Mazrui awataka wataalamu waunde msamiati unaofaa karne ya 21

Imepakiwa Thursday January 29 2015 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Prof Alamin Mazrui anatoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kujifungata masombo kuunda msamiati na istilahi za Kiswahili ambazo zitatufaa zaidi katika Karne ya 21.

MNAMO 2010, nilihudhuria kongamano la kimataifa la Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Pwani, Kaunti ya Kilifi.

Kikao hicho kilichowaleta pamoja wasomi, wakereketwa na  maashiki wa Kiswahili kutoka pembe mbalimbali za ulimwengu kiliandaliwa na Chama cha Kiswahili cha Taifa (CHAKITA) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Pwani. Mada kuu ya kongamano hilo ilikuwa ni  tafsiri na ukalimani.

Miongoni mwa wataalamu wa Kiswahili waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Prof Alamin Mazrui  (Chuo Kikuu cha Rutgers), Prof Mohamed Hassan Abdulaziz (Chuo Kikuu cha Nairobi ), Prof Rocha Mzungu Chimerah,  ambaye alikuwa mwenyeji wa kongamano hilo na Prof Kimani Njogu.

Nilikuwa makini sana kusikiza mijadala ya wasomi hao kwa sababu mbili. Kwanza, baadhi yao, kwa mfano Prof Abdulaziz  walikuwa walimu wangu katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Inakuwa ni tajriba nzuri wakati ambapo mtu anapokutana na  walimu wake kwenye vikao kama hivyo.

Pili, hiki ni kizazi cha wasomi ambacho kimetoa mchango mkubwa  na kuacha taathira mno katika taaluma ya Kiswahili. Wataalamu wengi wamepitia katika mikono yao.

Prof Alamin Mazrui ndiye aliyetwikwa heshima ya kutoa hotuba ya kuchochea mjadala kuhusu mada ya kongamano hilo. Alitoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kujifungata masombo kuunda msamiati na istilahi za Kiswahili ambazo zitatufaa zaidi katika Karne ya 21.

Alisema, kulikuwepo na haja ya kufanywa  juhudi za kimakusudi kusayansisha lugha za Kiafrika ili ziweze kukidhi maendeleo ya kasi yanayojiri ulimwenguni kila uchao.

Alikariri kwamba ubunifu wa kisanaa na sayansi unapaswa kupewa uzito sawa kwa sababu unatokana na kipawa kilekile kimoja. Alitahadharisha dhidi ya  ukasuku wa kukopa istilahi kutoka kwenye lugha za kigeni kupita mipaka kwa sababu kufanya hivyo kunachangia katika kusambaa kwa aina mpya ya ubeberu.

Prof Mazrui hali kadhalika alionya kwamba ipo hatari ya kutafsiri tu maandishi yanayotoka uzunguni.

Alipendekeza kuwa wataalamu wanapaswa kuwazia kutafsiri matini za Uarabuni, Uchina – kama vile kazi za Confucius na pia tungo za mwandishi kama vile Gabriel Garcia Marquez wa Colombia.

Naye Prof Mohamed Hassan Abdulaziz  aliukweza mjadala na kuuingiza katika viwango vya juu kabisa alipotoa changamoto kwamba, mataifa ya bara Afrika hayawezi kupiga hatua kubwa katika maendeleo kwa kutegemea lugha za kigeni tu.

Alitoa mifano ya mataifa ya Japan, Korea na Uchina ambayo yamepiga hatua kubwa sana katika mwana wa sayansi na teknolojia bila kuegemea lugha za kigeni. Abdulaziz aliushutumu mfumo wetu wa elimu unaopendelea watu wachache tu ambao ni wasomi teule.

Kupuuza lugha za kiasili

Alilalamika kuhusu hali ambapo licha ya  alisimia  90 ya uchumi wetu kuendeshwa kwa kutumia lugha za kiasili hususan Kiswahili na asilimia 10 pekee ikiendeshwa kwa  kutumia lugha za kigeni, lugha za asili zingali zinapuuzwa na kuonewa aibu.

Alisema, bila kutumia lugha zetu asili, 'uchumi utasalia tu kwenye mabenki’.

Alitahadharisha pia kwamba tafsiri za istilahi zinaweza kufanywa alini tukakosa mahali pa kuzitumia.

Alisema, huku lugha ya Kiingereza ikiwa ni lugha itumiayo sana muundo wa unominishaji – na lugha za Kibantu zikiwa zinaegemea sana vitenzi, pana changamoto au ndaro kubwa kwa wanataaluma wa Kiswahili kuibuka na mbinu murua za kiisimu zinazoweza kutumiwa kubuni istilahi au maneno zalishi.

Alitoa mfano wa istilahi infrastructure  - ambayo kwa Kiswahili ni amara, muundomsingi au muundombinu. Infrared itaitwaje kwa Kiswahili?” Akauliza Prof Abdulaziz.

Bitugi Matundura ni mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating