Mandela ametufunza jinsi ya kuandika historia

Imepakiwa Friday December 13 2013 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Watakapohesabiwa basi watu walioacha taathira kubwa mno ulimwenguni, Mzee Nelson Mandela hatakosa kuhesabiwa. Atatoka wapi mwingine kama yeye?

KWA muda wa miezi mitatu hivi, ulimwengu ulisubiri kwa hamu na ghamu kifo cha  shujaa wa Afrika kusini – Nelson Mandela Madiba. Mzee Mandela alilazwa hospitalini baada ya kupata maambukizi ya mapafu. Waganga waliposhindwa na hatimaye kuinua mikono, alirudishwa nyumbani kwake ambako hatimaye alijiondokea ulimwenguni kimyakimya wakati ambapo ulimwengu ulikuwa umekwisha ‘kusahau’  kusubiri kifo chake kilichokuwa kinasubiriwa.

Vyombo vya habari – ambayo vilikuwa vinatarajia kuondoka kwa jagina huyu duniani viliandaa mapema taarifa kuhusu maisha ya jagina huyu na kuzichapisha mara moja pindi tu tanzia hiyo iliposambaa ulimwenguni mithili ya moto kwenye biwi la nyasi kavu wakati wa kiangazi. Ulimwengu uliamkia taarifa za tanzia za Mzee Mandela kwa mshangao mkubwa hali iliyoonyesha kwamba haukutosheka na muda wa miaka 95 aliyoishi Mandela.

Pembe zote za dunia – wakiwemo makaburu wanafiki waliowatesa raia wa Afrika kunisi wanaelekea kukubaliana kwamba Mzee Mandela hakuwa mtu wa kawaida. Je, ni mhimili upi mkuu au ni kiunzi gani kilichomfanya Mzee Nelson Mandela  kuacha taathira kubwa kuwahi kuonekana mpaka sasa katika siku za hivi karibuni? Katika kitabu chake, No Easy Walk to Freedom (1965), Mzee Mandela anasema hivi kwenye blabu: “Katika maisha yangu, nimejitolea kwenye mapambano haya ya Waafrika. Nimekwisha kupigana dhidi ya  utawala na ubaguzi wa rangi dhidi ya Wazungu na vilevile ule wa watu Weusi.

Nimeishi na matumaini makubwa ya kujiri kwa jamii huru yenye demokrasia ambapo watu wote wanaishi kwa amani na utengamano na wakiwa na nafasi sawa. Ni azma ambayo ninatumainia  kuishi na kuitimiza. Lakini ikiwa kutakuwa na haja, ni azma ambayo niko tayari kuifia.” Mzee Mandela sasa amekwisha kufa. Je, azma ndoto hii yake ilikwisha kutimia? Jibu la swali hili ni ndio na la. Ni ndio kwa sababu kwa kiasi fulani, aliweza kuikomboa Afrika ya kusini, akatawala kwa miaka mitano – kisha sawa na hayati Mwalimu Kambarage Nyerere, akang’atuka kutoka uongozini. Licha ya kuchukua hatua hii ya kistaarabu, bado kuna viongozi wengine katika bara hili jeusi ambao wamekwamilia madaraka kwa minajili ya kutosheleza maslahi yao ya kibinafsi.

Mifano inayotajika kwa urahisi ni Yoweri Museveni wa Uganda na Robert Mugabe wa Zimbabwe. Jibu ni hapana kwa sababu mataifa mengi barani Afrika yanakabiliwa na tisho la utawala mbovu wa ukandamizwaji wa wanyonge na wachache matajiri pamoja na wasomi teule.

Kifo cha Mzee Nelson Mandela hivyo basi kinapaswa kuwa mwamko mpya kwa viongozi wengi barani Afrika ambao bado hawajazinduka na kufahamu kwamba siku moja, wataporomoshwa na wimbi la wakati. Mzee Mandela, sawa na mhusika Kinjeketile wa tamthilia ya Ebrahim Hussein, Mashetani alizaa neno  ambalo lilikuwa kubwa kuliko aliyelizaa.

Kusameheana

Katika utu wake na udhaifu wake, kiongozi huyu alidhihirisha wazi kwamba ulimwengu unaweza kuwa bora zaidi iwapo watu watasameheana na kuishi pamoja na kukirimiana kwa hali na mali; kwamba inawezekana mtu akaleta mabadiliko makubwa kwa kushirikiana na watu wengine na kupigana dhidi ya dhuluma bila kutarajia manufaa yoyote ya kibinafsi.

Historia itakapoandikwa hatimaye, itabainika wazi kwamba watu sampuli ya Mzee Mandela ni adimu sana kutokea katika sayari hii yetu iitwayo dunia. Lakini pia tunapomweka kiongozi huyu kwenye mizani ya majagina katika jamii zetu za Kiafrika na yingine ulimwenguzi inabainika wazi kwamba watu sampuli ya Mandela huzuka katika mazingira ya kutetea Wanyonge na kwamba vifo vyao vinapotokea, hutikisa utando wa kijamii kwa namna moja au nyingine.

Katika jamii ya Uswahilini, tuna Fumo Liyongo; katika jamii ya Wayahudi, tuna Yesu na akina Musa. Katika Mashariki ya Kati, tuna majagina kama Gilgamesh. Watakapohesabiwa basi watu walioacha taathira kubwa mno ulimwenguni, Mzee Nelson Mandela hatakosa kuhesabiwa.

Atatoka wapi mwingine kama yeye? Ni matumaini yangu kwamba kifo cha Mzee Nelson Mandela hakitasimamisha kamwe gurudumu la mapambano ya haki na usawa ulimwenguni. Ikiwa mapambano hayo hayakufua dafu katika uhai wake; yatakuja kunanikiwa siku moja. Mradi tusikate tama.

ematundura@chuka.ac.ke

Share Bookmark Print

Rating