Mwandishi alipotosha wasomaji kuhusu matbaa

Imepakiwa Friday January 30 2015 | Na Bitugi Matundura

Kwa Muhtasari:

Nilivunjika moyo baada ya kukamilisha kusoma makala ya Alex Ngure na kugundua kwamba ilikuwa inapwaya na kwa maoni yangu kuonekana chapwa. Mwandishi alipotosha wasomaji kwa kuwasilisha fahiwa kwamba ‘matbaa’ ni sawa na kampuni ya uchapishaji.

NILISOMA makala ya mwalimu Alex Ngure ‘Umuhimu wa hisi na ubunifu katika uandishi’ (Taifa Leo, Januari 29, 2015 kwa jicho kali sana kwa sababu  nimekuwa katika taaluma hii kwa  takriban zaidi ya mwongo mmoja sasa. Kwa hiyo, nilitarajia kwamba mwandishi  (ambaye pia ni mtunzi wa kazi za fani hizi) angefumbata kwa uketo mawazo na taswira murua inayoweza kuwapa mwongozo maridhawa waandishi chipukizi ambao daima wanatapatapa katika kujaribu kupata dira ya kutunga kazi zinazoweza kuchapishika.

Hata hivyo, nilivunjika moyo baada ya kukamilisha kusoma makala hayo na kugundua kwamba ilikuwa inapwaya na kwa maoni yangu kuonekana chapwa. Kwa usemi mwingine, makala yake iliishia kusomeka kwa toni ya ‘bora makala’ na ‘si makala bora’.

Nitatoa sababu zifuatazo. Kwanza, mwandishi alipotosha wasomaji kwa kuwasilisha fahiwa kwamba ‘matbaa’ ni sawa na kampuni ya uchapishaji. Hii si kweli hata kidogo. Msamiati ‘matbaa’ aghalabu umekuwa ukitumika vibaya na baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya waandishi kama Bw Ngure. Maana sahihi ya ‘matbaa’ ni  mitambo au mashine  ya kupiga chapa.  Kwa hiyo, haiyumkiniki dhana ‘matbaa’ ikawa kisawe cha kampuni ya uchapishaji.

Nchini Kenya, kampuni ya uchapishaji ambayo ina matbaa yake ni Kenya Literature Bureau (KLB) ambayo ni shirika la Serikali. Kwa sababu hiyo, kitabu ambacho kimechapishwa na  KLB kitaandikwa katika mojawapo ya sehemu za  matini kwenye ukurasa tangulizi: ‘Kimetayarishwa na kupigwa chapa na Kenya Literature Bureau. Aidha kampuni ya Nation Media Group pia ina matbaa yake. Kwa hiyo, katika ukurasa wa nyuma wa Taifa Leo, huandikwa taarifa hizi :  “Hutayarishwa katika Nation Centre, Kimathi Street, na kuchapishwa  Mombasa Road, Nairobi na kampuni ya Nation Media Group.” Aidha, kampuni nyingi za uchapishaji hazina matbaa zao binafsi. Phoenix Publishers Ltd kwa mfano  hutumia matbaa kama vile Kenya Litho, Ramco Printing Works, Printpak Ltd na kadhalika kupiga chapa vitabu vyao.

Vigezo

Pili, si kweli kwamba wachapishaji wengi  chambacho Bw Ngure  hawaweki wazi vigezo na viwango  wanavyovitaka wenyewe. Katika enzi hii ya dijitali, kampuni nyingi za uchapishaji zina nyavuti (websites) ambapo hubainisha vigezo ambavyo mwandishi chipukizi au yule aliyekomaa anapaswa kufuata katika kuwasilisha mswada. Maelezo haya aghalabu huwa ni maagizo ya kimsingi yanayoweza kuwa dira kwa mwandishi. Kwa hiyo nafikiri watunzi hasa chipukizi wanaoandika kwa papara huenda wasiwe na habari kuwa kuna tovuti za aina hiyo.

Tatu, akimnukuu S.A. Mohamed, Bw Ngure alidai kwamba  ‘mwaandishi aandikapo  huanza yeye mwenyewe  kufumwa na hisi fulani ambazo hujaribu kuzitoa na kuziwasilisha  kwa njia ya maandishi kwa  hadhira yake’. Ingawa ninakubaliana kwa kiasi fulani na rai hii, sikubaliani nayo pia kwa kiasi fulani. Nilimtarajia Bw Ngure kupanua mawanda ya rai hii ya hisi kwa labda kumulika aina za hisi au misukumo ambayo inaweza kuwaongoza watunzi katika kuchukua kalamu ili kutunga kazi za kifasihi.

Ingawa waandishi wenye vipawa huongozwa na hisi za kutunga ili kujiliwaza, pana pia watunzi wengine wanaotunga kwa sababu ya hisi za kujipatia hela. Waandishi wanaoongozwa na hisi za kujipatia hela mara nyingi huishia kuwa waandishi wa ‘masafa mafupi’. Vipi? Kazi za sanaa  zinazotokana na mkabala wa aina hii huishia kuwa chapwa – na nafikiri watunzi wengi wa fasihi ya Kiswahili nchini Kenya wamo katika pote hili.

Bitugi Matundura, mfasiri wa tungo za Barbara Kimenye za Moses series ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Chuka

mwagechure@gmail.com

Share Bookmark Print

Rating