Abdulaziz ana ndoto kuu kuhusu Kiswahili

Bitugi Matundura Na Bitugi Matundura

Imepakiwa - Tuesday, July 1  2014 at  18:21

Kwa Muhtasari

Prof Abdulaziz anatabiri kwamba, miaka ishirini hivi ijayo, Kiswahili kitakuwa kimefikia hadhi ya kutekeleza mambo yote ya taifa letu ikiwemo elimu, sayansi na kadhalika.

 

MTAALAMU wa lugha na mhadhiri mkongwe wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Profesa Mohamed Hassan Abdulaziz Mkilifi ni mmoja wa wasomi wanaoheshimika sana barani Afrika. Aliasisi Idara ya Isimu na Lugha za Kiafrika katika kiwango cha Chuo Kikuu nchini Kenya mapema miaka ya 1970. Somo la Kiswahili lilianza kuwa maarufu katika idara hiyo na wataalamu wengi wamekwisha kupitia katika mikono yake.

Je, mtaalamu huyu ana maoni na fikra zipi kuhusiana na masomo ya Kiswahili katika vyuo vikuu? Je, ana maoni gani kuhusu Kiswahili katika utambulisho na maendeleo nchini Kenya na kwingineko, Kiswahili katika maendeleo ya kisasa ikiwemo tafsiri na Teknohama? Mnamo Novemba 9, 2009,  mtaalamu wa tafasiri marehemu Profesa Naomi Luchera Shitemi alifanya mahojiano na Profesa Abdulaziz.

Kwa bahati nzuri, mtaalamu huyo alichapisha mahojiano hayo kwenye kitabu chake, Kubidhaaisha na Kuwezesha Lugha kama Sarafu ya Kiuchumi na Kijamii: Kielelezo cha Taaluma za Kiswahili na Tafsiri (Moi University Press, 2011) ambacho nimekwisha kumaliza kukisoma. Mwandishi wa kitabu hiki ameambatisha mahojiano baina yake na Profesa Abdulaziz ambapo anazungumzia kwa uketo na kina kikubwa sana masuala tuliyokwisha kuyataja katika mwanzo wa makala haya. Profesa Abdulaziz anavuta taswira ya hali ilivyokuwa tangu enzi ya Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki iliyokuwa na Idara ya Kiswahili na Isimu na wanafunzi wa kwanza  aliowafundisha  - mathalan Ebrahim Hussein, Euphrase Kezilahabi, Ruth Mfumbwa Besha (marehemu), Clement Maganga na Mugyabuso Mulinzi Mulokozi.

Anasema kwamba wanafunzi hawa walikuwa na ari kubwa sana – na kwa kweli wengi waliishia kuwa maprofesa wa fasihi na isimu ya Kiswahili, huku wengine wakiishia kuwa waandishi  hodari sana wa tamthilia na riwaya. Ebrahim Hussein kwa mfano alitunga tamthilia zilizoleta mabadiliko makubwa sana katika utanzu huo. Hizi ni pamoja na Kinjeketile na Mashetani. Euphrase Kezilahabi kwa upande mwingine anadaiwa na wahakiki kuwa mmoja wa watunzi mahashumu wa riwaya ya Kiswahili Afrika Mashariki na Kati. Tungo zake  ni pamoja na Kichwamaji, Rosa Mistika, Gamba la Nyoka, Nagona na Mzingile. Profesa Abdulaziz anasema kwamba wataalamu hawa walitoa fasihi ambazo mtu anaweza akachukulia kuwa fasihi za kilimwengu.

Anakiri kwamba profesa mmoja kutoka Ufini aliwahi kumwambia kwamba fasihi ya Kiswahili ilikuwa imeafikia viwango vya fasihi ya kilimwengu kwa sababu ina kiwango cha juu sana katika habari za wahusika, ploti na hata maudhui. Kauli hii ni ya kweli – hata bila kusubiri mtaalamu wa nje kutambua jambo hilo. Baada ya kuondoka katika Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki mnamo miaka ya 1970, Profesa Abdulaziz alianzisha Idara ya Isimu la Lugha za Kiafrika katika Chuo Kikuu cha Nairobi – na mwanafunzi wake wa kwanza aliyefanya shahada ya uzamili ni Profesa Chacha Nyaigotti Chacha ambaye alikuwa wa kwanza kuandika tasnifu yake kwa kutumia Kiswahili.

Maarifa

Hatua hiyo ilifungua milango ambapo wataalamu wa baadaye walianza kuandika tasnifu zao za viwango vya uzamili na uzamifu kwa kutumia Kiswahili. Hii inadhihirisha kwamba, Kiswahili kinaweza kutumika kuelezea maarifa yoyote yale yawayo kikamilifu. Profesa Abdulaziz anakariri kwamba asilimia tisini ya shughuli za uchumi nchini Kenya zinaendelezwa kwa lugha za kiasili na Kiswahili.

Katika maeneo ya viwandani na jua kali na hata polisi kwa mfano, wafanyakazi huongea Kiswahili. Kiingereza – ambayo ndiyo lugha inayotumiwa na wasomi teule hutumika katika uchumi wa juu kama vile kwenye mabenki. Prof Abdulaziz anatabiri kwamba, miaka ishirini hivi ijayo, Kiswahili kitakuwa kimefikia hadhi ya kutekeleza mambo yote ya taifa letu ikiwemo elimu, sayansi na kadhalika.

Ukweli ni kwamba Kiswahili ni sasa ni lugha ya kimataifa inayozungumzwa na takriban watu milioni 200  wengi wao wakiwa wakazi wa Afrika Mashariki na mataifa ya Maziwa Makuu. Lugha hii inazidi kupata imaarufu kila uchao katika teknohama na mawasiliano mengine ya aina hiyo.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka