Kiswahili na maazimio ya hadi mwaka 2030

Imepakiwa Saturday January 24 2015 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Lugha ni mojawapo wa raslimali kubwa ambayo inaweza kutumiwa na jamii yoyote ile iwayo katika kutekeleza na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

LUGHA ni mojawapo wa raslimali kubwa ambayo inaweza kutumiwa na jamii yoyote ile iwayo katika kutekeleza na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.

Lugha  ndiyo chanzo cha maisha na mamlaka aliyo nayo mwanadamu.

Kutokana na ukweli huu, lugha ndio wenzo na ufunguo wa maendeleo ya jamii na chombo madhubuti kinachoweza kutumiwa kuiwezesha Kenya kuafikia  Rajua yake ya 2030.

Iwapo raia watajihusisha kikamilifu na kwa ufanisi mkubwa katika nyanja zinazopewa kipaumbele kwenye maazimio husika ya maendeleo kufikia 2030 – hususan  kilimo, maendeleo ya viwanda, biashara, utalii na sekta nyingine za fedha hasa benki, watahitajika kupata maarifa na ujuzi.

Kwa bahati mbaya, maarifa haya hayamo katika lugha zinazozungumzwa na  idadi kubwa ya Wakenya. 

Hali hii inatulazimu sisi wasomi kusaka na kuonesha kiungo kilichoko baina ya lugha na maendeleo hasa kuhusiana na Rajua ya Kenya ya kupiga hatua kubwa katika maendeleo kufikia 2030.

Ni bayana kwamba Kiswahili na Kiingereza  ndizo lugha zinazotumiwa kwa mapana katika maisha ya Wakenya ya kila siku.

Hata hivyo, raia wengi huelewa Kiswahili zaidi kuliko Kiingereza.

Kwa hivyo, tunatarajia kwamba lugha  itakayofanikisha mawasiliano ya raia na wanavijiji katika  ngazi za Taifa na utawala ujao wa kaunti itakuwa ni Kiswahili.

Maafisa na wafanyakazi  wa serikali katika ngazi hizo wana uhuru wa kutumia lugha zao za asilia – lakini kuendesha shughuli za maendeleo katika ngazi hizo kwa Kiswahili  kutaleta natija kubwa sana.

Kiswahili kimekwezwa hadhi sawa na Kiingereza

Kwa hivyo, tunatarajia kwamba mifumo ya utawala wa kaunti itakapoanza kutekelezwa, Serikali itahakikisha kwamba Mipango ya Maendeleo inapatikana katika lugha hizi mbili; yaani Kiswahili na Kiingereza.

Kwa kuwa Kiswahili kimekwisha kwezwa hadhi na kuwa lugha rasmi sambamba na Kiingereza, uamuzi huu wa kisera unamaanisha kwamba nyaraka na stakabadhi zote za Serikali  zenye taarifa kuhusu ukuaji wa uchumi zitahitajika kuwa katika lugha hizo – Kiswahili na Kiingereza.

Stakabadhi ambazo kwa sasa zinapatikana katika Kiingereza zitahijajika kutafsiriwa kwa Kiswahili.

Kadhalika, Serikali itahitajika kuhakikisha kwamba huduma za nyanjani na vifaa – hasa stakabadhi za kutoa mafunzo hayo kwa umma zinaandikwa kwa Kiswahili na katika lugha nyingine za asili.

Vilevile, Serikali itahitajika kuwasilisha kwa Kiswahili mafunzo kwa umma kuhusu mikakati na mbinu za maendeleo katika lugha wanayoielewa na kuifahamu kwa urahisi – ambayo ni Kiswahili.

Kitatumiwa kuboresha utendakazi

Watumishi wa umma watakuwa na haki; kulingana na majukumu wanayoyatekeleza kutumia Kiswahili au Kiingereza katika kufanikisha utendakazi wao.

Ili kuhakikisha kwamba raia wanashiriki kikamilifu katika maendeleo, serikali italazimika kuanzisha vitengo vya Kiswahili katika ngazi za kaunti na taifa.

Mitazamo hii inatuchochea kuanza kuona Kiswahili kama raslimali inayoweza kutumiwa kufanikisha ajenda za maendeleo ya taifa hili.

Mataifa mengi yaliyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya viwanda kama vile Uchina, Japani na hata Malaysia hayategemei pakubwa sana matumizi ya lugha za kigeni katika kusukuma gurudumu la maendeleo yao.

Sekta ya juakali nchini Kenya kwa mfano ina watu wanaounda magari na vifaa vingine ingawa hawajui Kiingereza.

Je, lugha inayotumiwa katika harakati za kukarabati magari kwa mfano ni ipi? Bila shaka ni Kiswahili.

Kwa hivyo, ipo haja ya dharura ya Kenya kuanza kutafakari upya kuhusu nafasi ya lugha – hasa Kiswahili katika kufanikisha Rajua yake ya 2030.

Bila kutilia maanani suala la lugha, huenda ufanisi wa haja usiwahi kupatikana.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu  cha Chuka

mwagechure@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating