Kenya yahitaji asasi ya kudhibiti istilahi mpya

Imepakiwa Tuesday January 13 2015 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Mojawapo ya juhudi kuu  zinazoendelea kufanywa hivi  leo na wataalamu wa Kiswahili ni ukuzaji wa istilahi. Mawanda ya matumizi ya Kiswahili, sawa na lugha nyingine yoyote ulimwenguni yanaendelea kupanuka kila uchao - hasa kwa sababu ya maendeleo ya kasi yanayojiri katika nyanja za sayansi  na teknolojia.

MOJAWAPO ya juhudi kuu  zinazoendelea kufanywa hivi  leo na wataalamu wa Kiswahili ni ukuzaji wa istilahi. Mawanda ya matumizi ya Kiswahili, sawa na lugha nyingine yoyote ulimwenguni yanaendelea kupanuka kila uchao - hasa kwa sababu ya maendeleo ya kasi yanayojiri katika nyanja za sayansi  na teknolojia.

Jukumu la ukuzaji wa istilahi na usambazaji zinafanywa na mashirika kama vile Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) nchini Tanzania na Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (zamani ikijulikana kama Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI), katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – nchini Tanzania.

Hadi sasa, Kenya bado haina chombo mahususi cha kitaaluma au kiserikali kinachotwikwa  wajibu huu.  Jukumu la kubuni istilahi na kuzisambaza ama limeachiwa watu binafsi, vyombo vya habari au watu binafsi.

Baadhi ya wanataaluma ambao wanatajika kwa urahisi katika ulingo wa kubuni istilahi mpya za Kiswahini ni pamoja na Mzee Sheikh Ahmad Nabhany wa Mombasa, Profesa Rocha Mzungu Chimerah wa Chuo Kikuu cha Pwani, Profesa Kyallo Wadi Wamitila wa Chuo Kikuu cha Nairobi miongoni mwa wataalamu wengine.

 

Ukosefu wa chombo cha kiserikali

Wataalamu wanaojishughulisha na tathmini ya istilahi na leksikoni za Kiswahili wamewahi kulalamika kwamba, ukosefu wa chombo cha kiserikali na hata jopo la wataalamu wanaoweza kutwikwa jukumu la kudhibiti mchakato mzima wa kubuni, kusawazisha na kusambaza istilahi za Kiswahili nchini Kenya ni hatari.

Kwa nini? Kwa sababu mchakato huu unaweza kutekwa nyara na watu wachache wanaojitakia makuu na kuuvuruga au kupotosha shughuli nzima. Kwa bahati nzuri, nchini Kenya, hali hiyo bado haijatokea. Hadi sasa, istilahi zilizokwisha kubuniwa na Mzee Sheikh Nabhany kama vile 'tarakilishi’ na 'runinga’ zimekwisha kubalika.

Hata hivyo, Mzee Nabhany kwa muda mrefu amekuwa na wasiwasi kwamba Kiswahili kinakopa mno istilahi kutoka kwa lugha nyingine za kigeni na kuzifanyia marekebisho ili zichukue muundo wa Kiswahili.

Mapandekezo ya mtaalamu huyu aghalabu ni kuwa, aghalabu wataalamu wa Kiswahili wanapaswa kwanza kupekuapekua na kusaka lahaja zote za Kiswahili pamoja na lugha nyingine za Kiafrika kubaini iwapo dhana fulani zipo katika lugha hizo kabla ya kukimbilia kukopa.

Anachopendekeza Mzee Sheikh Nabhany ni kwamba Kiswahili kinapaswa kukuzwa mumo kwa mumo kwa kutumia kanzi ya misamiati na dhana za lugha zetu za kiasili badala ya kukopa mno kiasi kwamba lugha hii inaweza kupoteza upekee wake. Baadhi ya misamiati iliyokopwa kutoka lugha zetu za kiasili na ambayo imekubalika katika Kiswahili sanifu ni pamoja na  'ikulu’, 'kabwela’ na 'bunge (Kinyamwezi), 'kitivo’ (Kipare), na kadhalika.

 

Mapendekezo ya Nabhany

Hata hivyo, mapendekezo ya Mzee Nabhany – ingawa yana mashiko, haiyumkiniki yatekelezwe kwa urahisi. Sababu ni kwamba katika ulimwengu huu ambao umegeuka kuwa kijiji kwa sababu ya utandawazi, mipaka ya kijiografia imekwisha kufutwa. Maendeleo makubwa na ya kasi yanajiri katika sayansi na teknolojia hivi kwamba vifaa na dhana nyingi zinazuka kila uchao.

Kwa hivyo, dhana hizi zinahitaji kutafutiwa istilahi haraka mno. Na njia ya haraka ya kuzua istilahi hizi ni kwa njia ya ukopaji na utohozi.  Lugha zetu za asili huenda zisiwe na dhana ngeni kama vile kompyuta – ambazo hapo awali hazikuwa katika utamaduni wetu. Lugha huweza tu kuwa na majina na msamiati wa dhana zinazopatikana katika utamaduni wake.

Kwa sababu ya mtafaruku unaoweza kuzuka katika matumizi ya istilahi miongoni mwa vyombo vya habari na hata baina ya wataalamu wa Kiswahili, ipo  haja ya dharura ya Kenya kuwa na asasi inayoweza kutwikwa jukumu la kudhibiti mchakato mzima wa kubuni, kusawazisha na kusambaza istilahi mpya.

 

Matundura ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

Share Bookmark Print

Rating