali umewahi kuwavutia wasomi, wanasiasa, wanahistoria na hata wanahabari.

Si swala la mjadala tena kwamba lugha inayofumbata hisia za wenyeji wengi wa Afrika ya Mashariki ni Kiswahili. Ingawa watu wa mataifa haya waligawanywa kwa kuwekewa mipaka na wakoloni kwa minajili ya wakoloni hao kukidhi mahitaji yao ya kisiasa na kiuchumi, kimsingi watu wa eneo hili wana historia na tamaduni zilizokurubiana.

Sina hakika iwapo Prof Kezilahabi amekwisha kusoma vitabu vitatu ambavyo nafikiri vinaweza kujibu swali lake. Vitabu hivyo ni Swahili State and Society: The Political Economy of ana African Language (Alamin Mazrui na Ali Mazrui), The Power of Babel (Mazrui na Mazrui), Kiswahili: Past, Present and Future Horizons (Rocha Chimerah), na Language Policy in East Africa (Ireri Mbaabu). Katika Swahili State and Society, Prof Ali Mazrui na Prof Alamin Mazrui wanahoji kwamba ufuasi watu katika makabila yao bado ni mkubwa sana Afrika kwa jumla na hasa Afrika ya Mashariki.

Hali hii ilidhihirika katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika Machi mwaka huu – ambapo tuliona watu wakiamini sana vyama vya kisiasa kwa misingi ya ukabila bila kutilia maanani sera za vyama hivyo. Aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw Raila Odinga alikuwa na wafuasi wengi kutoka watu wa Kabila lake, huku rais Uhuru Kenyatta akiwa na wafuasi wengi kutoja jamii yake ya Agikuyu, naye naibu wake Wiliam Ruto akiwa na wafuasi wengi kutoka kwa jamii yake ya Wakalenjin.

Huku Prof Kezilahabi akiwa ana wasiwasi kwamba Kiswahili bado hakijafanikiwa kuunganisha watu wa Afrika ya Mashariki, Prof Chimerah ana mtazamo tofauti. Ameipanulia mawanda lugha hii na kuipigia upatu iwe lingua franka ya bara la Afrika. Mtazamo wa Prof Ireri Mbaabu wa Chuo Kikuu cha Kenyatta kuhusu suala hili ni kwamba, mikakati ya kisera kuhusiana na lugha  katika mataifa ya Afrika Mashariki ni tofauti. Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Tanzania.

Hivi majuzi, serikali ya Kenya ilikikweza hadhi Kiswahili kuwa lugha rasmi  sambamba na Kiingereza – licha kwamba bado Kiswahili ni lugha ya taifa. Nchini Uganda, Kiswahili bado hakijapokelewa vizuri kwa sababu kinaendelea kupata ushindani mkubwa kutokana na lugha ya Luganda. Isitoshe, kwa muda mrefu, Kiswahili nchini humo kimekuwa kikipigwa vita kwa sababu kilihusishwa na ukatili wa wanajeshi. Hatua ya Kenya kurasimisha Kiswahili sambamba na Kiingereza ni tamko la kisera.

Kuendeleza Kiswahili

Hadi sasa, hatujaona hatua za kimakusudi za kulifanyia kazi tamko hili. Kenya, haina chombo rasmi cha kiserikali kinachoweza kutekeleza majukumu ya kuendeleza Kiswahili kimakusudi. Jukumu hili limeachiwa watu binafsi na vyombo vya habari kama vile gazeti la Taifa Leo.  Kuhusu suala la kuwekwa pembezoni kwa fasihi ya Kiswahili na wahakiki wa fasihi wanaozingatia mno fasihi ya Kiingereza, ni hali ya kusikitisha mno. Wasichokifahamu wahakiki hawa ni kwamba, fasihi ya Kiswahili imepiga hatua mno hasa kuhusiana na utuzi wa kimajaribio.

Kwa hiyo, ni upumbavu wahakiki kuifumbia macho fasihi ya Kiswahili ambayo inazidi kupanuka kila uchao. Kimsingi, kinachozuia Afrika Mashariki kuungana na kuwa na mshikamano anaoutaka Prof Kezilahabi ni tofauti za kisiasa, kiuchumi na kisera ambazo hazijawianishwa. Muungano wa Afrika ya Mashariki utakapoimarika, labda ndipo mataifa ya eneo hili yatakapofikia mshikamano wa kuridhisha utakaofanikiswa kwa matumizi ya lugha ya Kiswahili.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

ematundura@chuka.ac.ke

Share Bookmark Print

Rating